Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Usalama wa Taifa, Dk. Hassy Kitine, ameshindwa kumtaja waziri anayedai kwamba amechota fedha katika mataifa kadhaa kwa ajili ya kujenga hoteli na kujiandaa kugombea urais mwaka 2015.

Dk. Kitine alipokuwa akihojiwa katika Kituo cha Televisheni cha Channel 10 cha jijini Dar es Salaam hivi karibuni, alidai kwamba waziri huyo ana kiasi kikubwa cha fedha.

Ingawa hakumtaja kwa jina, maelezo ya Dk. Kitine aliyewahi kuwa Mbunge wa Makete, yalionyesha kuwa mlengwa alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Kitine na Membe wapo kwenye msuguano wa muda mrefu. Membe aliwahi kumbana Dk. Kitine kuhusu udanganyifu alioufanya kwa matibabu ya mkewe kwa kutumia fedha za umma.

Membe alimtumia salamu Dk. Kitine akimtaka amtaje kwa jina au hata kwa ishara tu ya ‘kutikisa kichwa’ kwamba ndiye waziri anayetuhumiwa kukusanya fedha hizo kutoka ughaibuni.

Membe akasema kama Dk. Kitine angethubutu kumtaja kwa kumsingizia, basi Watanzania wajiandae kupata mengi na mazito yanayomhusu Dk. Kitine. Pengine ni kwa hofu hiyo ndiyo maana Dk. Kitine amekataa kumtaja.

Akizungumza na JAMHURI, Dk. Kitine amesema hana maelezo mengine zaidi ya yale aliyoyatoa kupitia televisheni. Hata alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi kama yupo tayari kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama kwa kumtaja na kumfanyia uchunguzi waziri aliyemtuhumu, Dk. Kitine alisema hatakuwa tayari kutoa ushirikiano wa aina hiyo.

“Mimi nilitimiza wajibu wangu wa kumsema huyo waziri, sasa kama kuna jambo la kumchunguza, basi hilo liwe la vyombo vya usalama. Waulizwe usalama, siwezi kuwapa ushirikiano kwa kazi ambayo ni yao. Siwezi kuingilia mambo ya uchunguzi. Sijamsema mtu, hakuna wa kunishitaki, hakuna jina nililolitaja,” amesema.

Dk. Kitine aliendelea kulalama kwa kusema, “Membe ni ofisa wangu, ananitukana. Lakini sijamsema mtu. Ananionea, kanitukana kweli kweli. Kasema mimi ni mchonganishi. Mimi nina heshima, sikumsema yeye, why ajihisi?

“Kama ni mawaziri, wapo wengi wanaosafiri. Sina malumbano naye (Membe)… sina comments zaidi. Pamoja na kusema, mambo ya nchi siwezi kunyamaza.”

Akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita, Membe alimfananisha Dk. Kitine na mganga wa kienyeji mchonganishi maarufu kwa jina la ‘Kingwendu’. Alisema Kingwendu alikuwa na tabia ya uchonganishi na kusababisha maafa katika jamii. Alimtaka Dk. Kitine aulizwe amtaje waziri aliyemtuhumu.

Membe alisema kama Dk. Kitine atathubutu kumtaja kwa tuhuma hizo alizoziita kuwa ni za ‘uongo’, basi Watanzania wajiandae kupata ‘Membe, Kitine Part II’.

Kwa upande wake, Membe ameulizwa na JAMHURI kama bado anataka kuendelea na mapambano hayo, naye akajibu:

“Mmekosa uhondo, mimi naomba anitaje halafu mpate mambo. Ni hatari kubwa katika taifa kuwa na watu wazushi. Hawa wanaweza kuliingiza taifa katika migogoro kwa sababu kama mzee wa makamo anaweza kuibua uongo tu wa kusema kuna waziri amepewa fedha – wakati ni uongo – anaweza kuibua chuki kuanzia kwenye familia hadi taifa.

“Ninyi waandishi mnapoelezwa mambo ya uongo kama haya lazima muwabane hao wanaoyasema wayathibitishe na wasipoyathibitisha muwapuuze.”

Membe anakumbukwa kwa kusimama bungeni na kutoa siri nzito za matibabu ya mkewe Dk. Kitine, huku akibainisha kuwa kiongozi huyo alikuwa akidanganya na hivyo akajipatia fedha za umma.

Dk. Kitine alilazimika kujiuzulu uwaziri (Utawala Bora) na akatakiwa arejeshe fedha za Serikali alizozichukua kwa kusingizia matibabu ya mkewe.

 

1489 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!