Ushindi wa goli moja la Tottenham dhidi ya Arsenal wiki iliyopita, linamshawishi Meneja wa timu hiyo, Mauricio Pochettino kumtaja mfungaji wake, Harry Kane kuwa ni ‘jembe’ la sasa na baadaye kwa timu hiyo.

Akitumia urefu wake, Kane aliiwezesha timu yake kuibuka na ushindi wa 1-0  kwenye uwanja wa Wembley dhidi ya washindani wao wa soka kaskazini mwa jijini Londoni nchini Uingereza.

Kane aliruka juu na kumzidi Laurent Koscielny wa Arsenal katika dakika ya 49 na kuuelekeza mpira wa krosi uliopigwa na Ben Davies, kisha kumuacha kipa Petr Cech wa Arsenal ‘akigaagaa’ na kuandika goli hilo lililoiwezesha Tottenham maarufu kama Spurs kupanda hadi nafasi ya Ligi Kuu ya Uingereza.

“Harry Kane hajapitwa na wakati, ni muhimu kwa wakati huu na ujao,’amesema Pochettino alipolizungumzia goli safi la mchezaji huyo na kuongeza, “tunajivuna sana kwa yeye kuwa upande wetu.”

Kabla ya ushindi huo, Spurs ilipata ushindi wa goli 2-0 dhidi ya ‘mashetani wekundu’-Manchester United  na kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Liverpool.

“Ninawapongeza wachezaji wetu, tumekuwa na mechi kubwa tatu za mfululizo na wamecheza kwa kiwango cha kuridhisha,” amesema Meneja huyo, raia wa Argentina.

Tottenham waliuanza mchezo dhidi ya Arsenal ‘kizembe’ na kuwafanya washindani wao kutawala mchezo.

Lakini Tottenham iliwazidi ujanja Arsenal ‘waliopotezana’ na kuruhusu matokeo ya mwisho kuwa 1-0.

By Jamhuri