Manu Dibango ni gwiji wa kupuliza chombo adhimu katika ulimwengu wa muziki, kilichobatizwa kwa jina la ‘midomo ya bata’ (saxophone) na watu wa ‘mujini’, aliyejizolea sifa kemkem barani Afrika na ulimwenguni kwa ujumla.

Nguli huyo Februari 10, 2014 alitimiza miaka 80 ya kuzalikwa kwake.

Jina lake halisi ni Emmanuel Dibango, ambaye, pamoja na kupuliza saxophone, pia ni mtunzi na mwimbaji mahiri mwenye sauti nzito. 

Ni kiongozi wa Bendi ya Makossa.

Alizaliwa Februari 10, 1934 katika mji wa Douala, Cameroon, Afrika ya Magharibi. Baba yake alikuwa mfanyakazi serikalini na vilevile alikuwa mtayarishaji maarufu wa nguo.

Kipaji cha Emmanuel Dibango kiligundulika baada ya kumuona alivyokuwa akipenda muziki tangu alipokuwa mdogo akiwa nyumbani, na hususani kanisani ambako mama yake alikuwa kiongozi wa kwaya.

Mwaka 1954 akiwa na umri wa miaka 20, alianza rasmi kupiga muziki. Kama kawaida ya wanamuziki walio makini kwa kazi yao, Manu ni miongoni mwao kwani alipiga ‘kitabu’ na kupata elimu yake katika Shule ya Baccalaureate nchini Ufaransa mwaka 1956.

Yaelezwa kwamba kati ya mwaka 1949 na 1954 alichukua masomo ya kupiga piano na kuanzia kupiga muziki wa jazz.

Ni mwanamuziki anayejiwekea kumbukumbu kwa wapenzi wa muziki kwa wimbo wake uliotamba wa Supa Kumba aliouimba akitamba kwa kutumia sauti yake nzito na kuwa na mvuto wa aina yake miaka ya 1970.

Dibango alikuwa mmoja wa waanzilishi wa muziki wa kidunia katika miaka 1970, na alifahamika sana takribani katika nchi  zote  zilizotawaliwa na Wafaransa huko Afrika ya Magharibi.

Aliendelea kuhodhi hadhi ya kimataifa akiwa mwanamuziki wa kutegemewa katika muziki wa Kiafrika miaka ya 1990. Mwaka 1994, Boston Globe ilimpendekeza kuwa mwanamuziki bora kwa kibao chake cha Wakafrika. Alipokea tuzo hizo akiwa na wanamuziki nyota  kutoka Afrika na Ulaya kama King Sunny Ade, Ladysmith Black Mambazo, Peter Gabriel na Sinead O’Connor.

Ingawa Manu Dibango amekuwa akipingwa sana kwa kutumia sauti za kigeni za Waafrika, Wazungu na Wamarekani lakini alikuwa na msimamo madhubuti wa kutetea alama (identity) yake katika muziki.

Muziki katika bendi yake ya Makossa ulipanda chati ambapo ulionekana ni wa kisasa zaidi kwa watu nchini Cameroon mwaka 1973, baada ya kutoa albamu ya muziki wa Soul iitwayo Makossa.

Kama nilivyokujuza awali, Dibango alipokuwa na umri wa miaka 15 akiwa na familia yake, walikwenda nchini Ufaransa na yeye akaingia shule akisomea cheti cha Stashahada. Akiwa huko alisikia muziki wa jazz wa Kimarekani na alitamka furaha yake kumsikia kwa mara ya kwanza redioni mwanamuziki, Louis Armstrong.

Kwenye miaka ya 1940, Manu Dibango ilielekeza nguvu zake katika upigaji wa saxophone, akilibwaga piano, chombo ‘kilichomtoa’ alichokuwa akikitumia awali.

Mwishoni mwa miaka ya 1950, Dibango alihamia  katika jiji la Brussels nchini Ubelgiji. Akiwa Ubelgiji, miaka ya 1960 yalifikiwa makubaliano ya kupatikana kwa Uhuru wa nchi ya Kongo.

Manu Dibango pia alipiga muziki na wanamuziki wakongwe wa muziki katika Afrika waliokuwa wakiishi Ulaya akiwamo Joseph Kabasele ‘Grand Kale’, ambaye alikuwa mwimbaji nyota kutoka nchi ya  Kongo.

Baada ya Kongo kupata Uhuru wake mwaka 1960, Rais wa nchi hiyo Mobutu Sese Seko akaibadilisha jina na kuwa Zaire.

Albamu yake ya Independence Cha-Cha ikaja kuwa moto kwa wapenzi wa muziki Afrika na Ubelgiji hususani mji wa Brussels.

Mwaka 1961 Dibango alipiga na kurekodi nyimbo zaidi ya 100  nchini humo,  akishirikiana na Grand Kale katika bendi ya African Jazz hadi ilipofika mwaka 1963 wakati Dibango alipoamua kurejea kwao Cameroon baada ya kuiacha kwa miaka  12.

Hata hivyo, mwaka 1965 alilazimika kwenda Paris nchini Ufaransa ambako wapenzi wa muziki wake wa Soul katika jiji hilo walimuhitaji. Huko Paris,  akaanza  kupiga muziki wa kimataifa akitumia saxophone yake.

Baada ya kupata mafanikio makubwa, Dibango alitoa albamu nyingi za muziki wa Kiafrika akichanganya na wa ule wa Jazz na Blues.

Mwaka 1979 alijaribu kupiga muziki  wa  reggae na kurekodi na baadhi ya wanamuziki wa kikundi cha The  Wailers cha Jamaica.  The Wailers ilikuwa ikimilikiwa na Robert Nesta Marley (Bob Marley).

Mwaka 1984 Manu Dibango alifanya sherehe kubwa ya kutimiza miaka 30 ya kupiga muziki, iliyowakutanisha wanamzuki wengine kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Mwanamuziki wa Ulaya, Sinead O’Connor, na Peter Gabriel waliungana na wanamuziki nyota kutoka Afrika kama Youssou N’Dour, King Sunny Ade na Ladysmith Black Mambazo kurekodi na Manu Dibango katika albamu yake ya mwaka 1994 iliyojulikana kama  Wakafrika.

Nyimbo  nyingine zilizompa umaarufu zilikuwa Supa Kumba aliyoitoa mwaka 1974 na Africadelic ya 1975, Gone Clear, Island ya mwaka 1979, Ambassador ya 1981, Waka Juju na Sonodisc ya 1982.

 

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa: 0713 331200, 0767 331200 na 0784 331200.

By Jamhuri