Manchester, Uingereza

Mabingwa wa Ligi Kuu nchini Uingereza, Klabu ya Manchester City, wametangaza kupata faida ya kiasi cha pauni milioni 500.5 sawa na Sh bilioni 1.5 kwa msimu wa 2017/18 na kuvunja rekodi ya mapato tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 1880.
Pia klabu hiyo imetangaza kuwa tangu kuwasili klabuni hapo kwa Kocha wake, Pep Guardiola, wamefanikiwa kupunguza idadi ya mishahara wanayolipwa wachezaji na kusaidia kuimarisha idara zingine na kuongeza kuwa chini ya kocha huyo msimu wa mwaka jana klabu ilifanikiwa kuweka rekodi ya kufikisha alama 100 na kutwaa ubingwa.
Klabu pia imefanikiwa kupata faida ya pauni milioni 10.4 kwa mwaka wa nne mfululizo, huku klabu hiyo ikijinasibu kupunguza mishahara ya wachezaji hadi kufikia asilimia 52.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Sheikh Mubarak, amesema klabu bado haijafikia malengo waliyojiwekea ya kuwa moja ya klabu yenye mafanikio duniani.
Mubarak amesema mwanzoni mwa uwekezaji wake klabuni hapo klabu ilipata hasara ya pauni milioni 584 kwa kipindi cha miaka sita kutokana na matumizi mkubwa ya usajili wa majina makubwa kama vile Robinho na wengineo.
Amesema katika miaka ya hivi karibuni Man City imeanza kupata ofa nyingi za TV na ushindani mkubwa wa nje na ndani ya uwanja dhidi ya klabu zingine, ambao umeendelea kuongezeka kila kukicha hasa kutoka kwa majirani zao Klabu ya Manchester United.
Amesema mbali na ushindani nchini Uingereza, pia ushiriki wa Man City katika michuano ya UEFA katika miaka ya hivi karibuni umewaweka kwenye kundi la vigogo wa soka barani Ulaya kwa kuwa kundi moja na klabu za Barcelona, Real Madrid, Bayern Munich, Liverpool na Man United.
Kabla ya Man City kuchukuliwa na Sheikh Mansour, klabu hiyo haikuwa na jina kubwa katika soka la Uingereza na Ulaya, hata hivyo hali imegeuka na kuwa tofauti kutokana na uwekezaji wa Mansour.

Mwisho

By Jamhuri