Zitto
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, mwishoni mwa wiki amefanya mahojiano maalum na Gazeti la JAMHURI kuhusiana na mwenendo wa Bunge na mwelekeo wa taifa hili kwa ujumla. Mwandishi Wetu DEODATUS BALILE anakuletea mahojiano hayo kama ifuatavyo:

Swali: Umekuwa mbunge kwa vipindi viwili sasa. Ni mambo gani makubwa umelitendea taifa hili na yanabaki kuwa kumbukumbu ya milele kama mtumishi wa umma?

Jibu: Buzwagi. Nimeingia bungeni nilikuwa siijui sekta ya madini, ila nilikuwa nikilifahamu kama eneo la uchumi mpana. Nilijiwekea vipaumbele – moja ikiwa ni kusimamia Sheria ya Maadili ya Viongozi. Hiki ndiyo kilichokuwa kipaumbele changu wakati nakwenda bungeni.

Baada ya kupata nyaraka mbalimbali za Serikali kama mbunge, nikawa najiuliza kwa nini sekta ya madini haichangii kiasi cha kutosha katika uchumi wa taifa hili? Januari 2006 au by [kufikia] 2007 nikawa knowledgeable (nikawa na ufahamu). Nikauliza ule mkataba wa Buzwagi. Waziri wa Madini Ibrahim Msabaha akatangaza bungine kuwa hakuna mkataba mpya utakaosainiwa, baadaye kwa siri ukasainiwa Mkataba wa Buzwagi tarehe 17 Februari, 2007 kinyume na maagizo ya Rais na Waziri.

Nikaona hili haliwezekani. Nikatoa ile hoja ya kutaka waliohusika wawajibishwe na kwa hoja ile nikasimamishwa ubunge. Hii iliwauma watu wengi, na nikazunguka karibu nchi nzima kuwaeleza ukweli. Baada ya ziara Rais akaniteua kwenye Kamati ya Jaji Bomani, baadhi ya watu wakasema ohoo! nisikubali uteuzi huo kwani umeletwa kama rushwa, mimi moyoni nikasema hapana. Kususa ni kuwakosesha Watanzania fursa ya kufahamu ukweli. Nikaona bora niwemo kwenye hiyo kamati ili nipate fursa ya kupata nyaraka na kuchunguza kwa kina tatizo liko wapi. Na kweli kazi hii tuliifanya kwa uzalendo wa hali ya juu, ambayo baadaye ikazaa sheria mpya ya madini.

Sheria hii imezaa vitu vikubwa vitatu; Kwanza kuwekwa kwa mujibu wa sheria kwamba ni lazima sasa uchimbaji wote wa vito uwe ni wa Watanzania wenyewe, isipokuwa tu pale Mtanzania atakapokosa mtaji wa kutosha ndipo anapoweza kuingia ubia na wageni, ila lazima abaki na asilimai 50. Hapa Watanzania wamepewa fursa ya kuchimba tanzanite na almasi kule Williamson Diamond. Kwa bahati mbaya kuna watu wanataka kutumia sheria hii Tanzanite One wasipewe kabisa mgodi ili wao wagawane vitalu. Mimi nasema tuanzishe shirika la umma au kazi hii ikabidhiwe kwa STAMICO iwekwe kisheria kuwa asilimia 50 zitakuwa za Serikali na nyingine mwekezaji.

Jambo la pili sheria hii mpya imeweka mazingira ambayo Serikali itakuwa na hisa kwenye migodi yote nchini. Jambo la tatu, sheria imebadilisha mfumo wa kukokotoa mrabaha kwa migodi yote. Watu wanaweza wakaliona ni jambo dogo, lakini ikumbukwe zamani mwekezaji ilikuwa anaondoa gharama zote alizotumia katika uchimbaji, kisha kiasi kinachobaki ndicho tunachogawiwa mrabaha wa asilimia tatu, lakini sasa unalipwa kwa kulingana na pato lote. Tunaangalia tani moja umeuza umepata fedha kiasi gani, tunachukua mrabaha kutoka kwenye pato lote ililoingiza kampuni.

