*Yumo aliyeghushi umri, atang’atuka mwaka 2017

*Mwingine ahitimu chuo kikuu na kupewa ujaji

Miezi kadhaa baada ya JAMHURI kuchapisha taarifa ya utetezi wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kuhusu uteuzi wa majaji wasio na sifa, mbunge huyo ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Upinzani na Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Katiba na Sheria, wiki iliyopita alijitokeza tena na kutishia kumshitaki Rais Jakaya Kikwete.

Ifuatayo ni taarifa yake – neno hadi neno – kama alivyoitoa kwa waandishi wa habari mjini Dodoma. Ndugu waandishi wa habari, nimewaita hapa kuwaambia jambo ambalo lilishatokea hapa bungeni katika kikao kilichopita, likapigiwa sana kelele, likaundiwa Kamati ya kulichunguza, Kamati ikalichunguza, tunaambiwa imemaliza uchunguzi.

 

Lakini kwa taarifa tulizozipata, tumeambiwa kwamba Spika (Anne Makinda) amekataa na hataki kuelezea matokeo ya uchunguzi wa Kamati. Hili ni suala ambalo nililizungumza bungeni wakati natoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Katiba na Sheria, kuhusiana na uteuzi wa majaji wa Mahakama zetu hapa nchini.

 

Mtakumbuka kwamba katika hotuba yangu ya Julai 13 (mwaka huu), nilitoa kauli kwamba uteuzi wa majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani Tanzania umegubikwa na kinachoelekea kuwa ukiukaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano  kwa sababu baadhi ya majaji ambao wameteuliwa na Rais Kikwete tangu ameingia madarakani (mwaka 2005) hawana sifa, uwezo na wala hawakufaa kuteuliwa kushika madaraka ya Jaji Mkuu, au Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania.

 

Hiyo ndiyo kauli niliyoitoa bungeni Julai na ndiyo kauli iliyopelekea (iliyosababisha) mimi kushitakiwa kwenye Kamati ya Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi.

 

Baadaye kabla kikao hicho cha Bunge hakijaisha, niliitwa kwenye Kamati hiyo kujieleza. Nilijieleza kwa kirefu sana na nilitoa ushahidi wa nyaraka nyingi zikiwemo kutoka Ofisi ya Rais-Ikulu, nyaraka kutoka mahakamani zinazoonesha kwamba hata ndani ya Serikali kwenyewe, wanafahamu kwamba kumekuwa na ukiukaji wa Katiba katika uteuzi wa majaji.

 

Niseme tu taarifa ya uchunguzi iliyoandaliwa na kikosi kazi cha Ofisi ya Rais, Machi 2008. Hiki kikosi kazi kiliundwa baada ya kikao kilichomshirikisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, wakati huo, na Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo, Desemba 2007.

 

Waliunda kikosi kazi kuchunguza suala la uteuzi wa majaji na ripoti yao ya Machi 2008 inasema majaji wengi, na iliwataja kwa majina baadhi yao, kwamba majaji wengi wanafanya kazi ya ujaji kinyume cha Katiba na ikaongeza kwamba majaji hao kazi ambazo wamezifanya na wanazoendelea kuzifanya ni sawa na zingefanywa na mtu mwingine yeyote asiyekuwa na mamlaka ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

 

Sasa hiyo ni mwaka 2008. Ushahidi huo wa hiyo ripoti ambayo nimeizungumzia niliikabidhi kwa Kamati ya Brigedia Jenerali Ngwilizi na baadaye kama mnavyofahamu, waraka niliouandika kwa ajili ya kamati, vilivile ulichapishwa katika magazeti, nafikiri katika Gazeti la JAHMURI liliichapisha na vilevile ilichapishwa katika magazeti mengine. Baadaye nilizungumzia masuala haya na ushahidi huu katika mkutano wa nusu mwaka wa Chama cha Mawakili wa Tanzania Bara.

