Kylian Mbape, mshambuliaji mahiri wa PSG ya Ufaransa anatajwa kuwa ndiye mchezaji ghali duniani hivi sasa akiwa na thamani ya Euro milioni 265.2, akifuatiwa na Raheem Starling wa Manchester City ya Uingereza mwenye thamani ya Euro milioni 223.7.

Lakini makinda wawili wa Chelsea, ambao wameaminiwa na Kocha wao, Frank Lampard, nao wamechomoza katika nafasi za juu katika orodha ya thamani ya wachezaji iliyotolewa hivi karibuni na The International Centre for Sports Studies (CIES). Makinda hao, Tammy Ibrahim na Mason Mount wamo ndani ya wachezaji 30 wenye thamani kubwa duniani.

Wakai Tammy akiwa katika nafasi ya 17, akiwa na thamani ya Euro milioni 87.4, Mount ameibuka katika nafasi ya 26 akiwa na thamani ya Euro milioni 79.7.

CIES ni taasisi inayojihusisha na utafutaji wa takwimu katika masuala la soka barani Ulaya, ikizihusisha ligi kubwa tano barani humo.

Ili kukadiria ada za uhamisho ambazo wachezaji watazidai, taasisi hiyo huzingatia kujituma kwa mchezaji uwanjani, katika klabu yake na katika timu ya taifa, matokeo ya klabu na timu ya taifa, umri wa mchezaji, nafasi anayocheza, ligi anayocheza na hali ya uchumi ya klabu anayotoka.

Orodha iliyotolewa hivi karibuni inahusisha wachezaji ambao CIES inaamini kuwa wana thamani ya zaidi ya Euro milioni 50. Wachezaji wengine wa Chelsea waliomo katika orodha hiyo ni pamoja na Kepa Arrizabalaga, Christian Pulisic, Jorginho, Callum Hudson-Odoi, N’Golo Kante, Fikayo Tomori, Mateo Kovacic, Ross Barkley na Kurt Zouma.

Hata hivyo, inaaminika kuwa orodha hiyo itazua gumzo miongoni mwa mashabiki, kwani kuna wachezaji ambao wana majina makubwa hivi sasa lakini thamani yao imeonekana kuwa ndogo.

Wakati Mbape akikamata nafasi ya juu akifuatiwa na Sterling, nafasi ya tatu imekwenda kwa Mohammed Salah (mashambuliaji wa Misri na Liverpool).

Kwa kuzingatia nafasi mchezaji anayo cheza, golikipa wa Liverpool, Alisson Becker, anaongoza katika nafasi hiyo akiwa na thamani ya Euro milioni 87. Virgil van Dijk anaongoza katika nafasi ya mabeki wa kati akiwa na thamani ya Euro milioni 93. Trent Alexander-Arnold naye anaongoza kwa walinzi wa pembeni akipewa thamani ya Euro milioni 110. Wachezaji hawa wote wanatoka Klabu ya Liverpool ya Uingereza.

Nafasi ya kiungo inatawaliwa na James Maddison, mwenye thamani ya Euro milioni 112 na Kylian Mbappé anaongoza kwa upande wa washambuliaji.

Wachezaji 11 miongoni mwa 20 ambao thamani yao inazidi Euro milioni 100 wanatoka katika klabu zilizomo katika Ligi Kuu ya Uingereza.

Kuna wastani wa wachezaji wawili wenye thamani ya zaidi ya Euro milioni 100 kutoka katika kila ligi miongoni mwa ligi tano zinazotazamwa katika orodha hiyo. Watatu wanatoka La Liga (Messi, Griezmann na João Felix). Wawili wanatoka Ligue 1 (Mbappé na Neymar). Wawili ni kutoka Serie A (Martínez na Lukaku), na wawili ni kutoka Bundesliga (Sancho na Werner).

283 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!