Mengi, Muhongo, mawaziri chapeni kazi

galleryNikiwa hapa mkoani Morogoro, nimesikia tangazo la Baraza la Mawaziri. Itakumbukwa kuwa mara kadhaa nimesema na nimeendelea kuamini kuwa Profesa Sospeter Muhongo alistahili kurejeshwa katika Wizara ya Nishati na Madini. 

Si Muhongo tu bali hata Katibu Mkuu aliyeondolewa, kisha akapangiwa kazi ya Ukatibu Tawala Manyara, Eliakim Maswi, naye bado naamini anapaswa kurejea Nishati na Madini.

Ninazo sababu za msingi. Siwapendi watu hawa kwa sababu tu ni watani zangu, la hasha. Nimeangalia, na Watanzania tu mashahidi, kwamba wawili hawa kwa kipindi kifupi walichoshikilia wizara hii tulishuhudia mambo mengi. 

Kwanza tulipata fursa ya kufahamu kuwa nguzo zilikuwa zinatengenezwa Iringa, zinapelekwa Kenya kisha zinarejeshwa nchini ikidaiwa zimetoka Afrika Kusini.

Si hilo tu, Mtanzania wa kawaida kuomba kufungiwa umeme nyumbani kwake ilikuwa ni adhabu kabla yao. Profesa Muhongo ameshusha gharama za kufunga umeme kwa watu wa vijijini hadi Sh 27,000. Wala hoja siyo kushusha bei tu, nguzo zilisambazwa kweli, watu walifika mahala wapo nyumbani wanafungiwa mita na umeme unawashwa hata kabla hawajalipa hata senti tano.

Leo, tangu Muhongo na Maswi waondoke wizarani hapo, tumeshuhudia mgawo wa umeme, nguzo zilizomwagwa chini huko Tandahimba, Rulenge Ngara, Himo Moshi, Dodoma na maeneo mengi ya nchi hii sasa zinaozea chini. Kauli za watendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO) zimerejea palepale. Watendaji wameanza kudengua. Ukiomba umeme utafikiri hutalipia.

Sitanii, naifahamu kauli aliyotoa Profesa Muhongo na msigishano uliokuwapo kati yake na Mwenyekiti wa Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi. Wawili hawa walisigishana katika mtazamo wa nani anapaswa kuwekeza katika mafuta na gesi. Wakati Profesa Muhongo alikuwa na hoja kuwa gharama za uwekezaji ni kubwa, Mengi alikuwa na hoja kwamba wazawa wanapaswa kushirikishwa katika uchumi wa gesi.

Binafsi huipenda misigishano ya aina hii kwani mwisho wa siku huzaa matunda. Tumemsikia Rais John Magufuli akisema atawawezesha wazawa kushiriki katika uchumi wa gesi. Naamini Profesa Muhongo kwa kukubali uteuzi wa Rais Magufuli ambaye amenuia kuwezesha wazawa, naye amekubaliana na hoja ya wazawa kupewa fursa ya kuwekeza katika mafuta na gesi.

Napenda kuamini kuwa wagombanao ndiyo wapatanao. Sidjani kama Mwenyekiti Mengi ataendeleza kinyongo. Kwa kuwa hoja yake alikuwa akiisema wazi na si kwa kificho, kuwa sera ya kuwezesha wazawa ya mwaka 2004 itekelezwe kwa vitendo, binafsi nataka kuona Serikali hii ikiitekeleza sera ya uwezeshaji. Sera hii inawapa fursa wazawa kushiriki katika miradi mikubwa.

Kufanya hivyo wala haitakuwa ubaguzi. Nchi kama Afrika Kusini akifika mwekezaji asilimia 40 ya mradi wowote lazima iwe ya wazawa. Kama hakupata mzawa wa kuungana naye ni wazi mradi huo hautatekelezeka. Watanzania hawakufanya kosa kuzaliwa nchini Tanzania, nchi yenye rasilimali nyingi. Tusiruhusu wageni kuja kuchuma na kuondoka.

Kuna faida nyingi tukiwezesha wazawa kushiriki katika miradi hii mikubwa. Fedha zao zitakuwa zinakaa katika benki za ndani tofauti na wageni wanaodhani wakati wowote kinaweza kunuka na hupendelea kuhifadhi fedha zao ughaibuni. Tanzania haiwezi kujivunia kuendelea kuwa ya Watanzania maskini. Serikali inapaswa kuwezesha watu wake kwa maana kwamba Watanzania wakiwa na uwezo kifedha watalipa kodi.