Mimi niliwaambia hawa watu walioko Serikalini kwamba sisi ni dola. Hawa wawekezaji hawawezi kutuchezea nasi tukanyamaza. Tumebadili na sasa wanalipa asilimia nne. Mwaka jana kwa mauzo ya dhahabu ya mwaka jana yalikuwa yanaongezeka kutoka Sh bilioni 99 hadi bilioni 203. Watu wanasema mbona mabadiliko ya one percent ni ndogo sana. Kwa kubadili kanuni ya ukokotoaji, tunajikuta sasa tunapata kwa mfano asilimia nne ya milioni 10, badala ya asilimia nne ya milioni saba. Maana zamani walikuwa wanaingiza hata gharama ambazo hawakutumia. Sisi tunasema ingiza hizo gharama hazituhusu, mwisho wa siku tunakutoza mrabaha kulingana na pato uliloingiza. Basi.

Najua utauliza swali hili; watu wanasema baada ya Buzwagi mbona Zitto yuko kimya amehongwa? Haya nayasikia na nabaki kusikitika tu. Katika ile Kamati ya Jaji Bomani nilikuwa na (Dk. Harrison) Mwakyembe na Jaji Bomani, lakini wao hawaambiwi wamehongwa. Najua baada ya kuona matokeo mazuri ya kazi niliyoifanya, wengine hawakufurahi. Njia pekee wanayoona inafaa ni kunipuuza nionekane sina maana mbele ya jamii, lakini leo kila mtu kwa sasa anarejea taarifa ya Bomani. Nasema sekeseke lililoanzia bungeni, ambalo nililianzisha mimi limezaa sheria mpya ya madini. Hili linanipa faraja sana na kila Mtanzania anayetaka kukumbuka hawezi kuzungumza sheria mpya ya madini ambayo nchi nyingi zinakuja hapa kwetu kujifunza tulifanyaje bila kunitaja mimi kama Zitto. Nasema kwa hili nimelitumikia vyema taifa langu, na namshukuru Mungu kwa kunipa fursa hii.

Swali: Katika Bunge la Aprili ulitoa hoja ya kupata saini 70 za wabunge kwa lengo la kumwondoa madarakani Waziri Mkuu Mizengo Pinda. Hoja hii imezaa mabadiliko ya baraza la mawaziri. Je, unadhani kilichofanyika kimetosheleza ulichokitaka bungeni?

Jibu:
Baadhi ya watu wanasema mabadiliko haya ni cosmetic changes (danganya toto). Wanasema ni mvinyo ule ule katika chupa mpya, lakini hakuna siku ambayo Watanzania wamewahi kufurahia. Kitu cha msingi ni kwamba Rais amefanya mabadiliko kwa shinikizo la Bunge. Hakuna tena Waziri ambaye atadharau ripoti ya CAG. Katika ngazi ya kuwajibika Bunge mara zote limekuwa rubber stamp (muhuri), lakini katika hili tulishikamana vilivyo na tumeiwajibisha Serikali. Kuna wabunge waliosaini na ambao hawakusaini, but through their own way (kwa njia zao) walitufikishia ujumbe kuwa tuko pamoja lakini tunafahamu chama chao kilivyo hawawezi kujitokeza wazi. Mimi nasema hili ni suala la kihistoria katika nchi hii.

[Edward] Lowassa alichukua political responsibility (uwajibikaji wa kisiasa) hapakuwa na kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu. Zamu hii, party caucus (kamati) ya CCM imekutana kumwambia Waziri Mkuu hawana imani naye, hili ni jambo kubwa na la kihistoria. Yote hii imetokana na moto niliouwasha bungeni. Waziri wa Utalii; Nishati na Madini ni key ministers (mawaziri muhimu). Kimsingi Rais amewafukuza baada ya Waziri Mkuu kuwa amewaambia wajiuzulu wakakataa. Mimi nafurahi kwa sababu naanza kuona ule mfumo wa kuwajibishana unashika kasi. Bunge linaondoka kwenye siasa za maneno linakuwa la matendo zaidi.

