MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekamilisha mpango wa kuwapatia Watanzania anwani za makazi.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma, aliwambia wahariri mwishoni mwa wiki kuwa taasisi yake imefanya utafiti nchi nzima na kuipa mikoa yote, wilaya na kata anwani za makazi (postal code).

Alisema kilichosalia sasa ni kushirikiana na mamlaka mbalimbali kuanza kuandika anwani hizo, baada ya kuwa umetekelezwa mradi wa majaribio katika mikoa ya Arusha na Dodoma kwa ufanisi mkubwa.

Anwani hizi hutumika katika nchi zilizoendelea ambapo anwani inamtambulisha mtu mkoa anaotokea, wilaya, kata na nambari ya nyumba anayoishi, hali inayorahisisha kufahamiana na kufahamika anakoishi mtu.

Profesa Nkoma alisema Tanzania imegawanywa kwenye kanda samba, ambazo kila mkoa utakuwa na namba ya utambulisho. Mfumo huu utatumika pia watu kupokea barua zao na vifurushi badala ya kutumia sanduku la posta.

“Namba 1 ni kwa ajili ya Dar es Salaam. Namba 2 ni kwa ajili ya mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Namba 3 ni kwa ajili ya mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera na Shinyanga. Namba 4 ni kwa ajili ya mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora na Kigoma.

“Namba 5 ni kwa ajili ya mikoa ya Iringa, Mbeya, Rukwa na Ruvuma. Namba 6 ni Pwani, Mtwara, Lindi na Morogoro na namba 7 ni Zanzibar kwa mikoa ya Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Mjini Magharibi, Kusini Pemba na Kaskazini Pemba,” alisema Profesa Nkoma.

Alisema anwani za makazi zitakuwa kwa utaratibu wa kila nyumba kuwekewa namba ambapo namba shufa zitakaa upande wa kulia na namba witiri zitakaa mkono wa kushoto mtu anapoingia kwenye mtaa wowote nchini.

Anwani hizi za makazi zinatumika nchi zilizoendelea duniani zimesaidia kupunguza uhalifu kwa kurahisisha utambuzi wa nani anaishi wapi na anafanya nini, hali inayoweza kushusha hata riba za benki kwa kuwatabua Watanzania wako wapi na wanafanya nini.

2481 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!