Siasa ni itikadi inayofuatwa na kundi au jamii fulani ambayo ni msingi wa kuendesha uchumi, utamaduni na mwenendo mzima wa maisha ya jamii hiyo. Aidha, ni mbinu ya utekelezaji au uendeshaji wa jambo kwa kutumia busara na hekima ili kufikia lengo linalotarajiwa.

Watu wanaopenda kuratibu na kuongoza shughuli za siasa hujichomoza mbele ya jamii na kuitwa wanasiasa. Ukweli watu hawa huwa na dhamira ya kushika nchi (dola) na kuhubiri aina ya itikadi wadhaniayo itastawisha uchumi na utamaduni wa jamii kuwa bora zaidi kila uchao.

Kuwa mwanasiasa si kazi rahisi kama baadhi ya watu wanavyodhani au kufikiri. Siasa ni kazi pevu na nzito ambayo daima huhitaji busara na hekima katika kila kauli na kitendo. Kauli au kitendo cha mwanasiasa huwa ni mvuto kwa mtu yeyote kufuata.

Kutaka kuwa kiongozi wa siasa huna hudi ubebe dhana mbili kichwani na kifuani, nazo ni busara na hekima. Dhana hizo zinalindwa na kauli safi na ya ukweli, vitendo bora na nadhifu (uadilifu) ushupavu na msimamo katika kukinga kile usemacho na utendacho bila kuvunja taratibu zilizowekwa na kukubalika na jamii husika.

Kila nchi duniani ina aina ya siasa (itikadi) ambayo ikifuatwa itawawezesha kuendesha mambo yao kiuchumi na kitamaduni. Na hapo nchi huweka malengo na dira ya taifa lao. Wanasiasa wa kila itikadi hupambana majukwaani kuhubiri malengo na misimamo yao, ni yupi atashinda.

Nchi yetu Tanzania ina vyama vingi vya siasa (vipatavyo 17) na kila kimoja hujieleza itikadi yake na kuahidi pindi kipatapo ridhaa ya wananchi ya kushika madaraka ya nchi, kitatekeleza malengo na dira yake ambayo itaweza kuinua na kuboresha hali ya maisha ya Watanzania.

Hivi sasa vyama 16 kila siku vinajisifu na kujigamba vina uwezo zaidi ya chama kilichoko madarakani – CCM. Vyama hivyo vinadai CCM haina jambo jipya. Imeshindwa kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Ushahidi wao ni uleaji wa rushwa, ufisadi na wananchi ni masikini.

Chama Cha Mapinduzi kinapinga maelezo hayo. Kinajigamba (ASP na TANU) kimewakomboa Watanzania kutoka kwenye unyonge na utumwa. Kinastawisha na kuendeleza maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Bado kuna vidosari vidogovidogo vinavyoshughulikiwa na vitaisha.

Sina nia ya kulezea kazi zinazofanywa na maendeleo yanayopatikana katika vyama vya sasa. Nia ni kuchangia fikira jinsi gani baadhi ya Watanzania wenzetu wanaopenda na kutaka kuwa wanasiasa ilhali hawana sifa, elimu na mbinu za kisiasa. 

Siasa ni sayansi ni utamaduni. Watu wa taaluma hii hutakiwa kuwa wajuzi wa mambo, wakweli na si wabinafsi. Kuwa mwanasiasa si kuchomoka kimaslahi na kiubwana. Ni kukubali kuwa mtumishi, mkweli na mtiifu kwa umma. Kinyume cha hayo si mwanasiasa bali ni mbabaishaji wa siasa. Ni mtu hatari.

Ndani ya vyama/chama cha siasa kuna mizungu yake ambayo mwanachama au kiongozi wa chama hana budi kufuata na kutii kwa dhati kama vile imani, ahadi na madhumuni ya mwanachama na chama. Chama cha siasa maana yake ni watu. Watu wanaokubaliana kuondoa kero za wananchi.

Ndani ya mizungu hiyo kuna mambo ambayo baadhi yanakubalika na baadhi hayakubaliki. Yako yanayotolewa nje na yako yasiyotolewa nje kirahisi. Mambo hayo yanafanana na nafaka ya mpunga. Mpunga una mizungu yake kuanzia upandaji, upaliliaji, uhemeaji, uvunaji, usombaji hadi uhifadhiji wake.

Mpunga unapotaka kuupata mchele wake lazima uutwange. Kamwe usitarajie kupata mchele bila ya chuya na chenga baada ya kutoa pumba. Vyama vyetu vya siasa vinafanana na mpunga. Iwe CCM, CUF, ACT-Wazalendo, TLP, Chadema na kadhalika  vina mchele, chuya na chenga. Kwa vipi?

 

>>ITAENDELEA 

By Jamhuri