Katika makala yangu, iliyotoka wiki iliyopita nilianza kujadili kurudi kwa mataba ya elimu katika jiji la Dar es Salaam ambalo ni kioo cha taifa hili. Hii ilitokana na kuonekana mabasi kadhaa yaliyoandikwa “INDIAN SCHOOL BUS” na mengine “YEMEN SCHOOL BUS”. Tuendelee na mjadala.

 

Hapa nchini Tanganyika walikuja kuishi wahindi wa aina mbalimbali kutoka Bara Hindi. Walifika makundi makubwa matatu ya hao wahindi. Sijui kama watanzania wa leo (vijana) wanajua makundi ya hao wa Bara Hindi. Sisi wazee tunakumbuka wapo wale wanaotoka maeneo ya Gujarati kule India. Hawa kwa ujumla ni Wahindi, miongoni mwao wapo tunaowaita Wahindu, wapo wa Shia na wapo wale wa Ithna-Asheri na wa Aga Khan. Kundi la pili ni wale wa kutoka maeneo ya Punjab. Hapo tunao Wahindu, na Makalasinga. Na kundi la tatu ndiyo wale wa kutoka sehemu za kusini magharibi mwa Bara Hindi na wengi wao tuliwajua kama Magoa na wafuasi ya dini ya Kikristo. Kila kundi kati ya hao walikuwa na shule zao hapa nchini.


 Baadhi ya shule zilizokuwa za Wahindi siku za ukoloni hapa Dar es Salaam ni hizi Shaaban Robert, Tambaza, Jangwani, Kisutu, Azania, Forodhani (St. Josephs Convent sasa Millennium), Mzizima na Zanaki hizo zote zilijukana kama Indian Schools. Zote zilitaifishwa mwaka ule wa 1970 na kupata majina hayo ya sasa badala ya majina yao ya Kihindi/Kigoa.
 Leo hii ninapoona basi limeandikwa Indian School Bus au Yemen School Bus mimi najiuliza, Wizara ya Elimu inaturudisha kule miaka ya 1950? Au mtazamo wangu huo ni potofu? Hapa nahitaji kuelimishwa.


Kama kweli Wizara imeamua kurudisha matabaka katika mashule, mitaala gani inatumika katika shule hizo? Kwa vile watu binafsi na taasisi zenye fedha zina uwezo wa kuendesha shule na wanaona fahari kuwa na shule za English Medium, je, nchi ya wajamaa, raia walio sawa, inaweza kuwaelimisha watoto wao kimatabaka namna hii?


 Hapo walionacho watapata elimu tofauti na katika mazingira tofauti na wasionacho ndiyo hao wa shule za kata. Ni sawa malezi namna hiyo? Mbona tunarudia kwenye ule utaratibu wa mkoloni? Tunawaandaa watoto wa Taifa lipi hapa Tanzania? Sijui kama mtoto anayetoka kule Indian School anaweza kushirikiana vizuri na mtoto wa kutoka kule Pembamnazi au Chanika?


Moja ya shabaha za elimu ya taifa ni kuwalea na kuwakuza watoto wa Taifa hili katika maadili ya Kitanzania na kizalendo. Hii shule ya Yemen, sijui wenyewe ni watu gani! Lakini sote tunajua kuwa nchi ya Yemen haijatengemaa kisiasa. Je, walimu wanaofundisha shule hiyo tunawajua vilivyo? Isije tukawa tunalea wanaharakati wa huko Yemen? Tuna uhakika gani na uzalendo wa wanaosoma humo? Wakaguzi kutoka Wizara ya Elimu wameridhika vilivyo na mafunzo katika shule hizo?


 Mimi nafikiria makuzi ya watoto wetu katika mashule yetu yanakuza na kulenga UZALENDO. Shule zote za gharama kubwa kwa mtazamo wangu huwa na mawazo ya unafsi, ubepari na sioni namna wanavyoweza kufikiria ujamaa huku mazingira waliyokulia yana muono wa ubepari. Jina la shule linatia wasiwasi na uzalendo wake. Sipendi kufikiria dhana ya mamluki katika malezi ya watoto kwenye mazingira ya utajiri unaoelekea kuwapo katika aina hii ya shule?


Nimechimbua historia ya mfumo wa elimu enzi za ukoloni, pale wakurugenzi wa elimu walipoweza kupanga na kuratibu elimu ya watoto wa Tanganyika. Hizo shule za Wahindi na Waarabu za sasa zinaratibiwaje? Je, zipo shule nyingine kama hizi mahali pengine katika Jamhuri yetu hii?
 Kuna methali inayosema KINGA NI BORA KULIKO TIBA. Taifa linafaa kuwa na tahadhari katika uanzishaji wa shule hizi za mataifa tusije tukatengeneza vituo vya kufunza magaidi hapa nchini. Utaifishwaji wa shule za mataifa na za madhehebu za dini ulikuwa kukinga kukua kwa matabaka miongoni mwa wakazi wa Tanganyika. Sasa kuongeza shule za English Medium ni kueneza sera ya matabaka. Taifa hili litaweza kuhimili matabaka miongoni mwa Watanzania?


Mimi nimetoa dukuduku langu la moyoni juu ya kile nilichokiona. Nitashukuru sana kupata maelezo sahihi juu ya shule zenye mabasi haya. Aidha, nitafurahi kuthibitishiwa kuwa elimu itolewayo katika shule hizi siyo hatarishi. Watoto wale siyo wakuja bali ni raia safi wa nchi hii. Wala siyo watoto wa uraia wa nchi mbilii (dual citizenship). Kumbe wazalendo ni wale wote wenye kuifia nchi yao na wana uraia wa nchi moja tu. Siyo vibaya kukumbusha wenzangu kuwa TANZANIA ITAJENGWA NA WENYE MOYO NA WAZALENDO.


Naomba tena nikumbushie maneno ya Mwalimu Nyerere kule kwenye Umoja wa Mataifa kikao cha 579 cha Kamati ya Nne, tarehe 20 Desemba 1950. Narudia lalamiko lake ….in Tanganyika education in racial “in terms of separate school systems for Europeans, Asians and Africans, with different financial, teaching and other resources….. so this apparent injustice to the African, like so many others, is done for the good of the African!


Kwa maneno haya sisi Watanzania wa leo bado tunakubali kuwapo kwa shule za wenye kipato eti wawe na majengo mazuri, walimu bora, mazingira tofauti kabisa na yale ya shule za watoto wa wakulima, kwenye shule za Kata ya Mlingoti au Nalasi kule Tunduru halafu wote wafanye mtihani ule ule kuingia kidato cha kwanza. Je, ni ulinganisho halali namna hii? Mwalimu alisema tofauti hizo siyo sahihi. Mtoto asiyepitia English Medium na yule wa English Medium tukubali jamani kimazingira hawapo sawa!


  Kama hivyo basi kwa nini Serikali iendeleze kusajili shule hizi za binafsi za English Medium? Kabla ya Uhuru zilikuwa 11 tu, leo hii zipo 651! “So, this apparent injustice to peasants’ children in our country should be discouraged”. Nionavyo mimi.
Naomba matabaka katika elimu ya nchi hii yasiruhusiwe kwa kisingizo chochote kile. Wizara isikubali kusajili shule za elimu ya matabaka Tanzania. Tujenge UZALENDO miongoni mwa watoto wetu hawa, taifa la kesho.

 

Mwandishi wa Makala hii, Francis Mbenna ni Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mwenye makazi yake jijini Dar es Salaam . Anapatikana kwa simu: 0755 806 758; email: [email protected]

By Jamhuri