Wakati Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli ikiwa na mikakati ya kupunguza matumizi ya fedha za umma yasiyokuwa na lazima kwa lengo la  kuwaletea wananchi maendeleo, kwa upande wake imeingia katika matumizi yanayozidi kiasi cha mapato yanayokusanywa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa bajeti ya robo mwaka unaoishia Machi 2016, Serikali imekusanya mapato yanayofikia Sh trilioni 3.435, huku kodi ya mapato ikiwa ni Sh trilioni 3.183 sawa na ongezeko la asilimia 1.5, kiasi ambacho  kimevuka makisio kwa kipindi hicho.

Kiasi hicho kinaelezwa katika taarifa ya BoT ni majumuisho ya mapato yote yanayofikia asilimia 89.7 ambayo ni pamoja na fedha za wahisani. Wakati Serikali ikikusanya kiasi hicho cha fedha imetumia Sh trilioni 3.791.

Matumizi kwa shughuli za kawaida kwa kipindi hicho yalikuwa Sh trilioni 3.268 huku shughuli za maendeleo yakifikia Sh bilioni 523.1. Vyanzo vya mapato vya ndani vimechangia kiasi cha Sh bilioni 420.6 kwa shughuli za maendeleo.

 Kwa mujibu ya ripoti hiyo, matumizi ya Serikali  kwa robo mwaka yamefanywa kwa kuzingatia mipango na matumizi muhimu ambayo yanahitajika  ikiwamo  mishahara – makisio yalikuwa Sh trilioni 1.664 fedha zilizotumika ni Sh trilioni 1.682 na malipo ya riba makisio ni Sh bilioni 459.7, fedha halisi iliyolipwa Sh bilioni 331.

 Akizungumza na JAMHURI kuhusu ripoti hiyo iliyotolewa na Benki Kuu, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Humphery Moshi, anasema lengo la Rais John Magufuli tangu alipoingia madarakani lilikuwa ni kubana matumizi.

 “Tunapaswa kutambua kuwa kipindi anaingia alikuta orodha kubwa ya madeni ya makandarasi yaliyotokana na ujenzi katika  maeneo mbalimbali ambayo kwa sasa yanahitajika kulipwa,” anasema Prof Mosha.

 Profesa Moshi anasema matumizi yangekuwa makubwa kutokana na kuwapo kwa madeni mengi ambayo yalikuwa bado hayajalipwa, mfano vyuo vikuu kuna kodi za nyumba nyingi ambazo bado hazijalipwa mpaka sasa.

 “Mzigo huo mkubwa wa madeni aliokutana nao, ni miongoni mwa sababu ambazo zimepelekea (zimechangia) kupanda kwa matumizi kuliko mapato na kile ambacho anaendelea kukifanya katika kubana matumizi hakiwezi kuonekana muda huu kutokana na sababu za kiuchumi, lakini faida yake itachukua muda mrefu kuonekana na kuwa na manufaa kwa Taifa.

 “Hivyo kama unataka kuangalia vizuri kwa hayo anayofanya Rais Magufuli yanaweza kuzaa matunda ni vyema pia kuipitia kwa makini ripoti ya bajeti ya robo mwaka katika mwaka ujao wa fedha, ambayo inaweza kuleta picha halisi katika masuala ya uchumi,” anasema.

 Profesa Moshi anasema kutopangilia miradi ya maendeleo pamoja na matumizi ya kawaida, ni miongoni mwa sababu zinazochangia matumizi makubwa na kulazimisha kukopa kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

“Tanzania kipindi cha nyuma nchi imekuwa ikilazimika kukopa kupitia vyanzo mbalimbali vya ndani au nje ili iweze kufanya mipango yake ya maendeleo kutokana na matumizi kuwa makubwa kuliko mapato yake,” anasema Profesa Moshi.

Prof. Moshi anasema siku za hivi karibuni Serikali imekuwa inakopa kupitia masoko ambayo riba yake inakuwa kubwa, hali inayochangia kushindwa kulipa mikopo kutokana na uwezo wa kiuchumi  kuwa mdogo.

“Kitu cha muhimu ambacho kinatakiwa kuangaliwa kwa mtazamo mpana wa kiuchumi ni tunakopa fedha kwa ajili ya kufanyia shughuli gani, kwani ukikopa kwa ajili kuwalipa watu mishahara basi ni vigumu kupata fedha za kurudisha mkopo huo kutokana na fedha hizo kutozalishwa,” anasema Profesa Moshi.

 Baadhi ya wadau wa masuala ya uchumi nao kwa upande wao wanasema Waziri wa Fedha na Uchumi ambaye ndiye kiranja wa taasisi nzito kama vile Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Amana, Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA), anapaswa kuendelea kuzisimamia kwa ukaribu ili kuleta chachu ya maendeleo.

By Jamhuri