Hii ndiyo tofauti yangu na wanasiasa wengine. Ningeweza kwenda kwenye mikutano ya hadhara nikapiga kelele kuwa ripoti ya CAG imebaini wizi, lakini nikasema hapana. Mahala mwafaka pa kufikishia kilio changu na kikafanyiwa kazi ni bungeni. Mbinu niliyoitumia ilikuwa ni jaribio kubwa kwa Rais. Alipaswa kupima, iwapo anawabakiza mawaziri tunamwondoa Waziri Mkuu Juni au awafukuze kwa kuwawajibisha, na ndicho alichofanya.

Tumefanikiwa kukusanya saini 75 za wabunge. Kwa mara ya kwanza nimefanikiwa kuunganisha vyama vya upinzani. Chadema na CUF kwa pamoja tumefanya kazi tukiwa kitu kimoja. Mimi najisikia vyema kwamba nimeweza kuunganisha kambi yote ya upinzani kuwa kitu kimoja. Tunaweza kuwa tofauti sisi Chadema peke yetu hatuwezi, tunawaghitaji CUF… tulipata saini ya Mjumbe wa NEC ya CCM [Nimrod] Mkono, mjumbe wa NEC ni mtu mkubwa sana. Niliyemshangaa ni mtu kama Christopher ole Sendeka. Huyu bwana anajifanya ni mpambanaji, lakini lilipofika la kumgusa Waziri Mkuu, akageuka wapigakura. Alikuwa anatupinga waziwazi na kwenye vikao vya CCM alisimama kuwatetea mawaziri akidai wanaonewa hawakutenda wao, akazomewa.

Ndani ya CCM wapo wabunge vijana kama Deo Filikunjombe, [Kangi Alphaxad Ndege] Lugola, Mzee Mkono, wote hawa waliunga mkono katika motion (hoja) ya kumuondoa Waziri Mkuu, isipokuwa UDP Mzee Cheyo aliniambia kwamba atasaini baadaye kwa kuwa amesafiri.

Swali: Kabla ya kutoa hoja hii ulishauriana na nani?

Jibu: Sikushauriwa na mtu yeyote. Nilisimama na kusema lazima tufanye kitu extraordinary (cha ziada), ambacho kitalifanya Bunge lifanye kazi yake. Nilipotoa hoja hiyo, nchi nzima wakaunga mkono. Nilichofanya tulichukua namba za simu za wabunge wote tukaziweka kwenye facebook. Wabunge walianza kupata pressure za wananchi wao wakiwahoji kwa nini hawajasaini au wanasaini saa ngapi. Walikuwa wanapigiwa simu kila kona. Wengine walikuwa wanakuja kusema chama chetu kinafahamika, lakini nasisitiza kumpata mjumbe wa NEC wa CCM ilikuwa muhimu mno. Kubwa zaidi ni hali tuliyopata ya vyama vyote kuungana.

Hili ni lesson (somo) kubwa sana kwamba kama Bunge tunayo meno na tunaweza kufanya jambo kubwa. Wapo watu wanaobeza kuwa tatizo ni mfumo na si watu, huwezi kubadili mfumo bila kuweka watu wa kubadili mfumo. Huwezi kutenganisha mfumo na watu. Ni neno jepesi sana kulisema watu wakaona ni mfumo.

Kwa mfano sisi Chadema tukiingia madarakani, civil service (utumishi wa umma) ni ile ile jeshi la polisi, jeshi la wananchi… Mfumo ni wa dola ya nchi. Chadema haitaenda na polisi wake – ma-RPC ni wale wale, isipokuwa tutawafukuza na kuwahamisha tukiweka wale tunaoona kuwa wanaweza kuchapa kazi zaidi. You can’t separate (huwezi kutenganisha) watu na mfumo.

Swali: Bunge limeipata wapi nguvu hii na ilikuwa imepotelea wapi?

