Jambo ambalo si rahisi kuacha kulitaja ni hali duni ya usalama inayowakabili watumiaji wa vyombo vya usafirishaji kutokana na kujirudia kwa ajali mbalimbali.
Watanzania tumo kwenye maombolezo ya vifo na hasara iliyotokana na ajali ya hivi karibuni ya mv Nyerere, kivuko kinachohudumia wakazi wa Kisiwa cha Ukara, Wilaya ya Ukerewe. Naandika makala hii ikiwa tayari imeopolewa miili zaidi ya 100 ya abiria waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo.
Taarifa za awali zinataja sababu ya ajali kuwa ni kuzidisha uzito wa abiria na mizigo kupita uwezo wa kivuko. Tunasubiri taarifa rasmi ya uchunguzi kubaini ukweli kabla ya kuanza kunyoosheana vidole.
Kunyoosheana vidole ni suala la msingi kabisa pale ambapo kunyoosheana vidole kunaambatana na kubaini kiini cha ajali na nini kifanyike kuepuka kujirudia.
Lakini uzoefu unatukumbusha kuwa tutaishia kunyoosheana vidole tu bila kupunguza au kusitisha tatizo. Kumbukumbu ya yaliyotokea ikianza kufifia tu na tahadhari ambazo zinachukuliwa kuzuwia kurudia kwa ajali ya aina hiyo nazo zitafifia na tutajikuta tumerudi kwenye hali ile ile ya awali ya kuhatarisha usalama wa abiria na mali zao.
Tunatibu maradhi bila kujikinga. Ni sawa na kutibu malaria bila kuondoa mazingira yanayosaidia mbu kuzaliana kwa wingi.
Hatua za kujenga mazingira ya kuzuia kujirudia rudia kwa ajali ni njia moja pekee inayoweza, kwa kiasi kikubwa, kupunguza maafa ya aina hii.
Njia moja ni kuhakikisha usimamizi wa kudumu wa utekelezaji wa sheria. Kuna vipengele vingi vya sheria za usimamizi wa matumizi ya njia za usafirishaji vinavyokiukwa kila wakati, au na watumiaji wa vyombo vya usafirishaji au na wale wanaohusika na kuhakikisha kuwa vipengele hivyo vinafuatwa.
Hatuna mfumo wa kudumu wa usimamizi wa sheria na kanuni na taratibu zinazozingatia usalama. Leo hii, kwa sababu ya kumulikwa kwa ajali ya mv Nyerere, wamiliki wa vyombo vya majini na wasimamizi wa usafiri huo watahakikisha vinabeba uzito ule ule ulioruhusiwa. Subiri mwaka mmoja upite na upo uwezekano mkubwa kuwa wamiliki na wasimamizi watasahau au kupuuza yaliyotokea na kurudia hali iliyozoeleka.
Wafuasi wa mwanafalsafa Karl Marx wanadai kuwa sheria ni mfumo unaotumiwa na dola kutetea masilahi ya tabaka la mabwanyenye au makabaila dhidi ya tabaka la wafanyakazi. Katika mfumo huo dola inatakiwa kuwa muamuzi ambaye analinda haki za pande zote mbili, lakini wafuasi wa falsafa ya Marx hawaamini kuwa inawezekana kulinda usawa kati ya wanyonyaji na wale wanaonyonywa. Aghalabu, makabaila ndio watanufaika na sheria zilizopo.
Kwa hakika ipo mifano mingi ya sheria au usimamizi wa sheria unaoshabihiana na msimamo huu wa Marx. Inapotokea ajali ya basi na kusababisha vifo, hautasikia dereva aliyesababisha ajali kusimamishwa kizimbani pamoja na mmiliki, ambaye pengine alichangia ajali kwa kutogharimia utunzwaji wa basi ili kuwepo kwenye hali ya usalama. Siku zote utasikia dereva peke yake akijibu mashtaka.
