Kocha gani ataiweza Ligi Kuu?

Kocha anayedumu ndani ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa zaidi ya misimu mitatu anastahili kupewa pongezi siku ile anayopewa barua ya kufukuzwa kazi.





Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime, ni mmoja wa makocha ambao wamedumu katika klabu moja kwa muda mrefu.

Wengi wao wakidumu sana ni msimu mmoja tu, baada ya hapo sababu za ajira kusitishwa huwa ni nyingi na zote ni figisu au uhalali wa kutimuliwa. Mfano tu, kwa misimu kadhaa sasa Simba imekuwa ikiendelea kutafuta kocha mwenye hadhi ya timu inayotafuta nafasi ya kusaka mafanikio makubwa Afrika.

Kulikuwa na Kocha Dylan Kerr ndani ya Simba, ambaye hakuridhishwa na wafungaji anaoletewa na kwa jinsi siku zilivyokuwa zinakwenda bila ya mfungaji mwenye ubora kupatikana, uongozi ulikuwa katika hali ya kuchanganyikiwa.

Wakati mazoezi ya Simba na Yanga yakiendelea, uongozi uliendelea na zile pilikapilika za kuimarisha timu.

Yaani programu za makocha zinaendelea, wakati huohuo kunakuwepo na wachezaji wapya wanaoletwa kwa ajili ya kuimarisha timu. Katika dirisha dogo lililopita Simba imefanya jambo la maana kwa kuamua kusajili kwa utulivu, huku Yanga wakiamua kubomoa kikosi kabisa.

Matarajio ya wanachama, mashabiki na wadau wa soka kwa ujumla ni kuona klabu zetu zinacheza soka la ushindani, lakini makocha wenye jukumu la kuusimamia utimamu wa mchezaji mmoja mmoja, wanakuja na ukweli ambao haupaswi kuchukuliwa kama habari isiyo na umuhimu.

Wataajiri makocha, lakini wanasahau mtaalamu wa afya ya viungo. Kuna changamoto mpya inayojitokeza kupitia namna tunavyosajili wachezaji wapya, ambao wengi wao hawana utimamu wa miili.

Changamoto ya kwanza inakwenda kwa TFF kama walezi wa soka la nchi, ya pili inakwenda kwa klabu zinazoingia gharama ya kutafuta makocha pamoja na wachezaji. Ushindani unaotegemewa kuonekana wakati Ligi Kuu ikiwa inaendelea, ni mafanikio ya mchanganyiko wa mambo mengi ya nje ya uwanja.

Kuajiri makocha kutoka kila kona ya Bara la Ulaya ni hatua ya mwanzo kabisa ya kutafuta mabadiliko ya uchezaji. Nini kinafuata baada ya makocha kuanza kazi huku wakikikosa wanachokitegemea kutoka kwa wachezaji, kwa sababu miili haina uimara wa kuweza kuendana na ugumu wa mafunzo?

Kumleta kocha wa Kizungu ni mwanzo wa vita ya kuimarisha timu, si dawa ya ubovu wa wachezaji wetu, kwa maana ya viwango vya mchezaji mmoja mmoja.

Anayemtafuta mwalimu wa kigeni awe tayari kumtafuta mwalimu wa viungo atakayewatengeneza wachezaji na kukabiliana na kila upungufu unaoweza kusababisha timu ikacheza soka la kiwango cha chini, tofauti na matarajio yaliyokuwepo wakati msimu wa Ligi Kuu ulipoanza.

Kocha wa Simba, Sven van der Broeck, bado hajaridhishwa na uwezo wa wafungaji wetu, lakini ni hawa hawa ambao wamekuwa wakitumika kwa misimu kadhaa. Wanapata nafasi saba, wanaitumia vizuri nafasi moja na baada ya mechi kadhaa za Ligi Kuu, kocha wa timu ya taifa analazimika kuwaita kwa ajili ya mechi za Taifa Stars!

Kocha wa Kizungu anapoajiriwa haitazami heshima ya mchezaji, anaangalia uwezo wake kwa vigezo anavyovitambua yeye kama kocha mkuu. Shabiki wa jukwaani hataki matokeo mengine isipokuwa ushindi na wachache kati yao wanao uwezo wa kuvumilia wakati benchi la ufundi likitengeneza timu ya ushindi kwa kuwatumia wachezaji wetu hawa hawa.

Kazi ya kocha mkuu wa timu yenye malengo makubwa ni nzito sana, kwani wanaomuajiri wanayo presha ya kuiona timu yao ikiwa na ubora walioutegemea wakati msimu wa usajili ulipoanza.

Charles Boniface Mkwasa

“Tuna kazi kubwa, lakini huu ni mwanzo, naamini Ligi Kuu inazidi kupanda hadhi siku hadi siku na kikubwa zaidi ni kuhakikisha tunakuwa na wataalamu wengi katika kila eneo.”

Mkwasa ambaye ni msaidizi wa Luce Eymael aliye Kocha Mkuu wa Yanga, anaamini wachezaji wengi wana vitu vingi wanavipata, lakini inapaswa kwa vile walivyonavyo lazima wapambane.

“Angalia Mbwana Samatta, nidhamu imemfikisha mpaka alipo na huu ni mwanzo mzuri, kwani wengi wataona wivu na siku ya mwisho tunatakiwa tuwe na akina Samatta wengi.”

Sven van der Broeck

Kocha huyu aliyerithi mikoba ya Patrick Aussems ndani ya Simba anakubali lazima wataalamu wengi wazalishwe ndani ya sekta ya mpira wa miguu ili kufikia malengo yanayotakiwa.

“Tanzania itafanikiwa tu, ila ukweli lazima wataalamu wengi wazalishwe katika kufikia malengo yale yanayotakiwa.” 

Mohammed Dewji

“Ndiyo maana kwetu tunaanza kwa kuzalisha wachezaji kuanzia chini, tunataka tuwe na kitu tofauti kabisa na wale wanaopita Simba wajue falsafa ya timu.”

MO Dewji ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, anasema ana uhakika mkubwa klabu hiyo muda si mrefu itakuwa kama Al Ahly, TP Mazembe au Esperance.

Luce Eymael

Kocha wa Yanga ambaye alipoulizwa swali la juu ya umuhimu wa wataalamu katika kila sekta, alikiri ni kitu kisichokwepeka kabisa.

“Naweza kusema neno moja tu, ni lazima ili timu ifike katika malengo inayoyataka.”

Maoni

Baadhi ya wachezaji wanashindwa kuendana na kasi za ligi kuu za nchi jirani na wanaamua kurudi tena kuchezea timu zetu. Wanarudi mahali walipopazoea katika ligi kuu ambayo ushindani binafsi si kitu chenye kutiliwa mkazo. Kuna timu za mikoani ambazo zinakuja Dar kwa ajili ya mazoezi ya mwanzo wa msimu kutokana na jiji hili kuwa na miundombinu yenye afadhali. Kuna nyingine hujiandaa katika mazingira magumu zaidi.

Hivyo kazi za makocha wa Ligi Kuu huathiriwa na mambo mengi. Wanaowaajiri makocha wasiwe wepesi katika kufikia hitimisho kwamba wameshindwa kazi.

TFF inao wajibu wa kuzifuatilia klabu kwa ukaribu zaidi, kwa nia ya kukabiliana na matatizo yanayochangia katika kupunguza ushindani baina ya timu zetu. Si kila timu inaweza kuweka kambi nje ya nchi au visiwani Zanzibar, huu uwe ni mwanzo wa kuipandisha hadhi Ligi Kuu.