Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilituhumiwa kuendesha njama za kuifanya Serikali isitawalike.
Sababu kuu iliyowapa nguvu wabaya wa Chadema kusema hivyo ni uamuzi wa chama hicho cha upinzani kukataa kutambua ushindi wa Rais Jakaya Kikwete.


Nakumbuka nilikuwa miongoni mwa tuliokataa hadaa hizo za wanasiasa za kwamba Chadema walikuwa na ubavu wa kuifanya Serikali isitawalike.
Mgomo wa madereva na vurugu zilizofanywa na vibaka wakati wa mgomo sehemu mbalimbali nchini, umenikumbusha kisa hicho cha mwaka 2010 ambacho kiliendelea hadi mwaka 2011. Nilikuwa miongoni mwa tulioamini na tunaoendelea kuamini kuwa wanaofanya Serikali isitawalike ni hawa hawa waliopewa dhamana ya kuiongoza Serikali.


Sioni sababu ya kutumia maneno mengine zaidi ya kusema tuna kundi kubwa mno la viongozi dhaifu ambao wakati mwingine unajiuliza waliwezaje-wezaje kuwa viongozi! Wapo waliofika mbali zaidi na hata kuanza kuamini kuwa huenda tukawa na viongozi wanaopata uongozi kwa nguvu za kiza. Wanaoamini hivyo wanajenga hoja kwa matukio mengi ya ajabu ajabu yanayotokea wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu.


Tuna viongozi wasiokuwa na visheni kiasi kwamba wakati mwingine mtu unabaki ukijiuliza; nani mwenye makosa kati ya anayeshauri na anayeshauriwa!
Watanzania wamekata tamaa kutokana na uongozi dhaifu wa Taifa letu. Nakumbuka wakati fulani Serikali iliwasilisha bungeni muswada wa sheria iliyokusudiwa kuyabana makanisa na misikiti kulipa kodi kwa baadhi ya vitu. Uamuzi huo ulitokana na taarifa zisizotiliwa shaka kwamba wapo viongozi wa kidini wanaotumia mwanya huo kuingiza vitu vyao vingi vya thamani bila kulipa kodi.   Ukawa hapo mfano wa askofu mmoja aliyetumia kanisa lake kuingiza magari bila kulipa ushuru akiongopa kuwa ni ya kanisa, lakini baadaye yakakutwa yanafanya kazi kwenye kampuni ya kusafirisha watalii.


Makanisa na misikiti waliposikia mpango wa Serikali wa kuweka kodi, wakaitisha Serikali kweli kweli. Waziri Mkuu Mizengo Pinda akawaita waandishi wa habari mjini Dodoma. Akatangaza kutengua uamuzi wa Serikali kwa kigezo kuwa “Serikali ya CCM ni sikivu”.
Nakumbuka sikumwuliza swali, lakini nilimpa maoni yangu kwa kusema: Waziri Mkuu, kama Serikali mnakuwa hamna msimamo wa dhati kwenye mambo makubwa kama haya kwa manufaa ya Taifa zima, kila siku mtasumbuliwa. Kila siku mtatengua uamuzi wenu…kwa maneno mengine mtachezewa. Nikasema si jambo la kawaida kwa Serikali yenye wataalamu na washauri mbalimbali, ikashindwa kutumia hivyo vichwa kufikia uamuzi kabla ya kuutangaza kwa umma. Je, ina maana mlipoamua kuwasilisha muswada huu hamkujua ukinzani utakaotokea na namna ya kuukabili?


Tangu wakati huo Serikali yetu imekuwa kama mwanasesere. Inachezewa tu na kila anayetaka. Imekuwa si Serikali yenye kuamua jambo kwa umakini na kulisimamia. Kwa mfano, hivi sasa kila jambo bovu linalosababishwa na udhaifu wa Serikali yenyewe ni kawaida kusikia viongozi wa kidini wakiombwa wawahimize wafuasi wao kuliombea Taifa.


Waziri wa Maliasili na Utalii anashindwa kubuni mbinu za kukabiliana na ujangili na majangili, anaamua kutumia mamilioni ya shilingi kuwastarehesha viongozi wa kidini kwa kuwapeleka katika ziara eti wasaidie waamini wao kupambana na ujangili. Badala ya kuwapa fedha na vitendea kazi watumishi wa wizara, hasa walio maporini, mamilioni yanatumiwa kuwalaza hoteli za nyota tano masheikh na wachungaji. Huu ni udhaifu mkubwa.


Kuna tukio la kugomewa kwa mashine za kielektroniki za EFD. Ukisikiliza hoja za wafanyabiashara, utabaini wazi kuwa wana hoja za msingi. Ukiwasikiliza TRA utabaini kuwa wanachofanya ni kutekeleza shinikizo la Serikali, lakini ukweli ni kwamba hata wao wanajua hapakuwa na utaratibu mzuri wa kuanzishwa kwa utaratibu huo nchini. Matokeo yake migomo sasa kila mahali nchini kote.


Lakini ni Serikali hii hii ambayo wakubwa walibariki malori yazidishe uzito licha ya waziri mwenye dhamana kuiweka wazi sheria, tena iliyotungwa tangu Awamu ya Kwanza. Ni wakubwa hawa hawa waliomzuia waziri mwenye dhamana kuwaondoa watu waliojenga ndani ya hifadhi ya barabara!
Ni wakubwa hawa hawa ambao walimzuia waziri mwenye dhamana kutenga eneo kule Loliondo kwa ajili ya uhifadhi. Walifanya hivyo kwa tishio la kukosa kura endapo mpango wa wizara ungetekelezwa. Tena ni wakubwa hawa hawa ambao bila haya wakawaahidi wananchi wa Ngorongoro kuwa wangewapa mahitaji ya chakula bure kwa mwaka mzima! Sasa huko kuna moto baada ya ahadi hiyo kutotekelezwa. Viongozi makini hawawezi kuwaahidi watu wazima wenye afya njema kuwapa chakula bure.


