“Maelezo kwamba Tanzania ni nchi masikini yananikera. Imefika mahala wanasiasa wanadhani ili uwe kiongozi bora ni lazima ujiainishe kuwa unatatea masikini. Natamani tukose misaada kwa miaka mitano, tutapata akili na kutumia vyema utajiri tulionao. Hatustahili misaada kabisa maana nchi hii inao utajiri wa kutosha.”

Maneno haya ameyasema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu, akiwaambia wahariri wa vyombo vya habari mjini Morogoro kuwa mawazo ya Watanzania yanapaswa kufikiria kufanya kazi zaidi badala ya kutegeshea misaada.

Askofu Tutu: Wamisionari walitupora

“Wamisionari walipokuja Afrika walikuwa na Biblia na sisi tulikuwa na ardhi yetu. Wakatwambia ‘Tuombe’. Tukafumba macho yetu. Tulipofumbua macho tukajikuta tuna Biblia na wao wana ardhi.”

Haya ni maneno ya mshindi wa Zawadi ya Nobel, Askofu Mkuu Desmond Tutu wa Afrika Kusini, wakati akieleza hila za Wazungu walivyoitawala Afrika kwa mbinu mbalimbali.

Idi Amin: Watu lazima wafe

“Katika nchi yoyote duniani kunapaswa kuwapo watu wa kufa. Ni sadaka inayopaswa kutolewa na taifa lolote katika kuhakikisha sheria inaheshimika.”

Haya ni maneno ya aliyekuwa Rais wa Uganda, Idi Amin Dada aliyeng’olewa madarakani na majeshi ya Tanzania mwaka 1979. Aliamini kuwa hakuna nchi inayoweza kuendelea bila kuua watu wasiotii sheria na dola.

 

By Jamhuri