Mwangwi wa kilio cha wakulima wa korosho unazidi kusikika pande zote za nchi.

Idadi kubwa ya wanafunzi wamekwama kwenda shuleni. Wale waliofaulu darasa la saba wameshindwa kuripoti shule za sekondari kwa ukosefu wa nguo na vifaa vya masomo.

Hata wale ambao kwa kawaida hawapendi watoto wao waendelee na masomo ya sekondari wamepata kisingizio cha ukosefu wa fedha za korosho. Hali ni mbaya.

Toleo lililopita la gazeti hili tuliandika habari na barua ndefu zilizohusu mtifuano kwenye uhakiki na malipo kwa wakulima wa korosho.

Serikali imeunda timu maalumu za uhakiki. Tayari kuna lawama nyingi kutoka kwa wakulima na wananchi kwa jumla kwamba timu hizo zinajihusisha na vitendo vya rushwa. Wanatajwa watendaji wa serikali, watendaji kadhaa wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wengine wengi waliopewa dhamana ya kuhakikisha vita dhidi ya ‘kangomba’ inafanikiwa.

Hii si habari njema kwa nchi. Ni kumkosesha usingizi Rais John Magufuli ambaye kwa nia njema aliamua kuingilia kati kwa kulitumia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuhakikisha wakulima wanaokolewa dhidi ya dhuluma.

Tunasikitika kuona kuwa wale walioaminiwa hata wakapewa kazi ya kusimamia suala hili ili haki itendeke kwa wakulima, nao wamekuwa sehemu ya kuongeza pilipili kwenye majeraha.

Suala la korosho kwa wananchi wa mikoa inayolima zao hilo si la kuchukuliwa kwa wepesi. Korosho ndiyo roho inayowapa uhai wa kimaendeleo wananchi hao.

Tunatoa mwito kwa wote wanaojihusisha na hujuma hizo kuacha dhambi hiyo. Tunaomba mamlaka za nchi zitumike kuwasaka na kuwashughulikia kisheria wote wanaoshiriki kuwaumiza wakulima.

Tunaishauri serikali itumie matatizo ya ununuzi wa korosho mwaka huu kama rejea ya kuwezesha upatikanaji wa suluhu ya kudumu ya kilio cha wakulima wa zao hili.

Taifa limefanikiwa kupambana na kushinda vita nyingi ngumu. Tunaamini kwa moyo na ari ile ile iliyoleta ushindi kwa vita zilizotangulia, vitatuongoza kupata ushindi kwenye mapambano haya.

Hii si kazi ya serikali pekee, bali ni wajibu wa kila Mtanzania mzalendo anayewatakia heri wakulima wa korosho na maendeleo ya taifa letu kwa jumla.

Viongozi wote watakaobainika kujihusisha kwenye hujuma ya mpango huu wa uhakiki, dola haina budi kuwachukulia hatua stahiki za kisheria. Kwa pamoja tunaamini tutaishinda dhuluma hii.

1346 Total Views 9 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!