Lakini ukweli wa hoja za wafuasi wa Marx hazifuti umuhimu wa sheria nyingi nyingine ambazo zinalinda masilahi ya wote – wanyonyaji na wanaonyonywa, wenye mali na wasio na mali, matajiri na maskini, na kadhalika. Ilimradi sheria hizo zifuatwe, jambo ambalo halitokei wakati wote. Sheria inayo pia hulka ya kutupima sote kwenye mizani moja.
Hakuna maana yoyote kuwepo kwa sheria za kulinda usalama wa watumiaji wa vyombo vya usafiri kama sheria hizo hazifuatwi wakati wote, au kama sheria hizo zinaonekana kuwagusa baadhi tu ya watu halafu ziwaache wengine wakikiuka sheria.
Mara kwa mara nashuhudia barabarani mifano mingi ya ukiukwaji wa baadhi ya sheria hizi.
Katika zile operesheni za polisi ambazo hufanyika kwa msimu halafu kusahaulika, mojawapo ya hizo operesheni ambazo msimu wake umekuwa mrefu kuliko kawaida lakini ambayo imezaa matunda ni operesheni dhidi ya mwendo kasi.
Kwa kiasi kikubwa sana madereva wanaotumia barabara za Tanzania wanazisoma alama za barabarani na kufuata maelekezo yake. Lakini bado wapo madereva ambao hawafuati utaratibu huu mpya.
Moja ya matamshi ya msingi kabisa ambayo yamezungumzwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, ni kusema kuwa madereva wote – pamoja na madereva wa magari ya serikali – wanapaswa kuzingatia kipengele cha sheria dhidi ya mwendo kasi.
Lakini inawezekana waziri hajatambua ugumu wa utekelezaji wa msimamo wake huo. Nimekuwa najiuliza sababu ya madereva wa magari yenye namba za usajili zinazoanza na DFP, SU, SM na ST – kutozingatia alama za kupunguza mwendo kwenye maeneo yaliyoainishwa na hivi karibuni nimesikia kutoka kwa ofisa wa Polisi kuwa madereva hao wakisimamishwa hawasimamishi magari.
Ofisa mwingine aliniambia kuwa alipojaribu kumtoza faini dereva wa gari la manispaa aliyezidisha mwendo aliamrishwa na mkuu wake kutomtoza faini na akaamriwa kumuachia huru.
Masuala mawili yanajitokeza hapa: kwanza, bado wapo madereva wanaoamini kuwa gari analoendesha haliguswi na baadhi ya sheria za usalama barabarani. Pili, polisi hawaweki jitihada inayostahili dhidi ya ukiukwaji wa sheria dhidi ya mwendo kasi kwa baadhi ya magari kwa hofu kuwa wanaweza kukosolewa na wakuu kuwa hawakupaswa kufanya hivyo.
Kuna njia mbili tu za kuweza kumaliza tatizo hili. Kwanza, kurekebisha sheria iliyopo kuruhusu madereva wa magari wanaokiuka sheria kuruhusiwa kuendesha kwa mwendo wanaoona unafaa wakati wowote. Kwa sasa hivi ni misafara maalumu tu ya magari (kama ya viongozi wa juu), magari ya polisi, Zimamoto na magari ya wagonjwa ndiyo yanaruhusiwa kufanya hivi.
Pili, kutokana na desturi ambayo ipo sasa hivi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi atoe maelekezo mahususi kwa polisi kutekeleza sheria kikamilifu bila woga ili kuwaondoa hofu kuwa watamsimamisha dereva wa mkubwa ambaye atawafukuzisha kazi.
Si ajabu kuwa haya mapungufu yanayojitokeza kwenye usimamizi wa sheria barabarani yapo pia kwenye maeneo mengine ya shughuli za usafirishaji nchini na ndiyo maana tumekutwa na ajali nyingine.
Ajali ya mv Nyerere inapaswa kuwa somo la mwisho juu ya njia sahihi za kuepuka maafa. Tulipaswa kuhitimu muda mrefu uliopita.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share