Sitanii, kwa muktadha huo, naamini Mzee Mengi na Profesa Muhongo watakubali busara za wahenga kuwa wagombanao ndiyo wapatanao. Hatutakuwa na miaka mingine mitano ya malumbano, badala yake watashirikiana na kwa mwongozo alioutoa Rais Magufuli tutawaona wakizindua miradi ya wazawa – iwe kwa njia ya ubia au uwekezaji wa kujitegemea.

Nimesikia maneno ya hapa na pale juu ya Profesa Muhongo. Naamini naye amewasikia Watanzania wanaosema ni mbabe, bila shaka atawaeleza ukweli, atachapa kazi, umeme wa kutosha utapatikana na atawapa fursa Watanzania sawa na alivyowezesha vijana wengi wa nchi hii kwenda masomoni nchi za nje kujifunza masuala ya gesi na mafuta.

Nimeliangalia pia Baraza la Mawaziri lililoteuliwa. Niseme sina matatizo na Baraza hili isipokuwa baadhi ya mawaziri wawe macho kwani wizara walizotangulia kushika waliacha majipu, hivyo wakihamishia majipu hayo katika wizara walizopewa itakuwa shida.

Balozi Augustino Mahiga ni mtaalam aliyebobea katika masuala ya diplomasia. Ikumbukwe kwa muda mrefu amekuwa mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (UN). Alikuwa mwakilishi wa Katibu Mkuu katika Umoja wa Mataifa. Ni kiongozi asiye na tamaa. Huyu amekuwa mtumishi wa kweli katika nyanja za kimataifa na hana migogoro na watu.

Nape Nnauye, amekabidhiwa wizara inayoshughulikia masuala ya habari. Binafsi najua watu wengi wanavyomfikiria Nape yule wa majukwaani akiitetea CCM, ila Nape ni rafiki wa vyombo vya habari. Mara kadhaa amekuwa akitembelea vyombo vya habari, akibadilishana mawazo na wanahabari utadhani yeye ndiye aliyekuwa Waziri wa Habari.

Sioni fahari kumzungumza mtangulizi wake, Dk. Fenella Mukangara, ambaye zaidi ya TBC sina kumbukumbu alipata kutembelea chombo kipi cha habari. Waziri huyu alijikita katika mapambano na vyombo vya habari. Vyombo vya habari ni Muhimili wa Nne wa Dola na ni rafiki wa wasio waovu. Sikupata kuelewa kwa nini mama huyu alivichukia vyombo vya habari kiasi hicho. Nape naamini ataushinda mtihani huu.

Sidhani kama napaswa kusisitiza zaidi juu ya Profesa Muhongo. Huyu utendaji wake hauna mfano. Amejipambanua na wengi. Anatekeleza anachokiamini na moja tu, ambalo Rais Magufuli amemwambia litekelezwe ni hili la kuwezesha si tu wachimbaji wadogo, bali hata wa kati na wakubwa. Akifanya hivyo, historia itamkumbuka milele.

Jenista Mhagama amepewa Wizara ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu. Naamini mama huyu ni mkomavu katika siasa. Sina kumbukumbu za kumuona akifanya ubabaishaji. Hata hivyo, anapaswa kufahamu kuwa yeye ndiye atakayekuwa Mnidhamu Bungeni. Bunge la 11 litakuwa na changamoto, hivyo awe tayari kuzikabili. Asiwachukulie wabunge wa Upinzani kuwa kila wasemacho hakifai.

George Simbachawene na Angela Kairuki; hawa wafahamu kuwa wana dhamana kubwa. Ukiacha eneo la Utawala Bora, wanalo jukumu la kusimamia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Hapa ndipo maisha ya Watanzania yalipolala. Kila wizara, mengi ya mambo yake yanatekelezwa na TAMISEMI. Iwe ni shule za msingi, afya na mengine huko ndiko msingi uliko na nyumbani kwa mchwa unaokwaza maendeleo. Yawapasa kuchapa kazi kweli.

January Makamba sina maneno naye. Huyu wapo wanaomuona kama kijana mwenye fitina, na wengi wanamkumbuka alivyowabana Watanzania kupitia sheria ya makosa ya mtandao. Wanataraji nguvu aliyoitumia kwenye mitandao ya kijamii kitambo, sasa ataielekeza kwenye kulinda mazingira hasa kuzuia mkaa unaotaka kuligeuza Taifa hili kuwa jangwa.

Charles Kitwanga amekabidhiwa Wizara ya Mambo ya Ndani. Ni matumaini yangu kuwa ataipa heshima wizara hii. Sitarajii chini ya uongozi wake tusikie yupo Kamishna wa Polisi ambaye mke wake anatapeli watu kuwa atawapatia ajira. Sitarajii askari waendelee kupewa mafuta lita tano, kisha waagizwe kukamata majambazi yenye lita 1,000 kwenye gari. Ukiwawezesha polisi, wataimarisha amani na uchumi utakua kwa kasi.

