Mgogoro wa kisiasa katika Visiwa vya Zanzibar umekuwa na athari kubwa kwa Wazanzibari na Watanzania kwa jumla.

Ingawa hatuungi mkono misaada ya masharti, lakini kitendo cha Marekani kuinyima Tanzania msaada kwa sababu ya mgogoro huo, kinapaswa kutuamsha.

Tuamke kwa kuhakikisha Zanzibar kunapatikana suluhu ya kisiasa ya kudumu, badala ya utaratibu wa kupooza mambo na baada ya muda yakalipuka.

Mvutano wa kisiasa Zanzibar ni jambo lililo ndani ya uwezo wa Watanzania wenyewe, ndiyo maana tunaunga mkono uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kukemea mataifa yanayotaka kuutumia mvutano huo kama bakora kwetu.

Miaka kadhaa iliyopita Watanzania wenyewe walihakikisha wanasimama kidete kumaliza mgogoro Visiwani Zanzibar baada ya wasuluhishi, wakiwamo kutoka Jumuiya ya Madola, kushindwa.

Imani yetu ni kuwa bado Wazanzibari na Watanzania wenyewe tunao muda wa kutosha kuhakikisha mwafaka unapatikana na hivyo kuondoa doa hili mbele ya jumuiya ya kimataifa.

Pamoja na kupongeza juhudi zinazoendelea za kuleta suluhu, tunadhani kasi ya mazungumzo inapaswa iongezwe. Wazanzibari wana kiu ya kumchagua rais wanayemtaka, kwa hiyo kuendelea kuwachelewesha ni kuwanyima haki yao ya msingi.

Viongozi wakuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameshakutana na wenzao wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF). Mikutano yao imekuwa ikielezwa kwamba ni ya mafanikio makubwa yenye kutoa dalili za kufikiwa kwa mwafaka.

Pamoja na maneno hayo matamu, bado wananchi hawaoni kama kuna dalili za kutangaziwa uamuzi uliofikiwa au unaokaribia kufikiwa-yaani uamuzi wa kurejewa kwa Uchaguzi Mkuu Visiwani humo, au kumtangaza mshindi kwenye uchaguzi uliofanyika Oktoba, mwaka huu.

Lakini kumekuwapo hoja kutoka kwa vyama vingine vya siasa ya kwamba matokeo ya uchaguzi yaliyofutwa, si ya CCM na CUF pekee, bali yamo ya vyama vingine vya siasa. Ni kwa mantiki hiyo, vyama hivyo navyo vimetaka vihusishwe kwenye mazungumzo yanayoendelea.

Vyovyote iwavyo, kiu ya Wazanzibari ya kufanya uchaguzi wa rais ni kubwa; ndiyo maana tunazihimiza pande zinazohusika kulitambua hilo na ikiwezekana wananchi wapate haki yao ya kumchagua rais wanayemtaka. Tunadhani sasa vikao vimetosha.

Tukiwa tunasubiri kutangaziwa matokeo ya mazungumzo yanayoendelea, tunawahimiza Wazanzibari na Watanzania wote kuendelea kudumisha amani na utulivu kwani tunaamini penye mazungumzo sharti mwafaka upatikane.

1213 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!