Wiki hii unafanyika uchaguzi mdogo katika majimbo ya Kinondoni, Dar es Salaam na Siha, Kilimanjaro. Uchaguzi huu umeitishwa kutokana na waliokuwa wabunge Godwin Mollel (CHADEMA) na Maulid Mtulia (CUF) kuhama vyama vyao wakajiunga na CCM baada ya kuvutiwa na utendaji wa Rais John Magufuli.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewateua Mollel kuwa mgombea wake Siha na Mtulia kuwa mgombea wake Kinondoni. Kwa upande wa Kinondoni wapo wagombea kutoka vyama 12 walirejesha fomu zao za uteuzi kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni. Uchaguzi katika jimbo hilo na Siha utafanyika Februari 17.
Wagombea waliorejesha fomu Kinondoni ni Maulid Said Mtulia (CCM), Godfrey Fataeli Malisa (TLP), Johnson Mwangosi (SAU), John Januari Mboya ( Demokrasia Makini), Mwajuma Noty Milando–(UMD), Mary Osward Mpangara- (DP) na Rajab Salim Juma (CUF).
Wagombea wengine ni Mwalim Salum Juma (Chadema), Mohamed Majaliwa Mohamed (NRA), George Justine Kristian (CCK), Bashiri Saidi Kiwendu–(AFP) na Ally Omari Abdallah–(ADA TADEA). Kwa bahati mbaya wanaosikika ni wagombea kutoka CCM, CHADEMA na kwa mbali – CUF.
Sitanii, huko Siha, Kilimanjaro wanaochuana ni Elvis Mosi wa CHADEMA na Mollel wa CCM. Yupo mgombea mwingine wa CUF- Lipumba, Tumsifuel Mwanri ambaye wengi wanamwona kama msindikizaji.
Kimsingi katika majimbo haya mawili wanaochuana kwa Kinondoni ni Mwalimu (CHADEMA) na Mtulia (CCM), huku Siha wakiwa ni Mosi (CHADEMA) na Mollel (CCM). Wapigakura wanayo nafasi ya kukumbuka utendaji uliotukuka wa Mollel na Mtulia wakawachagua tena, au wakaangalia madhambi waliyowatendea wakati wakiwa wabunge wakawanyima kura.
Zimekuwapo harakati nzito katika kampeni hizi zinazoendelea. Tumeanza kusikia shutuma za kadi za wapigakura kununuliwa. Tumeanza kusikia mafunzo ya mabaunsa. Hatujasikia taarifa za mikutano ya kampeni kuzuiwa. Tulishuhudia baadhi ya matangazo yakikatika siku ya uzinduzi wa kampeni. Tunazisikia teknolojia za kujiongezea kura zinazotumika ikiwamo chupa za chai, hotpot, wenye kura za ‘reserve’ kupanda dalini na kadhalika.
Kwa Tanzania wapinzani wanalalamikia uchaguzi mdogo uliopita Desemba, mwaka jana. Wanasema katika uchaguzi mdogo wa madiwani vyombo vya dola vilitumika kuwakosesha ushindi. CCM kwa upande wao wanasema hawakutumia vyombo vya dola, bali wananchi wamekubali utendaji wa Rais John Pombe Magufuli.
Sitanii, binafsi sitaki kufanya siasa katika hili. Mazingira ya uchaguzi ulivyotokea na kuitishwa tunayafahamu. Wapo wanaodhani unaweza kupatikana ushindi wa kutumia nguvu na wapo wanaodhani kuwa vyovyote iwavyo, zitapigwa kura za hasira. Ni katika hatua hii tupo njia panda. Wagombea wote hawa hakuna mwenye uhakika wa kushinda moja kwa moja.
Vyama vya upinzani vinaweza kuwa vinahakikishiwa na wananchi kuwa vinapendwa hivyo vikaona ushindi uko mezani, lakini kitu kinachoitwa kura ya siri ni cha kuogopa. Ingekuwa zinapigwa kura za kujipanga mstari nyuma ya mgombea, naamini ingekata mzizi wa fitna. Mgombea angejua walio wake na wasio.
Sitanii, Maulid na Mollel nao wanapaswa kukaa mguu sawa. Nadhani wamesikia kampeni zote walivyoambiwa kuwa ‘wamesaliti’ wapigakura. Wajiandae kupokea matokeo ya aina yoyote. Zipo kura za hasira na zinaweza kutokea. Baadhi ya wapigakura wanaona wamedharauliwa kurejeshwa kwenye uchaguzi huu.
Binafsi ninalo ombi. Zamani wakati tunachunga ng’ombe tukitaka kupimana ubavu tunakuwa na refarii asiye rasmi. Anachukua viganja vyake viwili; cha mkono wa kulia na wa kushoto, kisha anatangaza kimoja ni titi la mama yako na kingine ni titi la mpinzani wako.
Kama kuanzisha ugomvi anasema mwenye nguvu apige titi la mama wa mwenzake.
Likipigwa titi la mama unalitetea kweli kweli. Yule refarii haingilii.
Mnakunjana pale, anayeshindwa ama anakimbia au anatangazwa mshindi wa ndondi kisha unakusanya kuni zako unafunga kimyakimya na kurejea nyumbani ukijiandaa kwa ‘raundi’ ijayo.
Natamani na naomba uchaguzi huu, yule anayesimamia uchaguzi kwa majimbo haya awe mtazamaji na asubiri matokeo yatoke kwenye sanduku la kura. Kubwa ni kila upande ujiandae kushindwa na kukubali matokeo halali. Isiwepo mizengwe itakayokwaza nia hii.
 
Ends…
Please follow and like us:
Pin Share