Ninapotazama soka hapa nchini, nawaona wachezaji wetu ni kama yatima kutokana na mfumo wa ukuzaji wa vipaji wa nchi, kadhalika ni wa kujitakia. Kuna kitu kikubwa wachezaji wetu wanachokosa, wamekuwa ni watu wanaojipa majukumu mazito kwa kutokujua au ubinafsi tu.
Mchezaji kama alivyo Ramadhani Singano au Messi ni taasisi na anapaswa kuwa na jopo la wataalamu wa kumuongoza katika mambo kadhaa, ili kufikia ndoto zake katika kiwango alichotamani kwa miaka mingi.


Sidhani kama mchezaji anaweza kuwa na kipaji cha kusakata soka, kuijua vyema sheria ili imsaidie katika kusaini mikataba sahihi kwa usahihi na kuweza kujitafutia timu nyingine kubwa yenye maslahi bora zaidi.
Siamini kama mchezaji ana weledi bora kuhusu kutunza afya yake kuanzia mazoezi, vyakula na aina ya matibabu. Walau itoshe kusema kuwa ili mchezaji afikie ndoto zake anahitaji watu wa kumsimamia mambo yake.
Sisemi awaajiri hawa wote lakini walau awe na meneja wa kusimamia mambo yake yote ikiwamo kuwasiliana na mawakala, wataalamu wa saikolojia, sheria na kadhalika ili acheze soka na haya yafanywe na wengine. Apunguze mzigo wa majukumu na yeye acheze soka maana wachezaji wanatakiwa kuuishi mpira na haya mengine wakabidhi wataalamu husika wayafanye.

lionel-messi
Sidhani kama Lionel Messi wa Barcelona anajua hata kusoma mkataba na vile vifungu vya sheria. Sina hakika kama Yaya Toure anajishauri mwenyewe akiwa katika ‘stress’ za kushuka kiwango.
Siamini kabisa kama Falcao katika majeruhi yale alikuwa anawaza hospitali ipi aende na daktari yupi atamfaa. Naona wachezaji wanakosa vitu vingi sana kuanzia malezi ya vipaji vyao mpaka kuonekana lakini hata wakionekana wanayumba sana maana hawana usimamizi wowote.
Sidhani kama wachezaji hawa wana chama chao. Nilipata kusikia kuhusu makipa, lakini umoja wao una malengo yapi na malengo hayo ni ya aina gani? Unaweza ukakuta ni kwa ajili ya stori za hapa na pale na kusaidiana michango ya vocha mmoja akiwa katika ugumu au hata hilo yawezekana halipo kabisa.
Huwa haieleweki unaposikia Singano amekwenda kwenye kesi kwa sababu ya mgogoro wa mkataba wake pale Msimbazi. Messi halisi alikuwa na kesi za kukwepa kulipa kodi, lakini sidhani kama hata alikuwa na muda wa kuwaza kuhusu hiyo kesi.


Navuta picha ya Messi akiwa amesimama kizimbani anajibu kesi mbele ya hakimu aliyeshusha miwani yake mpaka kwenye ncha ya pua. Naona Messi angekuwa anatetemeka tu na hana cha kujibu na si ajabu angevurugwa kabisa na asingetamani tena kucheza mpira. Ila hapa kwetu ni kawaida mchezaji “kukomaa” mwenyewe na jambo ambalo siyo taaluma yake.
Namuona Lionel Messi akiwa anaambiwa na mtaalamu wa saikolojia kuwa kesi yake ni ndogo sana kuliko kipaji chake.
Namuona mtaalamu wake wa sheria akienda kupambana na kesi na kumwambia Messi kuwa kesi ile ni ya kitoto kabisa na wala siyo ya kumfanya ashindwe kuwapiga matobo mabeki pale uwanjani.


Hivi ndivyo mchezaji anavyopaswa kuishi ili kujitenga na jambo lolote litakaloua kipaji chake. Saa hizi huko Ulaya mawakala wanapishana hewani kwenda kujadili maslahi ya wachezaji katika timu zao za sasa au wanazotaka kwenda.
Saa hizi wakala anaamka anasema mchezaji wake hana furaha katika timu aliyopo wakati mchezaji huyo yupo ufukweni anaogelea tu wala hana habari. Wakala anafanya “vurugu” zote halafu mchezaji anaitwa kuweka saini tu.


