Nimesoma makala katika gazeti moja litolewalo kila siku, yenye kichwa cha habari, “NIDA imemdhalilisha Rais, majeshi iombe radhi”. Katika makala hayo, mwandishi amejitahidi kuueleza umma kile anachoamini ni ukweli, wa taarifa zilizotolewa katika vyombo vya habari nchini na baadaye kuja kufafanuliwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kuhusu sakata la vyeti 948 vya majeshi yetu kuwa feki (kughushi).

Baada ya kusoma makala hayo kwa makini na kulinganisha na kile nilichokuwa nikifuatilia kwenye vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya NIDA, nasikitika kwamba kama huu ndiyo uhuru wa kutoa mawazo, basi tuna kazi kubwa huko tuendako kutokana na uandishi wenyewe kuongozwa na chuki, hasira, jazba na kumlenga mtu badala ya NIDA kama Taasisi.

Najiuliza Tanzania yetu, yako wapi maadili ya uandishi wa habari na utoaji mawazo? Kilichofanywa na mwandishi huyo ni kupandikiza chuki, husuda na hasira isiyokuwa ya lazima kwa wananchi, viongozi wakuu wa kitaifa na wa majeshi. Huu ni uchochezi.

Nilichojifunza kama Mtanzania ninayependa haki ni kwamba NIDA walikuwa na kila sababu ya kutoa ufafanuzi baada ya kuelewa majukumu yao. Ni ukweli usiopingika kuwa kazi ya NIDA si kuhakiki vyeti wala viambatanisho vya mwombaji wa kitambulisho, isipokuwa ni kutengeneza mfumo wenye taarifa sahihi na kamili.

Lakini ni changamoto kwa taasisi zenye majukumu ya kuhakiki taarifa, kushirikiana kwa karibu na NIDA kuhakikisha kuwa nchi yetu inakuwa na mfumo mzuri wenye taarifa sahihi za watu wake.

Nitajaribu kuchambua baadhi ya hoja zilizoainishwa katika makala hayo. Nafanya hivyo si kwa lengo la kutetea upande wowote, kwani sifungamani na upande wowote, lakini kujaribu kupanua uelewa wa mambo ili Mtanzania wa kawaida apate fursa nzuri ya kupembua pumba na mchele.

Kwa bahati nzuri nimeishi ughaibuni ambako kitambulisho cha taifa ndiyo msingi wa kila jambo – kisiasa, kiuchumi na kijamii – mfumo ambao hapa kwetu umechelewa sana na umetuathiri kupata maendeleo ya haraka, ikilinganishwa na nchi ambazo wamekuwa na mfumo kama huu kwa muda mrefu.

Kwa Tanzania, falsafa ya kitambulisho ni ngeni, lakini manufaa yake ni makubwa kwa nchi yoyote inayotaka maendeleo ya haraka. Hakuna asiyechoshwa na vitendo vya ujangili, umiliki ardhi holela wa wageni, uingiaji holela wa wageni nchini kwetu bila kuwapo udhibiti na kadhalika. Kwa ufupi tumekosa namna au mfumo wa kututambulisha na sisi kutambuana.

Kwa kuelewa maana na umuhimu wake, ndiyo maana nimekuwa mdau mkubwa na mfuatiliaji wa karibu wa mwenendo mzima wa upatikanaji wa vitambulisho vya taifa.

Hapa naomba niwaambie Watanzania kuwa yanayotokea sasa ni sehemu tu ya changamoto, lakini bado zitajitokeza changamoto nyingi ambazo kama hatutaelewana na kuzungumza lugha moja, basi manufaa ambayo nchi za wenzetu wameyapata kwa kuwa na kitambulisho cha taifa, basi hapa kwetu itakuwa ni ndoto, simulizi isiyokwisha na hadithi.

Watanzania lazima kuelewa kuwa hakuna jinsi ya kukwepa ukweli kwamba NIDA lazima iwezeshwe, iaminiwe na iungwe mkono kufanya kazi yake. Kusema kuwa NIDA inafanya kazi za wengine hakuna mantiki, ni sawa na mtu kucheza ngoma asiyoijua, kwa kuwa jukumu kubwa walilonalo NIDA ni kutengeneza mfumo unaoaminika, utakaosadia utendali wa taasisi nyingine na wenye taarifa za msingi – si tu kitaifa bali kimataifa.

