Maswali yasiyo na majibu! Wakati Simba inalikosa Kombe la Mapinduzi, kukazuka taarifa kwamba Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohammed Dewji ‘MO’, ameamua kubwaga manyanga.

Si kuondoka ndani ya Simba, bali ni kujiondoa katika nafasi ya mwenyekiti na kubaki kama mwekezaji. Maneno haya yalipitia katika mitandao yake ya kijamii.

Akiwa miongoni mwa watu wanaotazamwa sana, ujumbe wake ukasambaa kwa kasi na kila kitu kikaonekana dhahiri. Watu walishambulia na wengine wakipongeza.

Kwa wapenda soka lilikuwa ni wingu jeusi baada ya ujumbe wa bosi huyo kupitia akaunti zake za Twitter na Instagram kutangaza kijiuzulu nafasi hiyo ya uenyekiti na kubakia katika nafasi ya mwekezaji tu, kwa madai kuwa analipa mishahara takriban Sh bilioni nne kwa mwaka, lakini haridhishwi na uwajibikaji wa timu.

Ujumbe huo ulisambaa kwa kiasi kikubwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii dakika kadhaa baada ya mchezo wa fainali wa Kombe la Mapinduzi kati ya Simba na Mtibwa Sugar. Simba ilichapwa na Mtibwa Sugar bao 1-0.

Wenye akili walijiuliza maswali mengi na kuona hapa ni ‘changa la macho’, na ndivyo ilivyokuwa, kwani alitumia tena ukurasa wake huohuo kuelezea kusitikitishwa na kilichotokea kwenye akaunti zake hizo, akibainisha yeye ni Simba damu na hana mpango wa kuondoka, akitaka Wanasimba wawe na amani kabisa.

“Oh! Nini kilitokea kwenye akaunti zangu jana? Tuko pamoja tunajipanga kwa ajili ya ligi tuko imara nawapongeza Mtibwa kwa kuchukua kombe. Mimi ni Simba damu damu na nitaendelea kuwa Simba,” ulisomeka ujumbe wa MO kupitia akaunti zake zote hizo mbili.

Ikumbukwe kuwa ule ujumbe wa awali ambao yeye mwenyewe aliushangaa, uliwafanya mashabiki wa Simba kuingiwa ubaridi kwelikweli, huku baadhi ya viongozi wa juu pia wakitumia kurasa zao kuonyesha kusikitishwa na ujumbe huo.

Miongoni mwao ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akiamini kuwa akaunti ya bosi huyo ilivamiwa. “Matokeo ya mpira huleta furaha na huzuni kwa wanaofungwa. Natoa pole kwa timu yangu ya Simba pamoja na mashabiki wote na wanaoitakia mema Simba, sina uhakika na kinachoendelea kwenye AC (akaunti) ya MO kama Mohamed Dewji mwenyewe ameandika.”

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangala, ambaye pia ni mnazi wa Simba akisema: “Poleni Wanasimba wenzangu, kimetuvuruga.”

Awali mwekezaji huyo alidai kwamba hawezi kupoteza mamilioni ya fedha kwa ajili ya timu hiyo ilhali wachezaji hawajitumi wala kujua thamani ya klabu hiyo.

Mwekezaji huyo alikiri kwamba jambo ambalo linamnyima raha ni pale timu hiyo inapofungwa na wachezaji kushindwa kutambua thamani ya klabu hiyo.

Nini kilitokea?

Kuna mambo mawili kwa MO Dewji; alitikisa au alitikiswa? Kutikisa, labda alitaka kupima imani ya mashabiki kwake na kutikiswa kama alilazimishwa kurudi ndani ya klabu hiyo.

Hapa ndipo unapoanza kuifikiria Mbagala Market, African Lyon na Singida United na kujiuliza maswali mengi. Alitikisa? Analipa mishahara ya wachezaji Simba au Simba Sports Club ndiyo inayolipa mishahara?

Je, alitikiswa na kulazimishwa kurejea Simba ili asifanye yale ya African Lyon na Singida United? Kwa nini aliziacha timu hizo? Maswali ni mengi.

Hata hivyo, Wanasimba hawana sababu ya kupata hofu sasa, kwa sababu mwekezaji ametangaza kuendelea na majukumu yake. Kwa upande mwingine, Kaimu Rais wa Simba, Mwina Kaduguda, anasisitiza Simba bado ni imara na itaendelea kuwa imara, kikubwa tu kwa mashabiki ni kuendelea kuwaamini.

Hilo pengine limejidhihirisha kwa matokeo ya mechi ya wiki iliyopita baada ya kuitandika Mbao 2-1 katika Uwanja wa CCM Kirumba kule Mwanza.

1051 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!