 

Sasa, baada ya taarifa zote hizi kutoka, Serikali haijawahi kukanusha rasmi kwamba majaji niliowatuhumu kwenye Kamati ya Brigedia Jenerali Ngwilizi na waliozungumzwa kwenye ripoti ya kikosi kazi cha Ikulu, wako mahakamani kihalali kwa mujibu wa Katiba. Serikali haijawahi kutangaza rasmi kwamba kauli niliyoitoa bungeni na baadaye nikaitolea ushahidi si ya kweli.

 

Sasa mnafahamu kilichotokea baada ya magazeti kuchapisha hizi taarifa, ilikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati, Brigedia Jenerali Ngwilizi kutoa makatazo kwa vyombo vya habari kuzungumzia hili suala la uteuzi wa majaji kwa hoja kwamba linazungumzwa na Kamati yake.

 

Hiyo taarifa ya Brigedia Jenerali Ngwilizi ilikuwa ni ya upotoshaji mkubwa kwa sababu kamati hiyo haina mamlaka kwa mujibu wa mamlaka yake kwenye kanuni, haina mamlaka ya kuchunguza masuala ya uteuzi wa majaji. Haikuundwa kuchunguza majaji, iliundwa kuchunguza kauli niliyoitoa bungeni kama ni ya kweli au si ya kweli. Kwa hiyo, hawakupaswa kukataza vyombo vya habari kuzungumzia uteuzi wa majaji kwa sababu hawakuwa wanachunguza ukweli wa uteuzi huo, walikuwa wananichunguza mie.

 

Sasa, kukataza vyombo vya habari kuandika hizi habari ilikuwa ni njama tu ya kuhakikisha kwamba uchafu ambao ulikuwa umefichwa kwa miaka mingi hautoki hadharani kwa kupitia vyombo vya habari.

 

Sasa leo nataka nisema na naomba vyombo vya habari vichapishe haya nitakayoyasema. Kwamba suala la ukiukaji wa Katiba kuhusiana na uteuzi wa majaji ni suala kubwa sana na haliwezi kuzimwa kwa mbinu kama hizo wanazotumia za kukataza vyombo vya habari kuandika hii habari, au kwa Spika kuzuia kutoa bungeni taarifa ya Kamati iliyochunguza kauli yangu. Hizo mbinu haziwezi zikazima mjadala huu kwa sababu tunazungumzia mhimili wa dola unaohusu utoaji wa haki kwa Watanzania.

 

Kama majaji wetu hawana uwezo, hawana sifa, hawana maadili ya kutoa haki, hili siyo suala la kuzimwa na Spika wala siyo suala la kukataza vyombo vya habari kuliandika kwa sababu linahusu uhai wa nchi yetu. Linahusu uhai wa mfumo mzima wa utoaji haki.

 

Kama majaji hawajui sheria, kama ilivyo kwa Jaji (jina tunalihifadhi), hana hata shahada ya sheria, ndiyo mwanafunzi sasa hivi na ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa, mahakama ya juu kabisa ya nchi hii, kama hana hata shahada ya sheria, anakaaje mahakamani?  Anatoaje haki kwa mujibu wa sheria ambayo hajaisomea?

 

Kama majaji wamekamatwa wakitoa rushwa wakiwa mawakili, majaji wawili tumeoneshwa tuna ushahidi kwamba wakiwa mawakili, walikamatwa wanahonga mahakimu, wakaamriwa wapelekwe kwenye vyombo vya nidhamu husika, kabla hawajapelekwa kwenye vyombo vya kinidhamu kushughulikiwa wakateuliwa kuwa majaji.

