Maoni ya wananchi kuhusu Katiba yaheshimiwe

Kesho Jumatano, Oktoba 8 mwaka huu, Rais Jakaya Mrisho Kikwete, wa Tanzania, na Rais Dk. Ali Mohamed Shein wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wanatazamiwa kukabidhiwa rasmi Katiba iliyopendekezwa kutoka Bunge Maalum la Katiba, mjini Dodoma.

Ni dhahiri Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, atawakabidhi marais hao Katiba hiyo kudhihirisha wajumbe wake wamekamilisha kazi waliyopewa na Serikali, ya kuandika mapendekezo ya Katiba mpya iliyo bora na makini kwa wananchi.

Ni kweli, kazi hiyo imekamilika Alhamisi ya wiki iliyopita, baada ya wajumbe hao kupita katika misukosuko, vikwazo, vijembe hata vitisho kwa baadhi ya wajumbe — achilia mbali wajumbe wengine waliosusia Bunge hilo baada ya kuona ndani si shwari.

Hapo mgawano wa kwanza ulitokea, wa upande mmoja kudai mijadala yote ihusishwe na Rasimu ya Katiba, iliyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.  Upande wa pili ulieleza ipo haja pia kujadili mambo mapya ambayo hayamo kwenye rasimu iliyotolewana Tume.

Migongano hiyo ya mawazo na misimamo ya wajumbe ilisababisha Bunge hilo kupata mtikisiko na kuyumba. Kuyumba kwa Bunge hilo hakukufanya wajumbe walio wengi kuzira majadiliano na kutoa mapendekezo ya Katiba hii. Sawa; mapendekezo yamepatikana na yamo katika maandalizi ya kukabidhiwa Rais Kikwete na Rais Shein hapo kesho. Wakati hayo maandalizi yanafanyika, tayari lele zimeanza mitaani, tunacho subiri ni ngoma tu kupigwa wananchi wacheze.

Hii si hali nzuri. Ni dalili ya kuleta mfarakano miongoni mwa wananchi. Ikumbukwe wajumbe wachache walizira mijadala na kutoka bungeni.  Wajumbe haoni UKAWA.  Hisia za maneno ya wananchi mitaani ni malumbano kati ya CCM na UKAWA.

CCM (Chama Cha Mapinduzi) na UKAWA – vyama vya siasa vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi, kila kimoja kinadai kinatetea na kuwasilisha maoni ya wanachama wao na wananchi kwa ujumla.  Pana ukweli hapo?

Watanzania ama tumepuuzia au tumekuwa katika vipimo kuona kati yao nani mkweli na muwakilishi wa umma.  Vyovyote iwavyo hatua tuliyofikia ya kuanza kusikia lele tunasubiri ngoma kulia, tuanze kucheza, si hatua nzuri.

Nashauri tufike mahali, Serikali ikubali kusikia sauti za wachache na kuzifanyia vitendo sahihi, siyo kusikiliza tu na kuacha kutenda vitendo.  Sipendi kurudia kuandika kauli zinazotofautiana kati ya Rais Kikwete na Waziri Mkuu Pinda kwa wananchi katika kupatikana Katiba mpya.

Sipendi kuandika kauli za viongozi wa dini — mashekhe na maaskofu — dhidi ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba na Serikali.  Kauli zote zina ukakasi vinywani, na zina nyange masikioni mwa wananchi.  Yaarabi tunusuru.

Wanasheria, wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba na wanasiasa ingawa mmemaliza kazi, mtambue mmekaanga mbuyu wananchi watafune.  Mbuyu hizi kwa meno na mazingira waliyonayo hawawezi. Nachelea wananchi kuburuzwa. Mchakato huu  mpya kwetu. Wananchi wapewe wasaa wa kuchambua na kuandika kile wanachotaka.  Si vyema kuona tena wanasiasa na viongozi wa Serikali kutulazimisha kwa kuweka muda mfupi maalum eti Katiba ipatikane kabla ya uchaguzi ujao na rais ajaye.

Indhari kwa Serikali kwamba iamini na kukubali kuwa wananchi wengi hawajapendezwa na mchakato ulivyoendeshwa.  Shida siyo Serikali tatu, mbili au moja, la hasha. Kiini ni maslahi na uadilifu wa viongozi na haki za wananchi. Narudia, kama Serikali inathamini wananchi wake, sioni sababu ya kuwaruhusu baadhi ya wanasiasa kuendelea kuweka mbinu zao za ushindi kwa wananchi. Nawaomba wasubiri wakati wao wa kugombea madaraka. Wanasiasa mna matatizo gani?

Serikali isikubali kuyumbishwa na baadhi ya wanasiasa. Naomba ifahamike siyo vyama vya siasa vya upinzani tu, hapana; hata ndani ya chama kinachotawala, wapo wanaojifanya wanaipenda sana CCM.  Si kweli.  Mbinu na hila zikifahamika za hao “wajanja” Serikali huenda ikawa mashakani na wananchi wakawa taabuni.  Tujifunze kutoka kwa majirani.  Isitoshe sisi Tanzania tuna mfano mzuri kule Zanzibar yaliyotokea 1963 na 1964.

Namalizia kwa kusema kupatikana kwa Katiba iliyopendekezwa ni jambo moja na kuruhusu bila shaka wala vishawishi kupiga kura ya maoni kwa wananchi ni jambo jingine.  Naomba uwazi, ukweli na uadilifu utumike.