Meneja wa Pori la Akiba Mkungunero lililopo mkoani Dodoma, Johnson Msellah, anatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yake pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Martin Loiboki, amezungumza na JAMHURI na kukiri kupokea malalamiko dhidi ya Meneja Msellah.

Amesema malalamiko hayo yapo ofisini kwake, na anaendelea kuyafanyia kazi.

JAMHURI imeambiwa kuwa Novemba 11, mwaka jana  hadi Machi 7, mwaka huu ilifanyika doria iliyohusisha washirika kutoka Kikosi cha Kupambana na Ujangili Kanda ya Kaskazini Arusha, Kanda ya Kati Manyoni na Washirika wa Pori la Akiba Mkungunero.

Msellah anadaiwa katika doria hiyo alikuwa anakwenda porini mara moja au mbili kwa mwezi, na kusaini kuwa amefanya kazi siku 30 na kulipwa Sh milioni 1.2 kwa mwezi kwa miezi minne. Februari 19, mwaka huu Msellah aliilipa Kamati ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Sh milioni 3 kwa ajili ya kusuluhisha mgogoro kati ya wafugaji wa Kimaasai na Kimang’ati ambao walikuwa wanagombea eneo lililopo ndani ya Pori la Akiba la Mkungunero.

Fedha hizo zilitolewa kwa hundi namba 109491 na kuwalipa kupitia Benki ya NMB, Tawi la Kondoa.

“Kitendo cha kuwalipa ni matumizi mabaya ya fedha kwa sababu hakupaswa kufanya malipo kwa ajili ya mgogoro ambao umesababishwa na watu ambao ni wavamizi wanaowasumbua askari kila siku,” kinaeleza chanzo chetu cha habari.

Akizungumza na JAMHURI, Msellah amesema akiwa msimamizi wa Pori hilo, wakati mwingine anakuwa na majukumu mengi ya kikazi ikiwamo kuhakikisha mambo yote yanakwenda sawa.

Kwa sababu hiyo, anasema kuna wakati anashidwa kutekeleza majukumu yote kwa wakati.

“Siyo kwa makusudi ila kwa kukosa muda kutokana na kuwa na majukumu ya hapa na pale,” anasema.

Anasema hakuna fedha za Serikali zinazotumika bila kufanyiwa hesabu katika matumizi, hivyo kila matumizi yapo ndani ya bajeti.

“Mimi sihusiki katika kufanya malipo yoyote ya posho kwa sababu kuna mtu ambaye anasimamia kufanya malipo hayo,’’ anasema.

Anasema kuwa hajawahi kuambiwa wala kusikia kwa mtumishi yeyote tuhuma dhidi yake, kwa kuwa kila jambo analofanya anashirikiana na wafanyakazi kujadili mambo mbalimbali.

Kuhusu tuhuma za ufisadi, anasema amekuwa akifanya vikao kila anaporudi kutoka katika safari za kikazi na pia huwapa nafasi ya kujadili na kuwafafanulia kila kitu wanachohitaji ufafanuzi.

Mkuu wa doria wa Pori hilo, Ayubu Sarikieli, anasema kazi kubwa wanayopaswa kufanya ni kuhakikisha watu hawavamii pori hilo.

Lakini anasema Msellah wakati mwingine amekuwa akikaa muda mrefu bila kuonekana katika Pori hilo. 

Sarikieli anasema wakati mwingine amekuwa akimwambia meneja kuhusu kufanya kazi, na kwamba amekuwa amkimjibu kuwa ana majukumu mengine mengi.

Anasema taarifa za utendaji wake zimefikishwa katika uongozi husika, lakini uongozi huo haujachukua hatua zozote.

Baadhi ya askari ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini, wanasema kuwa Msellah amekuwa akijilipa fedha nyingi bila kuwafanya kazi.

Wanasema mwaka jana walikutana na Naibu Mkurugenzi Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, ambaye aliwataka waendelee na majukumu yao wakati akiendelea kutafuta majibu ya malalamiko hayo, lakini hadi mwezi uliopita hakuna kilichotekelezwa.

Wameomba uongozi wa juu wa Wizara ya Maliasili na Utalii uwatembelee ili uelezwe ukweli wa mambo kuhusu uongozi katika Pori hilo.

2185 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!