Sidhani kama wakwepa kodi, maharamia, watu wanaojifanya kuwa Watanzania na hali tunawajua kuwa si Watanzania wataupenda mradi huu au kuunga mkono. Hili Watanzania lazima walifahamu. Kama tuna adui, basi kwa sasa adui yetu wa kwanza ni yule anayepinga mradi huu. Ndiyo maana sikushangazwa na mwandishi wa makala hayo, kwani nimepata shaka juu ya uraia wake na uzalendo alionao kwa Taifa hili.

Nasikitika kama nchi yetu itakubali kutumika kama kichaka cha mwendawazimu kwa kukubali mtu mmoja kuwalisha sumu mamilioni ya Watanzania kutokana na chuki binafsi. Hivi watawala, watumishi wa serikali vikiwamo vyombo vya usalama vilivyotajwa katika makala hayo naomba wajibu! Nani tajiri yenu; Serikali au wananchi?

Ni masikitiko makubwa kama leo tunaona thamani ya nchi hii iko kwa watawala, na si kwa wananchi na fedha zao za kudunduliza zinatufanya leo kutoka kifua mbele na vyeo vyetu. Tumefika wakati na kusahau kuwa wananchi wana haki ya msingi, tena ya kwanza ya kujua kila hatua inayoendelea nchini kwao kabla hata ya huyo aliyekuajiri.

Sioni mantiki ya kumlaumu Mkurugenzi wa Vitambulisho vya Taifa kwa hatua yake ya kuamua kuzungumza na umma. Ametambua thamani ya fedha ya walipakodi na kuthamini mchango wa wananchi, bila kuonyesha dharau kwa wakuu wake wa kazi.

Kwangu sioni kosa lake kwa kitendo chake cha kiungwana kuzungumza na umma, kwani mradi wa vitambulisho vya taifa ni wa wananchi.

Hoja kubwa iliyozua mjadala kwa takribani wiki mbili sasa ni hoja ya kughushi vyeti. Nimejaribu kujipa tafakari ya kina na muda mrefu tuliopoteza kulumbana kuhusu jambo dogo ambalo ukweli wake uko dhahiri licha ya juhudi za NIDA kujibu.

Pamoja na taarifa ya ufafanuzi kutoka kwa Mkurugenzi wa NIDA aliyotoa kwa vyombo vya habari akifafanua taarifa za vyeti 948 vya polisi na wanajeshi, bado mijadala na malumbano ya hapa na pale imeendelea wengine wakiamini kuwa ni vitisho ambavyo NIDA wamepewa na mamlaka ya juu.

Siamini juu ya hilo, ila ukweli utabaki kuwa NIDA si jukumu lao kuhakiki vyeti na hawana utaalamu wa kuhakiki vyeti kubaini hiki ni cha kughushi na hiki ni halali. Lakini wana haki ya kusema kuna majina yanayofanana ili mamlaka husika zipate ukweli.

Kama NIDA wasipobaini upungufu huu tutarajie daftari gani la kumbukumbu litakalotengenezwa? Na aina gani ya kitambulisho watapewa Watanzania? Je, ingesikika leo idadi hiyo ya watumishi wa jeshi imepewa vitambulisho bila kujali upungufu uliojitokeza, hilo lingekuwa sahihi?

Je, nani anapima ubora wa kazi ya NIDA katika kutengeneza mfumo wa utambuzi na usajili wa watu na hatimaye kuwapatia vitambulisho?

Mwandishi anataka kuendeleza utamaduni wa usiri hata katika mazingira yasiyohitaji usiri. Hizi ni zama za uwazi na ukweli. Sijaona popote panapohusisha taarifa hizo na usalama wa nchi. Tusipotoshe ukweli wala tusiwapotoshe Watanzania.

Wanajeshi wamenyamaza. Polisi wamenyamaza. Hawa wanaowashwa wana mpango gani? Je, wanataka wapewe NIDA ili waitafune? Naomba wananchi tutambue umuhimu wa NIDA na wajibu wao wa kuwezesha upatikanaji vitambulisho. Wasikatishwe tamaa.

Mwandishi wa makala haya amejitambulisha kuwa ni msomaji wa JAMHURI anayeishi mkoani Mwanza.

By Jamhuri