Matatizo ya sekta ya vitabu Tanzania

Kama tujuavyo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeanza kutekeleza mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), huku Taifa likiwa na matatizo makubwa ya kuwapo kwa vitabu vibovu shuleni. Ni matatizo yaliyotokana na sera mbovu ya vitabu Tanzania.

Katika mazingira hayo, Tanzania isitarajie kuvuna matunda ya kuonea fahari katika mpango wake huo. Itarajie matunda yatakayofanya tuyaonee aibu.  Ufike wakati tuone kwamba mataifa makubwa yameendelea kwa sababu yanashughulikia kwa umakini mkubwa sekta ya vitabu, hususan vya shule.

 

Bila kupoteza wakati ni vyema nikayataja matatizo yaliyoikumba sekta ya vitabu Tanzania. Tatizo la kwanza ambalo ndilo kubwa zaidi ni Tanzania kuwa na wizara inayoongozwa na watu walioshindwa kusimamia sekta ya vitabu. Watu hawa hawajali kama shule zetu zina vitabu vizuri au vibovu.

 

Kwa mfano, ingawa walimu wamelalamika kwa muda mrefu kwamba vitabu wanavyotumia kufundishia ni vibovu, zilipopatikana Sh. bilioni 36 za rada, wizara haikutafuta maoni ya walimu vitabu vipi vichapishwe upya baada ya kufanyiwa marekebisho.

 

Kwa hivyo, wachapishaji wa vitabu wamelipwa mamilioni ya shilingi kwa kusambaza vitabu vibovu nchini kote. Haya ni matumizi mabaya ya fedha ambayo usingetarajia kuyaona katika nchi maskini kama Tanzania.

 

Tatizo la pili la sekta ya vitabu Tanzania ni ukweli kwamba Wizara ya Elimu haitaki kutumia wastaafu waliobobea katika masuala ya vitabu, mwandishi wa makala haya akiwa mmoja wao. Si kama nilikuwa Mtanzania wa kwanza kupelekwa nchi za nje kuchukua mafunzo ya uandishi, uchapishaji na usambazaji vitabu vya shule, bali pia nilikuwa ofisa wa kwanza wa vitabu mzalendo wizarani.

 

Ukweli ni kwamba walioko wizarani wanakwepa kuwashirikisha wataalamu waliobobea masuala ya vitabu kwa sababu wanajua kwamba hawatakubali kushiriki shauri la kupitisha vitabu kwa rushwa.

 

Izingatiwe kuwa kitabu bora kina sifa zake zisizopungua 15. Lakini Wizara ya Elimu inaona kwamba kitabu bora kina sifa moja tu — kiwe na picha za rangi! Hii ni kwa sababu walioko wizarani hawana ujuzi wowote juu ya sifa za kitabu bora. Pia hawajui kuwa picha za rangi hupandisha bei ya kitabu.

 

Tuliosoma wakati wa Mwingereza tulitumia vitabu vingi vilivyokosa picha za rangi, lakini vyenye maelezo sahihi. Leo wanatumia vitabu vyenye picha za rangi, lakini vyenye maelezo potofu. Kwa hivyo, sisi tuliosoma enzi za mkoloni bado tuna elimu bora zaidi kuliko vijana wetu wa leo. Katika hili najua nitaonekana kuwa nautukuza ukoloni. Lakini kwanini tusiambiane ukweli?

 

Serikali isiendelee kuimba wimbo wa kutaka wataalamu waliostaafu wathaminiwe huku ikiwa haiwathamini. Na hii si katika sekta ya vitabu tu, bali katika sekta zote za maisha.

 

Tatizo la tatu ni kukosekana kwa ushirikishwaji wa walimu katika masuala ya vitabu. Kukosekana ushirikishwaji walimu katika masuala ya vitabu kumeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya vitabu, hasa vya shule.

 

Tayari nimekwisha kudokeza Wizara ya Elimu ilivyoamua kutoa zabuni kwa wachapishaji vitabu, vilivyosambazwa nchini kote huku walimu wakiwa wameona siku nyingi ubovu wa vitabu hivyo.

