*Imejengwa na kuziba barabara ya mtaa

*Mmiliki, wanafunzi waishi eneo moja

 

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

 

Shule ya St. Florence Academy iliyopo Mikocheni, Dar es Salaam, ambayo mwalimu wake anatuhumiwa kuwadhalilisha kingono wanafunzi wa kike wanne, inadaiwa imejengwa kwenye barabara na hivyo kufunga mtaa.

Mwalimu huyo ambaye vyombo vya dola vinamsaka, anadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti; na sasa baadhi ya wazazi wameanza kuwahamisha watoto wao.

Wakati hayo yakiendelea, imefahamika kuwa, licha ya shule hiyo kujengwa mahali pasipostahili, mmiliki wa shule na familia yake wanaishi pamoja na wanafunzi ndani ya eneo la shule hiyo.

Mmiliki alipewa vibali vya kuanzisha shule hiyo kutoka kwa iliyokuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, huku eneo hilo likitajwa kukosa sifa za kujengwa shule.

 

Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni inazo taarifa za kufungwa kwa mtaa huo ili kupisha ujenzi wa shule hiyo, lakini majirani wanaolalamikia kitendo hicho wamesema hakuna hatua zozote zilizokwishachukuliwa.

Ramani ya eneo la shule ya St. Florence Academy inaonyesha kuwa mahali yalipojengwa baadhi ya madarasa na ofisi ni barabara ya mtaa.

Eneo la nyuma nalo lidaiwa kumegwa bila vibali, na sasa kumejengwa vyumba vya madarasa na mabweni.

Kwa mujibu wa ramani, eneo ambalo shule imejengwa, lina ukubwa wa mita 30 kwa 30; kinyume na mwongozo wa Waraka wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa mwaka 2011 ambao unataka shule iliyo mjini ipewe usajili endapo itakuwa na eneo lenye ukubwa wa hekta 1.5.

“Shule ina wanafunzi wengi, zaidi ya 500. Barabara ni moja, magari yanayopeleka na kutoa wanafunzi hapa ni mengi. Kama itatokea suala la moto watakufa wanafunzi na watu wengine wengi. Kuna kelele nyingi hapa, uharibifu wa mazingira kwa majirani ni mkubwa. Kuna mapipa ya taka yananuka, kuna moshi unaotoka shuleni unaudhi majirani.

“Suala hili tumelipeleka Manispaa lakini hakuna suluhisho. Sheria zimevunjwa, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa,” wamelalamika majirani kwenye barua yao kwenda Manispaa ya Kinondoni.

Mei 11, 1999 iliyokuwa Tume ya Jiji la Dar es Salaam, katika barua yake ilitamka wazi kuwa mahali kulikojengwa shule hiyo ni makazi ya watu.

Uongozi wa shule hiyo, kwa nyakati tofauti uliomba na kufanikiwa kupewa kibali cha kuendeleza eneo la nyuma ya shule kwa ajili ya kupanda miti na kujenga uwanja wa michezo.

Uamuzi wa uongozi wa shule ulilenga kupunguza hewa chafu inayotoka kwenye mabwawa ya maji machafu, na hivyo kuwa na athari kwa afya za wanafunzi na watu wanaoishi eneo hilo.

Hata hivyo, imebainika kuwa eneo hilo limeangukia mikononi mwa mmiliki wa shule hiyo kwa kuongeza wigo wa shule.

Julai 22, 2009 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ilimwandikia barua mmiliki wa St. Florence Academy iliyosema: “Eneo unaloomba ni eneo lililoachwa wazi kwa ajili ya kuzuia hewa chafu kutoka kwenye mabwawa ya majitaka yaliyopo eneo hilo…Kuna mtindo wa baadhi ya wana mazingira wasio waaminifu ambao mara wapewapo idhini ya kuotesha miti katika eneo fulani wanatumia eneo hili kwa matumizi mengine kinyume cha taratibu. Kwa barua hii unapewa idhini ya kuotesha miti na kuitunza ili eneo hili lipendeze na liwe endelevu na si vinginevyo.” Barua hiyo ilisainiwa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo aliyetambulika kwa jina la Mkomba.

Hata hivyo, Wizara ya Elimu, katika namna inayozua maswali, ilitoa kibali cha ujenzi wa shule licha ya kutambua kuwa mahali inakojengwa ni katikati ya barabara ya mtaa.

Waraka wa Elimu Na. 10 wa mwaka 2011 ambao unakazia Mwongozo wa Usajili wa Shule uliotolewa mwaka 1982; pamoja na mambo mengine unaagiza kuwa: “Mashirika, taasisi mbalimbali na watu binafsi wenye uwezo wa kuanzisha shule zisizo za serikali hapa nchini, wanashauriwa kuzingatia masharti yaliyoainishwa katika sheria na miongozo mbalimbali inayotolewa na Wizara.

Mwenye nia na uwezo wa kuanzisha Shule/Chuo cha ualimu ni lazima atomize masharti yafuatayo:-

  • Awe na eneo lisilopungua hekta 3 kwa maeneo ya vijijini na 1.5 kwa eneo la mjini lililotolewa kwa madhumuni ya Elimu na Mamlaka husika (Wizara ya Ardhi na Serikali za vijiji).
  • Aombe kibali cha kujenga majengo ya shule/chuo kwa kufuata ramani zilizopendekezwa na Wizara ama zitakazokubaliwa na Wizara na ambazo

zimepitishwa na mamlaka za Halmashauri husika (Mhandisi wa Wilaya na Mipango Miji wa Wilaya).”

Mkurugenzi wa Shule hiyo, Flora Assey amekielezea kitendo cha shule kujengwa katikati ya barabara ya mtaa kuwa ni cha kawaida kwani hata katikati ya jiji kuna shule nyingi zimejengwa kwa namna hiyo.

“Hakuna njia kule, kuna mabwawa na matuta yameinuliwa juu, pia kuna uzio kwa hiyo njia wanayosema nimeiziba kwa kujenga shule, haipitiki,” anasema Assey.

Aliyekuwa Msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, aliyefahamika kwa jina la Bunyazu, aliwahi kusema suala hilo litashughulikiwa mara baada kupata taarifa za kutosha.

1517 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!