Serikali ya Rais John Magufuli imejidhihirisha kwa umma, kwamba azma yake ni kuhakikisha wananchi wanyonge wanapata huduma wanazozistahili bila ukiritimba.

Kutokana na dhana hiyo, Mpita Njia anaamini kuwa raia hawapaswi kuombwa rushwa, ‘kuzungushwa’, kunyanyaswa ama kufanyiwa kitendo chochote kinachokiuka haki zao za msingi.

Kwa muda mrefu sasa wananchi hasa wa hali ya chini, wamenyanyasika kutokana na watumishi wa umma wasiokuwa waadilifu kuwanyanyasa, kuwadhulumu haki zao na kuwasababishia hasara, achilia mbali unyanyasaji wa kisaikolojia.

Kwa bahati nzuri, Rais Magufuli hawavumilii watumishi wa umma wanaoshiriki vitendo hivyo na vingine vinavyofanana na hivyo.

Hata wasaidizi wake wakiwamo wakuu wa mikoa, wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanamsaidia Rais Magufuli kuwaona raia wa Tanzania hawanyanyasiki. Nyakati za manyanyaso zimepita.

Ni kutokana na hali hiyo, Mpita Njia ameamua kuweka wazi kuhusu utendaji unaoashiria  vitendo visivyofaa kwa watumishi wa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), kanda ya Mbezi jijini Dar es Salaam.

Mpita Njia amebaini kuwapo matukio kadhaa yasiyoashiria utayari wa Tanesco-Mbezi ‘kusafiri’ njia moja na Rais Magufuli katika kutatua kero za wananchi.

Rekodi zilizomfikia Mpita Njia, zisizotiliwa shaka zikiwamo za sauti, ujumbe mfupi wa maandishi, milio ya simu zisizopokewa na watoa huduma wa ofisi hiyo ni miongoni mwa vielelezo vinavyomshawishi kuona hitaji la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ‘kuimulika’ ofisi hiyo. Kwa maana nyingine ni sawa kuandika,Tanesco-Mbezi ‘wanamtafuta’ Makonda awafunde. Atawafunda.

Vielelezo vinaonesha kuwa baadhi ya watumishi wa Tanesco-Mbezi wameshindwa kukidhi mahitaji ya wateja kunufaika na huduma wanayoilipia na kuliingia pato Taifa.

Yapo matukio mengi, lakini la hivi karibuni kulikatika umeme na baada ya kurejea, baadhi ya nyumba zikikosa nishati hiyo.

Cha ajabu, iliwachukua watumishi wa Tanesco-Mbezi zaidi ya siku tatu kufika kwenye nyumba husika kurekebisha tatizo ili shirika hilo liendelee kupata mapato yake.

Kwa maana kupungua kwa wateja ni kupungua kwa mapato ya Tanesco na hivyo kupunguza pato la Taifa. Mpita Njia anaamini kwamba mtumishi anayeshiriki vitendo hivyo, awe Meneja, Mkuu wa kitengo kama kile cha huduma za dharura ama mfanyakazi wa kawaida, hapaswi kuutumikia umma.

Ingawa yapo maeneo kadhaa ya ufanisi wa huduma za ofisi hiyo, lakini uzembe unaowasababishia wateja kadhia, haupaswi kuvumilika. Kama watumishi waliopo sasa wanashindwa kazi, bora wawachie wenye kwenda na kasi ya Rais Magufuli wachukue nafasi zao. Makonda, watembelee watu hawa.

By Jamhuri