 

Binafsi nimebahatika kuendesha semina mbalimbali za walimu. Swali ninalokumbana nalo kila siku ni hili: “Mzee, una maoni gani kuhusu vitabu tunavyoendelea kufundishia? Je, tuendelee kuwafundisha watoto wetu upotofu uliopo vitabuni ili wafaulu mitihani au tufundishe ukweli wa mambo ili washindwe mitihani?”

 

Hii ni kusema kwamba katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, tumeweza kuyapata, lakini yasiyosaidia juhudi zetu za kuboresha elimu.

 

Tatizo la nne la sekta ya vitabu Tanzania ni kuwapo kwa wachapishaji wa vitabu wasio waaminifu, wanaofanya chochote wanachokitaka ilimradi wanufaike huku elimu ikiendelea kudidimia na wakiwaacha waandishi wa vitabu wakiendelea kuwa maskini.

 

Wachapishaji vitabu wanaiba kazi za waandishi wao, wanachapisha vitabu na kuviuza kinyemela bila kuwekeana mkataba na waandishi wenyewe. Tabia hii huwakatisha tamaa waandishi bora wa vitabu. Kwa hiyo, vitabu huandikwa na waandishi wabovu.

 

Kuna wachapishaji wanaoendelea kujinufaisha wenyewe tu huku wakiwapunja waandishi husika malipo ya kazi zao, kwa kisingizio cha gharama kubwa za uchapishaji vitabu.

 

Chukua, kwa mfano, wachapishaji wengi wanawapa waandishi wao mrahaba (malipo) wa asilimia kumi ya mwanzo ya vitabu. Kwa hiyo, wakiuza kitabu kwa Sh 6,000 mwandishi wanampa Sh 600 tu! Wao wanabaki na Sh 5,400. Kumbe mwandishi ndiye chanzo cha kitabu.

 

Halafu kuna wachapishaji wa vitabu wanaotumia umaskini wa waandishi wao kama bahati ya kuwanyonya. Kwa mfano, mwandishi ataandika kitabu kitapitishwa na wizara, mwandishi ataomba kwa mchapishaji mkopo wa Sh 100,000 mchapishaji atamwambia mwandishi hela hiyo haitamaliza shida yake, atamshawishi akope Sh milioni moja kwa sharti kwamba hatafuata chochote kwa mchapishaji.

 

Baada ya hapo mchapishaji ataandika katika kitabu hicho kwamba yeye ni mchapishaji wa kitabu hicho pia ni mwandishi! Mwandishi hapati kitu tena!

 

Tatizo la tano na la mwisho ni ukweli kwamba Serikali haiwajali na inawakatisha tamaa waandishi wa vitabu waliotoa mchango mkubwa katika Taifa hili. Kwa mfano, tupo waandishi wa vitabu tuliotoa mchango mkubwa katika kuelimisha wananchi masuala ya siasa na mengine nchini Tanzania.

 

Kuna wanasiasa na viongozi wengi wa Serikali waliofanya vizuri katika masomo yao ya siasa kutokana na mchango wetu waandishi wa vitabu. Lakini unapofika wakati wa kutunukiwa nishani watu mbalimbali, waandishi wa vitabu waliotoa mchango mkubwa katika Taifa hili hawakumbukwi!

 

Wakati Tanzania haiheshimu waandishi wake wa vitabu, nchi kama Uingereza, Nigeria na hata Kenya zinaheshimu waandishi wao wa vitabu. Kwa hiyo, wana moyo wa kuendelea kutoa mchango wao katika kuboresha sekta ya vitabu.

 

Tena, wakati Serikali haiwajali waandishi wa vitabu inawajali sana wanamuziki wa kizazi kipya ambao nyimbo zao nyingi hazina maana yoyote kwa Taifa hili. Tena baadhi yao wameliletea Taifa hili aibu kwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, lakini Serikali inawapapatikia.

 

Hayo basi ndiyo matatizo makubwa ya sekta ya vitabu Tanzania.