 

Majaji wa aina hiyo watamtendea nani haki? Nani atakayekuwa na amani kama kesi yake iko mbele ya majaji wa aina hiyo? Majaji ambao hawajui hata kuandika sentensi moja iliyonyooka ya Kiingereza, na sheria zetu zinasema jaji lazima aandike mwenendo wa kesi Kiingereza na atoe hukumu Kiingereza. Sheria zimeandikwa Kiingereza. Kama jaji hafahamu Kiingereza, hajui, hawezi kuielewa hiyo sheria, hawezi kuandika hukumu, nani atakuwa na amani kesi yake ikiwa mbele ya jaji wa aina hiyo?

 

Mfumo wetu wa utoaji haki uko salama kiasi gani na majaji wa aina hii? Kama majaji ambao Katiba inasema wastaafu, wamefika muda wa kustaafu na wakastaafu, halafu baada ya kustaafu wakapewa mikataba. Katiba yetu inasema jaji hawezi akafanya kazi kama hajala kiapo cha ujaji.

 

Unapostaafu, ukalipwa mafao ya ustaafu, kiapo chako kinaisha, ukipewa mkataba unatakiwa ule kiapo upya, na wote ambao tumewataja hakuna hata mmoja aliyekula kiapo upya, akiwemo Jaji Kiongozi (jina tunalihifadhi) ameongezewa mkataba, hii ni mara ya tatu, kinyume kabisa cha Katiba.

 

Na huo uvunjaji wa Katiba; kuwapa majaji mikataba umeandikwa na hicho kikosi kazi cha Ikulu, imeandikiwa waraka na aliyekuwa Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani, imeandikiwa waraka na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Benerd Luaga, tangu mwaka 2005.

 

Majaji hao wanalalamika kwamba Katiba inavunjwa, hakuna jaji wa mkataba katika nchi hii. Lakini wanapewa mikataba kinyume cha sheria. Majaji wa aina hii inapokwenda kesi ya Serikali – wafanyakazi wamegoma, mnaona ajabu Serikali inashinda kila kesi.

 

Majaji wa aina hii ikienda kesi Serikali imeua kama ilivyomuua Mwangosi (Mwanadishi wa habari, Daudi Mwangosi) na watu wengine wengi tu, mtaona ajabu Serikali ikishinda kwa majaji wa aina hii?

 

Ikienda kesi inayohusu utendaji wa Rais, au watu wake, utaona ajabu Serikali ikipeta kwa majaji ambao wamepewa kazi kinyume cha Katiba na wanajua wamepewa kinyume cha Katiba kabisa?

 

Kwa hiyo hili suala ni kubwa sana, haliwezi likazimwa kwa vyombo vya habari kukatazwa kulizungumza, na nilikuwa nasema kwa sababu hiyo, nataka nichukue fursa hii, kutoa, kuzungumza mambo matatu.

 

Jambo la kwanza, Spika wa Bunge atoe hadharani, atoe bungeni matokeo au taarifa ya Kamati ya Brigedia Jenerali Ngwilizi ili Bunge lililoambiwa kwamba majaji walioteuliwa wameteuliwa kinyume cha Katiba, na baadaye Serikali kupitia Waziri Katiba na Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakasema huo ni uongo, Bunge lifahamu ukweli ni upi.

 

Na Bunge likifahamu ukweli ni upi, Watanzania walionisikia nikisema majaji wao hawafai na Watanzania waliomsikia Waziri Chikawe (Mathias) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Werema (Frederick) wakisema huo ni uongo, Watanzania nao wafahamu ukweli ni upi. Hiyo taarifa ya Kamati ya Brigedia Jenerali Ngwilizi itolewe bungeni ukweli ujulikane.

 

Pili, kwa vile ushahidi ulishatoka hadharani, umechapishwa magazetini, kwamba kuna majaji hawana hata shahada ya sheria, Jaji Mbarouk Salim Mbarouk wa Mahakama ya Rufani ndiyo anasoma shahada ya kwanza ya sheria sasa hivi. Wakati Katiba inasema awe amesoma shahada ya sheria na amefanya kazi kwa miaka isiyopungua 15, yeye ni mwanafunzi sasa hivi.

