Ilikuwa Jumamosi ya Machi 17, 2018 nchini Misri. Dakika 90 zinamalizika kwa sare tasa katika dimba la Port Said katika mechi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika ambapo Al Masry ya Misri iliikaribisha Simba ya Tanzania. 

Ahmed Gomaa na washambuliaji wenzake kina Bance na Grendo hawaamini kama wameshindwa kutikisa nyavu na ustaa wao wote.

Ilikuwa ni bonge moja ya mechi huku Simba ikitumia mfumo 3:5:2. Pamoja na kufanikiwa kutofungwa katika mechi hiyo, lakini matokeo hayo yaliitupa nje Simba baada ya sare ya 2-2 jijini Dar es Salaam. Hakuna aliyelalamika sana. Si mashabiki wala kocha wa timu hiyo, wakati huo Mfaransa Pierre Lechantre.

Kati ya wachezaji waliofanya kazi kubwa mno siku hiyo ni beki wa kati, Yusuph Selemani Mlipili. Si tu alikaba, lakini pia kiwango chake cha hamasa binafsi kilikuwa juu sana mithili ya mpiga ngoma kubwa. Alikaba hadi vema, alifanya kila kitu ambacho beki anatakiwa kufanya na nyongeza. Ndiyo maana pamoja na ustaa wao, washambuliaji wa Al Masry walishindwa kuzifumania nyavu siku hiyo.

Achana na hiyo, rudi Septemba 24, 2012 mechi moja ya kibabe sana inapigwa ikiikutanisha Simba dhidi ya African Lyon pale kwenye ‘Shamba la Bibi’. Simba inashinda  magoli 3-0, lakini uwanja mzima unashangaa kijana beki mmoja chipukizi alivyoweza kumzuia Mganda, Emmanuel Okwi, asifurahie mpira siku hiyo. 

Mlipili akicheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza akiwa na jezi ya African Lyon baada ya kushinda mchujo wa usajili uliohusisha kundi la wachezaji zaidi ya 70 pale kwenye viwanja vya Sigara (TCC), Chang’ombe. Anakutana na Simba yenye Okwi anakichafua vibaya sana.

Lakini leo hii asikiki tena. Yupo wapi Mlipili? Atakuwa wapi kesho? Kwa nini hachezi? Ana nafasi gani Simba?Maswali haya yamenifanya nimtafute mtu akamwambie Mlipili mambo kadhaa.

Pascal Sergie Wawa Sfondo ana urefu wa meta 1.78, Erasto Edward Nyoni ana urefu wa meta 1.78, Mbrazili Traione Santos da Silva ana urefu wa meta 1.91 na Kennedy Wilson Juma naye pia ni mrefu. Hawa wote ni mabeki katika Klabu ya Simba.

Hapa ndipo alipo mchawi wa Mlipili. Hawa ndio washindani wa Mlipili pale Msimbazi na hayupo hata mmoja wao anayelingana naye kwa kimo. 

Kocha wa Simba aliyepita, Patrick Aussems, alionekana ‘karogwa’ na mabeki warefu. Aliupenda uwezo wa Mlipili lakini alizidiwa na limbwata la ‘matolu’. Ndiyo maana huku akijua kuwa Mlipili, Wawa na Nyoni wapo, akasajili mabeki wapya wawili (Kennedy na Traione) kwa sababu katika mipango yake Mlipili si beki tegemeo.

Nendeni mkamwambie mtoto huyu wa kipa wa zamani ya Pamba, Mseto na Reli ya Morogoro, marehemu Selemani Mlipili, atafute timu itakayompa nafasi. Simba wanapenda kipaji chake ila hawaupendi ufupi wake.

Amekuja Sven Ludwig Vandenbroeck bado mambo yamekuwa magumu kwa Mlipili. Imekuwa rahisi kwa ngamia kupenya kwenye tundu la sindano kuliko yeye kuanza kikosi cha  kwanza. Ili uone maajabu Simba haijamuacha Mlipili licha ya kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kipindi cha miaka miwili mfululizo.

Nataka nimtume mtu kwa huyu mtoto wa mchezaji  wa zamani wa netiboli Timu ya Taifa  na Halmashauri  ya Mji wa Morogoro, Stella Kanuti Msata, akamweleza kuwa dunia haijasimama kumsubiri. Dunia inafahamu kipaji chake lakini anahukumiwa  na kimo chake.

Asikubali kuendelea kusubiri kudra za Mwenyezi Mungu. Akumbuke umri unakwenda. Kama amesahau ninamkumbusha tu, amezaliwa Aprili 4, 1989 pale Mwananyamala na ifikapo mwaka 2025 atatimiza umri wa miaka 36. Atakuwa na bahati sana kama dunia ya soka bado itakuwa inamhitaji wakati huo.

Najua kuna baadhi ya wasomaji hapa wamekwenda shule lakini wameiacha shule shuleni na kurudi na vyeti vya kuringishia. Hawa kwenye andiko hili hawataelewa kuwa sijasema Mlipili hatacheza kabisa Simba, au ni mchezaji mbaya. Ninachojaribu kusema nafasi yake ni finyu kwenye akili za makocha wanaopita Simba.

Nataka nimtume mtu kwa Mlipili akamwambie kwamba kuna tofauti kati ya kuwa hai na kuishi. Kwa sasa ndani ya kikosi cha Simba yeye yupo hai tu ila haishi.

Amwambie pia mbio za maisha ni za ajabu sana. Anayetafuta hachoki na aliyepata naye anataka zaidi, ndiyo maana Traione ameuacha msitu mkubwa zaidi duniani wa Amazon kwao Brazil akaja Tanzania kuushangaa msitu wa Nyambwiga, Ulanga.

Kutokana na kipaji chake cha soka sijawahi kumuona akiwa benchi tangu anacheza ligi daraja la kwanza kwa ‘wahuni’ wa Morogoro  pale Rhino FC, kabla ya kwenda kwa wauza  mitumba wa Ashanti, baadaye AFC ya Arusha, kabla ya kutua African  Lyon.

Basi, ninamshauri ili achague jibu sahihi kati ya kushindwa na kutojaribu anapaswa ama aanze kujifunza kucheza beki wa pembeni, au ampishe Vandenbroeck na Simba yake arudi baadaye akiondoka.

Hizi falsafa na mbinu za makocha wa kileo zimeharibu sana vipaji. Leo wachezaji wenye vimo vya Mlipili ama utawakuta katikati ya uwanja kama viungo, au pembeni  kama mabeki na mawinga. Ili mchezaji mfupi apangwe eneo la katikati kama ushambuliaji au beki, inabidi awe na kitu cha ziada na cha kipekee kama ilivyokuwa kwa Tobero Carlos au Lionel Messi.

Kitaalamu nafasi ya ulinzi haihitaji mchezaji mwenye kasi sana. Kasi kubwa ya mchezaji huathiri pia uwezo wa kufikiri na kimaamuzi kwa mchezaji husika. Uamuzi wa beki ya kati unapaswa kuwa sahihi zaidi kwa sababu kosa lolote linaweza kuigharimu timu.

0629500908

nnnguzo@gmail.com

2975 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!