William Lukuvi amepewa dhamana ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi. Kwa nchi zilizoendelea, wizara hii ndiyo mwarobaini wa kuondoa umaskini. Ikiwa kuna jambo Lukuvi anaweza kuwatendea Watanzania, basi ni kuhakikisha kila Mtanzania mwenye shamba, shamba lake lipimwe apate hatimiliki. Tukiwa na hatimiliki, basi tutakopesheka benki na kufanya uwekezaji utakaotukomboa kiuchumi. Ni imani yangu kuwa Lukuvi atahakikisha ardhi inapimwa.

Nimemfhamu Dk. Hussein Mwinyi zaidi ya miaka 20 sasa tangu nikiwa mwandishi wa habari za Bunge. Namkumbuka akiwa Naibu Waziri wa Afya chini ya Anna Abdallah alivyokuwa na uwezo mkubwa wa kujibu maswali na ambavyo hakuwa na majivuno. Ameongoza wizara hii kitambo sasa na sijasikia mang’uniko yoyote dhidi yake. Naamini ataendelea kuchapa kazi, bila wasiwasi.

Harrison Mwakyembe, huyu amepewa Wizara ya Katiba na Sheria. Wapo Watanzania wanaomtaja kuwa mmoja wa wapiga fitina nchini. Lakini pia wanatazama alikotoka na majipu aliyoacha. Makontena kupotea bandarini, kununua mabehewa feki 290, ambayo yakikimbia kasi ya kilomita 40 kwa saa yanadondoka na mengine. Bodi ya Bandari imevunjwa, Katibu Mkuu wa Uchukuzi ametimuliwa kazi, ila Mwakyembe aliyekuwa waziri wao yuko safi tu! Simsemi, ila aangalie mapito yake.

Mwigulu Nchemba, huyu amepewa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Hapana shana anafahamu kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanategemea kilimo. Ukiacha siasa zake za majukwaani na vijembe vya kisiasa, ukimtazama kwa jicho la uchunguzi wakati anatetea maslahi ya Taifa unauona uzalendo ndani yake. Naamini hatavaa suti kama mtangulizi wake na kuacha mbolea ikichakachuliwa au mazao ya wakulima yakioza kwa kukosa soko.

Kubwa afahamu kuwa watendaji wengi katika wizara hii hawajitumi. Hii ni wizara yenye wasomi wengi wataalam wa kilimo, mifugo na ugani. Wanatumia shahada zao za PhD kubabaisha mawaziri wanaoingia pale na kuishia kula fedha za miradi. Huko ndiko waliko wataalamu wa semina na makongamano. Mwigulu anapaswa kuwabana waende vijijini. Utaalamu wao tunautaka shambani na si kwenye semina na makongamano.

Charles Mwijage amepewa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Naamini amesikia muda wote Rais Magufuli alivyojinadi kwenye kampeni. Anatarajia uchumi wa nchi hii ukue kupitia viwanda. Mwijage afahamu kuwa analo jukumu kubwa la kuhakikisha ahadi ya Rais kwa Watanzania inatekelezeka. Kwa kushirikiana na Lukuvi watu wakipata hatimiliki, uwekezaji utawezekana kisha masoko ya bidhaa zinazozalishwa.

Ummy Mwalimu sina tatizo naye katika kazi aliyopewa ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Kwa kushirikiana na Naibu wake, Dk. Hamis Kigwangalla, naamini afya za Watanzania zitaimarika. Wajue kuna changamoto ya kila kata kuwa na kituo cha afya. Wajue nchi hii ina kipindupindu, hivyo wizara waliyopewa inahusu afya za Watanzania na hivyo wachape kazi.

Kwamba Wizara ya Sayansi, Teknolojia, Elimu na Ufundi, Waziri ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, mawaziri hawajapatikana hili nalo neno. Naamini Rais Magufuli atateua wachapa kazi katika eneo hili. Kubwa ninalotarajia, sitarajii kusikia maneno mkakati, mchakato, mipango… bali nataraji matokeo ya utekelezaji.

Sitanii, naomba kuhitimisha makala yangu kwa maneno yafuatayo. Inawezekana wapo mawaziri waliorejeshwa ambao watu wanadhani hawakustahili, ila niseme tu kuwa kichwa cha treni kikiwa kibovu, mabehewa hayawezi kwenda kasi. Kasi aliyoanza nayo Rais Magufuli inadhihirisha kichwa cha treni ni kipya na kimefanyiwa ukarabati nzuri. Watake wasitake, mawaziri hawa watachapa kazi tu. Mungu ibariki Tanzania.