Maimu
Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dickson Maimu
Vitambulisho vya taifa ni kitu muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya taifa letu. Kukamilishwa kwa mchakato wa vitambulisho vya taifa kwa Watanzania na wageni mbalimbali hapa nchini, ni juhudi na mafanikio makubwa ya Serikali na watumishi waliojitoa kwa nguvu na maarifa yao yote kufanikisha azma hii.

Ikumbukwe kuwa suala la vitambulisho limeanza kushughulikiwa miaka michache baada ya Uhuru, lakini limewezekana baada ya miaka 50. Hii ni hatua ya kujivunia.
Vitambulisho vya taifa vina faida kubwa sana. Vitambulisho hivyo ni zaidi ya vitambulisho hivi vya kupigia kura! Vinaiwezesha Serikali na taasisi zake kuwa na maelezo ya kila raia na watu wengine wanaoishi katika taifa letu.

Vitasaidia kuwa na idadi halisi ya watu wanaostahili kulipa kodi. Vitasaidia kupunguza udanganyifu shuleni, kazini, katika taasisi za fedha na kwenye nyanja nyingine nyingi.

Kwa kushirikiana na mamlaka nyingine, vitambulisho vya taifa vitasaidia kuwa na idadi halisi ya wapigakura, vitasaidia pia wananchi kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha na kadhalika.

Pamoja na maudhui haya mazuri, kumejitokeza kundi la watu wachache wanaotaka kuchafua hali ya hewa. Hawa ni wale wanaowahadaa wananchi wakisema kuwa vitapatikana kwa malipo. Wezi wameanza kuwahadaa wananchi. Hili tunawaomba wananchi walipuuze.

Vitambulisho vya taifa vinatolewa bure kwa Watanzania wote na wale wasio Watanzania. Hao ni pamoja na wakimbizi na wafanyakazi mbalimbali.

Fomu hadi kupata kitambulisho ni bure. Sana sana mwananchi ataingia gharama ya kupeleka vyeti vya kuthibitisha masuala fulani fulani kama vile kubadili jina, ndoa na kadhalika.

Sifa kuu ya kupata kitambulisho ni kuwa Mtanzania au mkazi wa Tanzania. Waliosoma na wale ambao hawakuwahi kuwapo darasani, wote watapata vitambulisho bure. Kuna watu sasa wanawahadaa wenzao kuwa kama mtu hakusoma shule, hawezi kupata kitambulisho. Huo ni uongo wa hali ya juu, na wananchi hawana budi kuupuuza. Vitambulisho ni kwa watu wote – masikini na matajiri.

Tunachukua fursa hii kuwataka Watanzania waunge mkono watendaji na wafanyakazi wote wa NIDA kwa kufanikisha mchakato huu muhimu.

Tunatambua kuwa vita ya vitambulisho ilianza muda mrefu, na wale waliokosa zabuni hawajakata tamaa ya kuendelea na mapambano ingawa hayana tija. Ndiyo maana sasa kunazuka mambo mengi tunayodhani hayana msingi wala ustawi wowote kwa maendeleo ya Watanzania.

Suala la kuwapo polisi na wanajeshi ambao majina yao yameonekana kufanana kwa kila hali, si la kificho na wala kuzungumzwa kwake hakuwezi kuleta machafuko.

Ikumbukwe kuwa moja ya kazi kubwa na muhimu sana ya vitambulisho hivi, ni kupata na kuhifadhi maelezo sahihi ya kila mtu mwenye sifa ya kupata kitambulisho. Ndiyo maana tunasema vitambulisho hivi ni ukombozi kwa sababu vitaondoa kabisa hii tabia ya kughushi au kupeana vitambulisho vya elimu kwa njia za udanganyifu.

Lazima tuwe taifa la watu wakweli, na kwa dunia ya leo maisha ya mkato au ya ujanjaujanja hayana nafasi tena katika dunia hii. Tusiwakatishe tamaa wala kuwatisha watumishi wa NIDA kwa kuibua tatizo hili la watu kudanganya.

 

1281 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!