Mbalamwezi
Mbalamwezi

Baada ya kifo cha aliyekuwa msanii nyota wa Bongo Fleva, maarufu kwa jina la Mbalamwezi aliyekuwa anaunda kundi la The Mafik,  mastaa mbalimbali wa muziki wa  Bongo Fleva nchini wametumia mitandao yao ya kijamii kama Instagram  kumuaga nyota mwenzao huyo wa muziki aliyefariki dunia Ijumaa iliyopita na kuzikwa siku iliyofuata kwao Tandika, jiijini Dar es Salaam.

Msanii wa muziki wa miondoko ya kufokafoka maarufu kama Hip hop, Stamina, aliandika katika akaunti yake ya mtandao wa Instagram: “Sisi ni mavumbi na tutarudi mavumbini. Mungu akuepushe na adhabu ya kaburi.”

Naye msanii nguli nchini, Diamond Platnumz, kupitia akaunti yake ya mtandao wa Instagram aliandika: “May your soul rest in Paradise.”

Naye nyota wa muziki wa Hip Hop, Fid Q, kupitia mtandao wa Instagram alimuaga Mbalamwezi huku akiweka picha ya mshumaa unaowaka akisema: “ Inna lillah wainna ilaih raajiuun… Pumzika pema kaka Mbalamwezi – The Mafik.”

Naye msanii anayetamba na ngoma ‘We Endelea Tu’, Mwana FA, kupitia mtandao wake wa Instagram naye alimuaga  Mbalamwezi kwa kuandika: “Pumzika kwa amani mdogo wangu… doh!’’

Vilevile msanii mkongwe na Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Joseph Haule, maarufu kama  ‘Professor Jay’ kupitia mtandao wa Instagram naye aliandika: “Daaah! Kipaji kingine kikubwa kimezimika kama mshumaa. Pumzika kwa amani mdogo wangu Mbalamwezi, poleni sana. The Mafik, ndugu na jamaa wote.”

Msanii Mbalamwenzi ana sifa enzi za uhai wake kuwa mahiri katika kuimba na sauti yenye kuvutia wapenzi wengi wa burudani hasa wa muziki wa Bongo Fleva.

Kundi la The Mafik limekuwa likifanya vizuri katika muziki wa Bongo Fleva tangu kuanzishwa kwake hivi karibuni baada ya kukonga nyoyo za wapenzi wengi wa muziki. Mbalamwezi alikuwa akichagiza, hasa namna alivyokuwa akitumbuiza katika ‘show’ ambazo kundi hilo lilikuwa likitumbuiza katika majukwaa mbalimbali.

Kundi la The Mafik kwa pamoja lilikuwa linajumuisha nguli watatu ambao ni Hamadai, Rhinoking na marehemu Mbalamwezi. Kutokana na juhudi zao, kibao chao cha ‘Passenger’ kiliwapa umaarufu na kujulikana mapema kupitia tasnia ya muziki wa kizazi kipya, hali iliyowafanya wajipatie mashabiki wengi ndani na nje ya nchi.

The Mafik wametoa vibao vingi ambavyo vyote kwa pamoja vinafanya vizuri ikiwemo kupigwa katika vituo mbalimbali vya redio na runinga pamoja na kutazamwa kwenye mtandao wa Youtube. Ngoma hizo zinazobamba ni pamoja na wimbo wa ‘Passenger’, ambapo katika mtandao wa Youtube umeangaliwa na watazamaji zaidi ya milioni moja na laki mbili. Ngoma nyingine ni ‘Carola’, ‘Vuruga’ na ‘Bobo’.

By Jamhuri