 

Au hao wengine ambao wamefanya kazi, wengine miaka mitatu, kama Jaji (jina tunalihifadhi) amemaliza Chuo Kikuu Huria, hajakaa miaka mitatu, ni jaji, hawezi kuandika hata sentensi moja ya Kiingereza.

 

Majaji hawa na hao wengine ambao tumesema hawakupitia kwenye Tume ya Utumishi wa Mahakama. Majaji hao tunataka waondolewe kazi mara moja, na anayeweza kuwaondoa kazi ni mamlaka yao ya uteuzi, yaani Mheshimiwa Rais.

 

Naomba nifafanue hapo; utaratibu wa kikatiba wa kuwaondoa majaji madarakani, unasema kwamba kama jaji ametuhumiwa kwa makosa ya kimaadili anatakiwa aundiwe tume yenye majaji watakotoka kwenye Jumuiya ya Madola, na wengine ili wachunguze hizo tuhuma, akipatikana na hatia anaondolewa madarakani. Huo ndiyo utaratibu wa kikatiba.

 

Ninachotaka kufafanua hapa ni kwamba hao majaji ninaowasema na ambao tumewatolea ushahidi, hawa hawahusiki na utaratibu huu. Utaratibu huu unazungumzia majaji ambao wameteuliwa sawasawa; majaji ambao uteuzi wao umetokana na Tume ya Utumishi wa Mahakama. Majaji ambao wameapishwa, majaji ambao hawana tuhuma za uhalifu, tuhuma za ukosefu wa maadili, majaji ambao wana sifa za kitaaluma za miaka 10 ya mahakama za rufani.

 

Hao ambao Katiba inasema waundiwe tume ni majaji ambao wameteuliwa sawasawa, siyo majaji ambao wameteuliwa kinyume cha Katiba. Hao ambao wameteuliwa kinyume cha Katiba hawawezi wakalindwa na Katiba namna hiyo.

 

Ndiyo maana tunasema Rais afute uteuzi wao na aufute haraka iwezekanavyo kama ilivyoelekeza kamati yake mwaka 2008; ilisema Rais ashauriwe afute uteuzi wa majaji hao haraka iwezekanavyo. Hii ilikuwa Machi 2008, mpaka leo miaka minne hawajafanya hivyo.

 

Sasa Rais, haya yalizungumzwa wakayaficha, leo tunayazungumza hadharani, Rais afute uteuzi wao haraka iwezekanavyo. Kama Rais hatafuta uteuzi wa hao majaji, ambao ofisi yake yenyewe inasema wanafanya kazi kinyume cha Katiba, basi sisi kama Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, hatutakuwa na namna nyingine, tutaanzisha mchakato wa kumshitaki Rais bungeni.

 

Katiba yetu na kanuni za Bunge zinasema huwezi kujadili utendaji wa Rais isipokuwa kwa kuleta hoja maalumu bungeni. Tunaenda kuandaa hiyo hoja maalumu, tunaileta kwenye Bunge lijalo, tutatafuta sahihi. Kanuni zinasema na Katiba inasema, ili hoja hiyo ijadiliwe, inatakiwa isainiwe na si chini ya asilimia 20 ya wabunge.

 

Kwa hiyo tunahitaji sahihi za wabunge 72 au 73 and above (na kuendelea), ili kuingiza hoja ya kumjadili Rais na uteuzi wa majaji huu kama hatachukua hatua za kuwafuta hawa ambao amewateua kinyume cha Katiba aliyoapa kuitetea na kuilinda.

 

Kwa hiyo, hili jambo ndugu zangu si dogo, hili jambo haliishi, hili jambo halitafunikwa tena, namna pekee ya kulitatua ni kwa Rais kutimiza wajibu wake kikatiba. Kuondoa wale ambao wamewekwa kinyume cha Katiba na wanasimamia mfumo wetu wa utoaji haki.