Wakala anakuwa amemkabidhi mwanasheria mkataba na mwanasheria ameuchambua na wameridhika halafu mchezaji hana muda wa kupoteza kusoma mkataba zaidi ya kuweka dole gumba. Kwanza hata akisoma haelewi.
Suala la kupandisha thamani ya mchezaji hufanywa na mchezaji kwa miguu yake kisha mdomo wa wakala utavumisha kiwango kile mpaka dau litapanda. Hapa kwetu haya hayapo na ndiyo maana wachezaji wetu wanayumba sana na hata wakienda nje wengine hurudi kwa sababu ambazo hazieleweki masikioni mwetu.
Ukichunguza vizuri utagundua kuna tatizo la usimamizi ndiyo maana mchezaji anaweza kukataa ofa nzuri nje kwa kuwa ana mapenzi na timu yake na anasahau kuwa mpira ndiyo maisha yake na siyo suala la mahaba tena.
Kazi ya hawa watu wa kati ni kuvunja hayo mahaba, kuondoa ile tabia ya kupenda nyumbani na kuogopa kutoka nje ya hapa. Ndiyo, wengine hawaendi nje kwa kuwa wana “home sick” na au mahaba na timu zao hapa Bongo.
Wachezaji na hata makocha hebu changeni karata zenu vizuri, haya ni maisha yenu na mashabiki ni mashabiki tu wao watashangilia na mwishowe watawazomea sana tu. Wachezaji watendee haki vipaji vyao na siyo ushabiki wao kwa timu.
Najua vyema kuwa wapo wataalamu wanaoweza kuwaingiza wachezaji matatani kwa tamaa zao lakini hiyo itatokea tu endapo mtaalamu huyo ni wa kudandia. Mtu ambaye anajua kuwa mchezaji ndiyo taasisi iliyomwajiri, hawezi kuleta mchezo hata kidogo maana hata yeye anataka kufanikiwa kwa kumtendea vyema mchezaji wake.


Najua jambo hili haliwezi kufurahiwa na wamiliki wa klabu kwa kuwa litafanya wachezaji kuwa ghali lakini wao watapata faida kubwa kwa kuwa watakuwa na wachezaji wenye usimamizi mpaka nje ya uwanja. Itakuwa ni afya kwa soka letu kwa kuwa watakuwa na wachezaji wanaosukumwa kujituma ili thamani izidi kupanda na ofa nono zije mwishoni mwa msimu.


Wachezaji watacheza mpira na kazi ya kutafuta klabu nje itafanywa na wengine na hata “video clip” za mchezaji anayependa kumuiga atazikuta katika “Ipad” yake zikiwa zimeandaliwa tayari yeye kutazama na kujifunza.
Kingine kinachokosekana hapa kwetu ni wachezaji kukosa malengo ya muda mfupi ambayo yatawasafirisha kuelekea malengo yao makubwa. Tujifunze walau kwa wachezaji wa kigeni waliopo nchini.


Mchezaji anapotoka Nigeria, Ivory Coast, Cameroon na nchi nyingine kuja hapa nchini kucheza soka, tena akiwa na kiwango bora si kama amepotea njia bali ana malengo ya muda mfupi kuelekea malengo makuu.
Anatengeneza wasifu wake na kuondoa ile “home sick” taratibu ili muda ukifika asipate shida. Wachezaji wetu hawajifunzi ila utawasikia wanawarushia vijembe wachezaji hao eti mchezaji anayetoka nchi yenye mpira mkubwa hawezi kuja hapa na hao waliopo siyo wachezaji wa maana. Jamani eeh, kama hamuwezi kusoma basi nimewaletea picha mtazame.


Maana mambo haya yangefanyika kusingekuwa na ukame wa wachezaji huko majuu tena kusingekuwa na hizi kelele za utovu wa nidhamu usiokwisha, maana meneja angeshampeleka mchezaji kwa mtaalamu wa saikolojia. Sidhani kama kungekuwa na haya matatizo ya kusaini mikataba timu mbili tofauti au wachezaji kurushiana maneno na viongozi wa timu yake.
Wachezaji ongeeni kwa miguu yenu halafu haya mengine wapeni wenye fani zao ili huu mzigo mzito mnaojipa usiwepo tena na nyinyi mcheze soka la uhakika.

Baruapepe: [email protected] Simu: 0715 36 60 10

 

By Jamhuri