Mpaka utakapokuwa unasoma makala hii kuna uwezekano mkubwa kuwa Mbwana Samatta atakuwa tayari amekwisha kuwa mchezaji rasmi wa Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu nchini Uingereza (EPL). Anakuwa mmoja wa wachezaji ambao wamenufaika na dirisha dogo la usajili katika Bara la Ulaya.

Wakati Aston Villa, iliyo katika hatari ya kushuka daraja katika msimamo wa EPL imemwona Samatta kama mmoja wa wachezaji ambaye anaweza kuisaidia timu hiyo ibakie kwenye ligi, nahodha huyo wa Taifa Stars anaandika historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza kwenye Ligi Kuu nchini Uingereza.

Lakini Samatta anapaswa kufanya mambo zaidi ya hilo la kuandika historia. Anapaswa kuwaonyesha Aston Villa kwa vitendo kuwa hawakukosea kumsajili. Samatta anatakiwa kufanya mambo ambayo yatamjenga yeye mwenyewe kama mchezaji, na kulijenga jina la nchi. Samatta anapaswa kufahamu kuwa ameshikilia ufunguo wa Watanzania wengi kucheza EPL au ligi nyingine kubwa Ulaya.

Lakini hilo si jukumu la Samatta peke yake. Wakati yeye ana sehemu ya kufanya na wachezaji wenye nia na dhamira ya kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya nao wana sehemu kubwa zaidi ya kufanya kwa sababu atakachofanya Samatta ni kuwasaidia kufagia njia na uamuzi wa kuifanya safari ni wa kwao wenyewe.

Ili kumwezesha Samatta kufanya hivyo, ni vema Watanzania wakamuunga mkono kwa kila hali ili kuhakikisha kuwa maisha yake ya soka nchini Uingereza yanakuwa mazuri. Ni kweli kuwa wapo ambao hawajafurahishwa na Samatta kwenda Aston Villa. Wanaweza kuwa na sababu mbalimbali lakini Samatta asiwaone hao kama maadui, bali watu ambao wanampa changamoto ya kuwa mzuri zaidi.

Villa ilikuwa imetenga pauni milioni 8.5 kumnunua mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27 kutoka KRC Genk ya Ubelgiji, aliyojiunga nayo misimu miwili iliyopita akitokea TP Mazembe ya DRC. 

Mashabiki Aston Villa wamkubali

Samatta anaingia Aston Villa huku mashabiki wengi wa klabu hiyo wakimkubali kutokana na vitu mbavyo alivionyesha akiwa Genk ya Ubelgiji.

Wakiandika katika mitandao ya kijamii, mashabiki hao wamewasifia wasaka vipaji wa timu hiyo kwa kumleta mtu sahihi na kwa wakati muafaka.

“Wasaka vipaji wako sahihi kwa asilimia 100. Mbwana Samatta ni chaguo sahihi, ana uchu na kiu ya kufunga mabao. Kama angekuwa ameanza msimu na sisi kwa hakika angekuwa mfungaji bora,” anaandika shabiki mmoja.

Shabiki mwingine anasema ana uhakika Samatta ataingia Aston Villa na moto na kuhakikisha anamaliza tatizo la umaliziaji katika timu hiyo.

“Ninashukuru sana tunapata mshambuliaji kama huyu tofauti na wale tuliokuwa tunawasikia wakitajwa wiki zilizopita. Anaonekana anajua goli liko wapi. Ni matarajio yangu kuwa ataizoea ligi haraka sana,” anaandika shabiki anayejitambulisha kama Gav1827.

Shabiki mwingine anasema Samatta anaonekana kuwa ni mzuri kuliko Islam Slimani au Piatek, ambao ni kati ya washambuliaji wanaopewa sifa sana katika EPL.

Kutokana na jitihada zake za kujinasua kutoka balaa la kushuka daraja, Villa ilikuwa imepanga kusajili washambuliaji wawili katika dirisha hili dogo la majira ya baridi. Hivyo, Samatta hatakuwa mshambuliaji pekee ambaye ataingia Aston Villa katika kipindi hiki.

Mshambuliaji mwingine ambaye amekuwa akiwindwa na klabu hiyo ni Sliman, ambaye kwa sasa anakipiga kwa mkopo huko Monaco ya Ufaransa, akitokea Leicester City ya Uingereza.

Makali ya Samatta

Samatta ameivutia Aston Villa na klabu nyingine kadhaa barani Ulaya kutokana na mambo aliyoyafanya akiwa Genk. 

Msimu uliopita aliibuka kuwa mfungaji bora katika ligi ya Ubelgiji na kuisaidia klabu yake kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Aliendelea kuonyesha makali katika ligi hiyo, kwani licha ya timu yake kutofanya vizuri lakini yeye alifanikiwa kufunga magoli kadhaa, moja likiwa dhidi ya timu yenye ukuta wa chuma na mabingwa wa dunia kwa sasa, Liverpool.

Alikotoka

Kabla ya kujiunga Genk, Samatta alikuwa akiichezea TP Mazembe ya DRC. Samatta alijiunga KRC Genk Januari 29, 2016 akitokea TP Mazembe kwa ada ya uhamisho ya Euro laki nane.

TP Mazembe ilimsajili Samatta kutokea Simba ya Dar es Salaam Julai 1, 2011 kwa ada ya uhamisho inayotajwa kuwa Euro 70,000.

Simba ilimsajili mchezaji huyo kutokea African Lyon nayo ya Dar es Salaam Julai 1, 2010. African Lyon ilimuona Samatta kama mchezaji mzuri wakati akisakata soka katika klabu za mtaani za huko Mbagala.

Akizungumza na vyombo vya habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam, baba wa Mbwana, Ali Samatta, ameonyesha kumuamini mtoto wake huyo na kubainisha kuwa huo ni mwanzo tu wa mambo makubwa ambayo Samatta atayafanya katika soka.

Mzee Samatta, ambaye pia ni mchezaji wa mpira wa miguu mstaafu, ndiye chachu kubwa iliyomfikisha Mbwana hapa alipo leo, kwani licha ya mafunzo anayokutana nayo akiwa katika timu anazozichezea, mzee huyo amekuwa akimpatia mwanawe wosia wa jinsi ya kujitunza kama mchezaji, ambao amekuwa akiuzingatia, hivyo kufikia mafanikio anayoyaonyesha.

1037 Total Views 10 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!