Serikali imechukua hatua za kutekeleza mambo makubwa yanayowagusa wananchi; ama bila weledi, au pale ilipoona wananchi wamekuja juu. Imekosa watu wa kusimama na kutetea hoja hata waweze kueleweka kwa wananchi. Tumekuwa na Serikali ya ku-beep na kusubiri kuona kama itapigiwa au haitapigiwa.
Ime-beep suala la madereva, imepigiwa. Ninavyoandika makala hii wala haitashangaza kuona ikinywea. Itanywea kwa sababu, ama imekurupuka, au imekosa watu wa kusimamia kutetea hoja.
Nikiyatafakari yote haya, sioni ni wapi ambako Chadema wanasababisha nchi isitawalike. Sioni wapi kuna nafasi ya chama chochote cha siasa ya kuivuruga Serikali. Mchawi wa Serikali ni Serikali yenyewe iliyokosa weledi.


Tumekuwa na Serikali inayoongozwa kwa matukio na hisia. Suala la Katiba mpya linathibitisha hiki ninachokisema. Kwa viongozi kadhaa kusaka umaarufu na kuweka alama ya kuendelea kutambuliwa ‘milele na milele’; walidiriki kuwaletea Watanzania Katiba kwa kasi ambayo haijapata kutokea mahali popote katika ulimwengu huu wa kidemokrasia.


Tangu awali Katiba ilionekana ni kitu kilichokuwa nje ya mpangilio wa kazi za Serikali. Tuliwasikia mawaziri wakisimama na kutamba hadharani kwamba hapakuwa na mpango wa kuandikwa kwa Katiba mpya. Mara tunasikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali akisema hivyo hivyo, lakini muda si mrefu kiongozi mkuu wa nchi akaibuka na kutoa kauli iliyokinzana na wasaidizi wake.


Watu wenye utashi wakasema muda wa kuandikwa, kupitishwa na hata kutumika kwa Katiba hiyo mwaka 2015 haukuwapo. Lakini kwa sababu walioko serikalini ndiyo wenye akili nyingi, wakalazimisha. Matokeo yake ni hii aibu kubwa iliyoikumba Serikali.
Serikali ya matukio haiwezi kuwa na mambo yaliyonyooka. Kwa Serikali ya matukio moja jumlisha moja si mbili! Ni moja! Serikali inayoendeshwa kwa matukio ndiyo ambayo viongozi wake utasikia leo wakisimama majukwaani kulaani mauaji ya albino kwa sababu yametokea! Huwezi kuwasikia wakiyahami.
Utaisikia Serikali ya matukio ikiishia kupeleka rambirambi kwa wafiwa wa ajali za barabarani, na baada ya siku mbili tatu hakuna hatua zozote za maana zinazochukuliwa kupunguza au kumaliza tatizo hilo.


Serikali ya matukio ndiyo inayoweza kuamka na kuanza kuwasaka waganga matapeli kwa kigezo cha ushiriki wao kwenye mauaji ya albino. Huwezi kuisikia ikilaani wananchi wake wanaopoteza fedha nyingi kwa sababu ya uongo na utapeli wa wazi wazi kama ule wa kuwa na uwezo wa kumwongeza akili mwanafunzi au kutengeneza fedha za majini!
Utaona watendaji wa Serikali dhaifu wakisoma matangazo ya matapeli, lakini licha ya matapeli hao kuweka namba zao kwenye matangazo hayo, hakuna hatua zinazochukuliwa.


Tunachokishuhudia nchini ni kwa sababu ya matokeo ya udhaifu wa Serikali uliosababisha kuibuka kwa makundi ya kila aina, yanayoweza kufanya kitu chochote bila kuhojiwa au kubughudhiwa. Vikundi vya ‘Panya Road’ ni matokeo ya udhaifu wa Serikali.   Tumefika mahali ambako vijana wanaweza kujikusanya na kufanya uhalifu mchana kweupe.


Wananchi wameona Serikali haina msaada. Wameamua kutumia sheria mkononi. Wanawakamata wahalifu na wasio wahalifu. Wanawapiga. Wanawaua. Wanafanya hivyo kwa sababu wanajua polisi hawawajibiki ipasavyo. Wanaona karaha ya kumpeleka mtuhumiwa polisi halafu hao hao walalamikaji wakatakiwa wawapelekee chakula!


Wanafanya hivyo kwa sababu wanajua mahakamani mwenye fedha ndiye mwenye haki. Njia ya mkato waliyoona inawafaa ni kumalizana na watuhumiwa huko huko mitaani. Matokeo yake wapo wanaouawa wakiwa hawana hatia. Wanaoyafanya haya si Chadema, CUF, ACT wala chama kingine, isipokuwa ni matokeo ya Serikali ya CCM.
Ukiyatafakari matukio mengi ya ajabu-ajabu yanayoendelea nchini mwetu, unafikia hitimisho la kuomba Oktoba iwadie haraka ili Serikali hii ipumzike, maana hata anayeiongoza keshasema wazi kuwa kachoka.

1785 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!