Jibu: Kuna kipindi Bunge linakuwa kama Kamati ya Chama. Katika Bunge la 10 kuna mambo yanayoonekana kuwa Bunge linachukua nafasi yake. Suala la umeme, mgogoro wa mafuta, wabunge wote waligeuka na kuungana wakawa kitu kimoja. Hii inaonyesha kwamba tunaanza kukua kidemokrasia katika mfumo wa vyama vingi. Labda kwa sababu Bunge la 10 lina vijana wengi na ndani ya CCM vijana hawataki kuona kuwa wao wanakuwa ‘ndiyo mzee’, ikilinganishwa na wenzao wa Chadema.

Bunge la tisa tungetoa hoja kama hii, tusingepata saini 70. Bunge lile lilikuwa linafanya strengthening ya individuals (linajenga watu), si taasisi. Haijawahi kutokea katika nchi hii. The next one (zamu nyingine) itakwenda mbali. Tumevunja ule mwiko. Katika hili ni wabunge wenyewe walioamua kushikamana, vyombo vya habari vikasaidia mno, pressure ikaongezeka zaidi na viongozi wakaona hali inazidi kuwa mbaya. Uhuru wa vyombo vya habari umelisaidia Bunge kufanya kazi nzuri zaidi.

Swali: Baada ya hatua hii nini sasa mwelekeo wa Bunge?

Jibu: Mimi nawaonea huruma sana na mawaziri. Bunge will never be the same, psychological prison (halitakuwa kama zamani tena, ufungwa wa kisaikolojia) imeondoka. Si wabunge wote wa upinzani wana uwezo sawa, lakini hata wabunge wa CCM woga umewaondoka sasa. Kwa upande wa CCM tunao wengi, wakati January [Makamba] anaingia bungeni watu walijua ni mtoto wa Makamba, [Peter] Serukamba umeona kwenye Kamati ya Miundombinu?

Mawaziri wana very short honeymoon (muda mfupi wa kustarehe). Wabunge watawatesti (watawajaribu). Katika hatua hii ndipo nasema wabunge wasiwe mawaziri. Bunge la Juni tunakwenda kwenye bajeti, mawaziri watanyukwa vilivyo. Wanachopaswa kufanya sasa ni kujiandaa kupambana maana hali si nzuri kwenye wizara zao na wabunge wanataka kuona matokeo mazuri.

Swali: Nchi hii inaingia kwenye mabadiliko ya Katiba. Ni mambo gani ungependa yaingizwe kwanye Katiba mpya?

Jibu: Kama kuna neno napenda liingie kwenye Katiba mpya ni ‘uwajibikaji’. Uwajibikaji utakuwapo kwa kwa mawaziri kutokuwa wabunge. Naunga mkono mia kwa mia wazo la wabunge kutokuwa mawaziri. Mawaziri wanajiona na sisi ni wabunge. Tufanye kama Uganda wanavyofanya, hatua hiyo itaongeza uwajibikaji.

Katiba iwe na neno moja tu, mfumo mzuri wa ‘uwajibikaji’. Kwa sababu ya kutokuwa na mfumo mzuri, ndiyo maana hata hawa mawaziri walioondolewa imekuwa kama tumewavizia. Hawakupata muda wa kujitetea. Mtu apate fursa ya kujitetea, case kama ya Chami, alikuwa anabwa na sheria, hakupata fursa ya fair hearing (kujieleza) na kuulizana baadaye kuja kwenye conclusion on the issue of TBS (hitimisho suala la TBS). Kesi ya Nundu, ana kosa la kuingilia manunuzi ya bandari, lakini yuko sahihi kuhoji gharama ya ujenzi wa gati 13 na 14, huko tunakokwenda watu wawe wanapata fair treatment (wanatendewa kiungwana).

Mawaziri wakitoka nje ya wa Bunge itatusaidia kuondoa mgongano. Kwa sasa wabunge wapo kwenye bodi za mashirika ya umma na wanayasimamia. Hivi mjumbe wa Kamati ya Mashirika ya Umma unakwenda kuwa mjumbe wa Bodi NSSF, tukianza kikao cha Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma na wewe upo ndani utafanyaje? Utaitetea NSSF au utaikandamiza? Hapa ndipo ninaposema nchi yetu ione umuhimu wa kutenganisha mamlaka.

Swali:
Kwenye suala la Muungano unataka nchi yetu iwe na mfumo upi?