La mwisho ndugu zangu, kuna ambayo yamejitokeza baada ya mimi kuwa nimezungumza na Kamati ya Brigedia Jenerali Ngwilizi, kuna ambayo yamejitokeza baada ya mimi kuandika waraka ambao umekuja kuchapishwa baadaye na magazeti.

 

Tuna taarifa, tuna taarifa kwamba kuna jaji, hatutamtaja sasa hivi, kuna jaji ameghushi nyaraka za umri wake. Katiba yetu inasema jaji wa Mahakama Kuu atafanya kazi hadi atakapofikisha umri wa miaka 60. Jaji wa Mahakama ya Rufani na Jaji Mkuu, watafanya kazi ya ujaji wa Mahakama ya Rufani hadi watakapotimiza umri wa miaka 65.

 

Sasa taarifa tulizonazo, na hatuna sababu ya kushuku ukweli wake, zinasema kwamba kuna Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, aliyezaliwa tarehe 4 Septemba 1949, alitakiwa kwa mujibu wa Katiba, astaafu kazi rasmi tarehe 3 Septemba, 2014.

 

Sasa taarifa tulizo nazo zinasema kwamba kuna watu wamechukua faili lake la Chuo Kikuu na wamechukua mafaili ya aliosoma nao Chuo Kikuu – Kitivo cha Sheria, darasa la mwaka 1974 na mafaili yote yale yamenyofolewa taarifa zote zinazohusu hizo taarifa za walizaliwa lini na mahali walikopita.

 

Halafu wameenda wakapata hati inayoonesha kwamba jaji huyu badala ya kuzaliwa tarehe 4 Septemba, 1949, amezaliwa mwaka 1952, tarehe hiyo hiyo ili kumwezesha kuendelea kukaa Mahakama ya Rufani hadi mwaka 2017.

 

Nimesema hatutamtaja sasa hivi, lakini taarifa tulizonazo hatuna sababu ya kuzitia shaka kwa sababu ni taarifa za ndani kabisa. Sasa nachotaka kusema ni kwamba kama jaji huyo na mamlaka yake ya uteuzi inanisikiliza, kama wananisikiliza, wahakikishe hizo nyaraka za darasa la Kitivo cha Sheria la mwaka 1974, lina majaji kadhaa wa Mahakama ya Rufani sasa hivi, lina maprofesa kadhaa wa sheria sasa hivi, hizo nyaraka zirudishwe Chuo Kikuu sasa hivi na huyo anayejifanya amezaliwa mwaka 1952, hicho alichokiandaa cha kughushi wakiondoe. Vinginevyo tutamtaja hadharani, na tukimtaja hadharani hapatakalika nchi hii.

 

Hizo  nyaraka walizozitoa Chuo Kikuu za darasa la mwaka 1974 la Kitivo cha Sheria, ambapo wamo majaji kadhaa wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania kwa sasa, zirudishwe na hiyo forgery (ughushi) iondolewe. Huyu anayetakiwa kustaafu 2014 astaafu 2014, vinginevyo tutamtaja jina hadharani na hapatakalika.

 

Hatuwezi, nasema hatuwezi tukawa na mahakama chafu kwa sababu mahakama ikiwa chafu hakuna mtu atakayepata haki nchi hii. Mahakama ikiwa chafu, wananchi wakakosa imani na mfumo wa utendaji haki, mfumo wa utoaji haki, Serikali itakuwa inafungulia milango ya fujo na maafa kwa taifa.

 

Kwa hiyo, Rais tafadhali, kama anasikia asikie, hawa majaji mavihiyo hawa na majaji wasiokuwa na sifa hawa awaondoe madarakani, huyu aliyeghushi umri ili aendelee kuwepo hadi 2017 bahati mbaya tumeshapata hizo taarifa, waweke hayo mabo sawasawa kwa mujibu wa Katiba.

 

Ya kwangu ndugu zangu yalikuwa ni hayo, nawashukuruni sana.

 

1298 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!