Baada ya kustaafu utumishi wa umma, Mpita
Njia au maarufu kama MN, amekuwa na fursa
nzuri ya kutembea huku na kule kujionea fahari
ya nchi.
Anajua wapo wanaoweza kumuuliza wapi
anakotoa fedha za kumwezesha kufanya utalii
wa ndani ilhali ka-pensheni kenyewe
hakaeleweki-eleweki. Ndiyo, pensheni ni
ndogo, lakini anasema maisha ni kujiandaa.
Wiki iliyopita MN alikuwa Dodoma – Makao
Makuu ya nchi! Miongoni mwa vijembe
vinavyotawala Dodoma sasa ni kwa wageni wa
aina yake wanapofika jijini humo kuitwa
‘karibuni wa mikoani’. Yaani Dodoma sasa wao
ndio wa mjini! Wale wanaotoka Dar es Salaam
ni wa mikoani.
Mpita Njia amefaidi mengi, lakini
anayokumbuka ni haya yafuatayo: Mosi, licha
ya kusafiri kwa gari lenye kiyoyozi cha nguvu,
aliposhuka tu katika stendi ya mabasi Dodoma
akapokewa na wingu la vumbi. Akajiuliza, mkuu
wa mkoa alikuwa na haraka ya nini kuwapeleka

wasafiri kwenye jangwa la namna ile? Akawaza
na kuwazua, akaona hilo pengine si tatizo lake.
Akajiuliza, yale maelfu yanayokusanywa hapo
stendi hayawezi kumegwa kiasi ili kuwe na
boza la kunyeshea maji ili kukata makali ya
vumbi? Jibu aliloondoka nalo MN ni kuwa
Watanzania mahali penye haki zao wao bado
huona ni hisani. Hakuna anayediriki kulalamika.
Pili, kabla MN hajafika Dodoma, lakini pia
wakati anarejea Dar es Salaam, alishuhudia
makumi ya vijana wenye baiskeli na pikipiki
ndani ya eneo la Ranchi ya Kongwa wakinunua
mafuta ya wizi kutoka kwenye malori. Wote
wana madumu makubwa na kila gari linapopita
huashiria kutaka kununua au kuuza mafuta ya
wizi. Eneo hili ni la Wilaya ya Kongwa
anakotoka mkubwa fulani wa mhimili fulani wa
dola. MN akajiuliza, wizi huu ambao kimsingi ni
uhujumu uchumi kweli amekosekana wa
kuukemea?
Tatu, Mpita Njia akiwa ndani ya basi, akakutana
na ukaidi wa agizo la bosi wa Mambo ya Ndani
ya Nchi la kutaka trafiki waulize kadi na mambo
mengine ndani ya mabasi. Wengi bado wakawa
wanakwenda ‘chemba’ kukutana na
makondakta wa mabasi. MN anadhani wenye
akili hawapaswi kuambiwa huko ‘chemba’
kinafanyika nini.
Nne, Mpita Njia akiwa Dodoma aliona kuna
jambo linapaswa kutafakariwa upya na serikali.

Nalo si jingine, bali ni la kuamuru watu walale
kuanzia saa 5 usiku. Watu wakiwa bado
wanahitaji kuburudika, wanaambiwa waondoke!
Hilo Mpita Njia akaona linapunguza kasi ya
utalii, na pengine hata mapato ambayo
inasemekana Dodoma imeongoza, yangeweza
kuongezeka maradufu kama sheria hizi
‘kandamizi’ za kulazimishana kulala saa 5
zingeondolewa.
Mwisho, Mpita Njia akaona awambie wale
wapenzi wa Jacana – pale kwenye kona
alipoandaliwa ‘mnyama mkubwa’- wenye lugha
yao wanasema “Is no more”. Pamebaki
magofu. Halmashauri ya Jiji la Dodoma
imekwisha kufanya yake! Kilio kwa wapenzi wa
huyo mnyama kinasikika kila kona Dodoma.
Kwa kukosa mapumziko Jacana, MN akaona
hana sababu ya kuendelea kuwapo jijini humo.
Akajiondokea zake.

Tamati…

1438 Total Views 6 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!