Jibu: Mkataba wa Muungano unasema kuwa shughuli za Serikali ya Zanzibar zitafanywa na Kinogozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambaye atakuwa ni Makamu wa Kwanza wa Rais, na kwa upande wa Tanganyika shughuli za Muungano zitafanywa na Makamu wa Pili wa Rais. Muungano ni dola. Tuwe na Rais mmoja tu. Mkuu wa Serikali ya Zanzibar na Mkuu wa Serikali ya Tanganyika waitwe mawaziri wakuu. Wawe na nguvu za kiutendaji. Hawa wateuliwe na Rais wa Muungano. Bunge la Muungano liwe dogo sana liwe kama seneti. Kiongozi wa chama kilichoshinda kwa kura nyingi ateuliwe kuwa Waziri Mkuu wa ama Zanzibar au Tanganyika.

Huyu Waziri Mkuu awe kiongozi mkuu wa shughuli za Serikali bungeni. Liwepo Baraza la Wawakilishi la Tanganyika na Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar. Isipokuwa Rais asiwe na nguvu ya kumfukuza Waziri Mkuu hadi Bunge liwe limeendesha kura ya kutokuwa na imani naye. Baada ya hapo, hawa mawaziri wakuu waamue aina ya utawala wanaoutaka. Wanaweza kuunda majimbo katika Tanganyika na Zanzibar, na haya yakaharakisha kasi ya maendeleo.

Swali: Katika hali ya sasa nini kinachokukera katika siasa?

Jibu:
Wanasiasa wamepoteza dhana ya kwamba cheo ni dhamana. Katika mawaziri wote waliotuhumiwa ni [George] Mkuchika pekee aliyeandika barua ya kuresign. Cheo ni dhamana kwa nini ung’ang’anie? [Rashidi] Kawawa alishakuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu, akapelekwa Wizara ya Ulinzi, [Edward] Sokoine mwaka 1977 na mwaka 1980 akaenda kusoma akiwa Waziri Mkuu, Sokoine akarudi Mzee [Cleopa] Msuya akaondoka akawa Waziri wa Fedha.

Mwaka 1985 [Mzee Ali Hassan] Mwinyi alipochaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, ikaonekana huwezi kuwa na Waziri Mkuu Mzanzibari, Mzee Salim Ahmed Salim akakubali kushuka cheo akawa Deputy Prime Minister (Naibu Waziri Mkuu), Mageni Msobi alikuwa Waziri wa Ardhi, akawa District Commissioner, huku kwetu concept ya cheo ni dhamana lazima irejeshwe. Napisha mwingine, Chami, Maghembe na Mkuchika ilikuwa ni sawa kabisa, tofauti na Ngeleja, Maige, Mponda, Nundu na Mkulo. Lakini badala ya kujiuzulu, Chami akaandika barua yenye page nne kwa Rais anajitetea, analalamika kwamba mimi (yeye)nimeonewa (kaonewa). Wapi na wapi! Kuna siku baadaye huko nchi inaweza kukupa madaraka makubwa zaidi. Tuwajibike jamani.

Swali: Umekaririwa ukisema unautaka urais. Je, bado una nia hiyo?

Jibu:
Bado natamani kugombea urais lakini sijasema lini. Watu wanadhani labda lengo langu ni 2015, mimi bado ni kijana, na sina haraka kabisa. Nilisema natamani na napenda kuwa Rais wa nchi hii. Watu wanajitokeza hapa wanasema uongo eti ohoo, nimeombwa na wazee, mimi haya mambo sikubaliana nayo. Ukimuuliza ataje hao wazee walioniomba hakuna hata mmoja ni uongo mtupu.

Najua nini nataka kuifanyia nchi, hata nikifa leo I am happy, I have done something (nina furaha nimefanya jambo) kwa ajili ya nchi yangu. You can’t talk about mining (huwezi kuzungumzia madini) bila kumtaja Zitto. Hivyo nasema wazi nautaka urais, lini? Hilo sisemi. Nafahamu wapi naweza kuifikisha.

 

 

1259 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!