Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Dk. Allan Kijazi, amezungumza na JAMHURI kuhusu mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano. Ifuatayo ni sehemu ya pili ya mahojiano ya Dk. Kijazi na Mwandishi MANYERERE JACKTON. Endelea…

Katika kuboresha uhifadhi, si tu kukabiliana na ujangili, lakini pia kuimarisha tafiti za kisayansi zinazotusaidia kujua hali halisi ya maeneo yetu ili tuweze kuweka mikakati ya kubuni mbinu nzuri za kuyasimamia.

Katika eneo hili tumekuwa tukifanya tafiti za ndani ya kiikolojia kubainisha mabadiliko ya kiikolojia yanayotokea katika maeneo yetu mbalimbali. Kubainisha pia sababu zinazochochea mabadiliko hayo, lakini pia kuangalia mbinu za kukabiliana na mabadiliko hayo.

Taarifa hizi za kisayansi zimetusaidia sana kuandaa mipango yetu ya usimamizi na uendeshaji mipango ya uhifadhi kwa kutumia mikakati ambayo inalenga kutatua changamoto ambazo ni halisia badala ya changamoto za kukisia.

Pamoja na hizi jitihada ambazo tumekuwa tukizifanya sisi wenyewe za kuwasaidia watafiti wetu kufanya hizo tafiti tumekuwa tukishirikiana pia na taasisi nyingine za nje ambazo huwa wana nia ya kufanya tafiti. Tunakaa na wenzetu wa TAWIRI tunabainisha umuhimu wa hizo tafiti katika maeneo yetu na zile tunazoona zina umuhimu, basi huwa tunashirikiana nao kuzifanya. Wakati mwingine huwa tunatumia taasisi zetu wenyewe za ndani ya Tanzania kama vyuo vikuu kwa maeneo tunayohitaji taarifa za haraka. Kwa vile uhifadhi ni sayansi, tafiti hizi zimetusaidia kutupatia taarifa za kisayansi ambazo zimetusaidia kukabiliana na tatizo la usimamizi wa uhifadhi hasa changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa kiasi kikubwa yameathiri na yanaendelea kuathiri hifadhi zetu.

Eneo la tatu katika uhifadhi ni changamoto ya mipaka. Tumekuwa na migogoro ya muda mrefu ya mipaka kati ya hifadhi na wananchi. Changamoto hii imekuwa ikisababishwa na vitu viwili – kwanza; wananchi kutoelewa hiyo mipaka.

Pili, kuna maeneo ambayo wananchi wanaelewa mipaka lakini kutokana na ile dhamira ya kutaka kutumia rasilimali zilizopo katika hifadhi wamekuwa wakiikataa ile mipaka na kutaka kulazimisha ibadilishwe. Baada ya kuligundua tatizo hili, serikali kupitia kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu iliagiza tufanye survey ya mipaka yetu yote na tuweke vigingi (beacons) kwenye maeneo yote ambayo ndiyo mipaka ya hifadhi kwa kufuata GN zilizoanzisha hizo hifadhi. Tulishirikiana na wenzetu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi tukaweka beacons katika maeneo yote na sasa hivi hakuna mahali ambako wananchi watasema mpaka hatuufahamu.

Maeneo yote yameshawekewa mipaka isipokuwa maeneo machache ambayo bado yana migogoro. Hatua ambayo tumeifanya baada ya kumaliza kazi hiyo sasa hivi tunaandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji vyote 392 vinavyozunguka hifadhi za taifa.

Kazi hii itagharimu shirika kati ya Sh bilioni 4 mpaka Sh bilioni 5. Tunaamini mipango ya matumizi ya ardhi ikiandaliwa itasaidia wananchi pia kusimamia maeneo yao kikamilifu kwa sababu watajua ni kitu gani kinafanyika wapi na kwa sababu gani.

Lakini pia kwa sababu mipango hii ni mipango ya matumizi ya ardhi, itabainisha fursa mbalimbali ambazo wananchi wanaweza  wakazitumia – zinazotokana na uhifadhi ili wafaidike. Itasaidia kuongeza kipato chao cha mtu mmoja mmoja, lakini pia kama jamii, hivyo kuona umuhimu wa uhifadhi.

Kwa mantiki hiyo tunatarajia kwamba ule ule uungaji mkono shughuli za uhifadhi utazidi kuwa mkubwa.

Kazi hii ya matumizi ya ardhi inafanywa na Tume ya Ardhi. Wao wanatoa utaalamu, fedha tunatoa sisi. Kimsingi kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ni kazi ya hiyo tume katika nchi nzima, lakini sisi tunawawezesha.

Mwaka huu wa fedha (2018/2019) tutakamilisha kwa vijiji 92 na mwaka ujao tunatarajia kuwa na vijiji kama 100. Baada ya miaka mitatu mipango hii itakuwa imekamilika, na hii mivutano tuliyonayo na wananchi kuhusu matumizi ya ardhi itakuwa imepungua.

Uzuri wa hii mipango ni kuwa kwa vile inafanywa na taasisi iliyopewa mamlaka ya kisheria ya kuiandaa na kuisajili hii mipango, ina maana ikishaandaliwa viongozi wa vijiji wanawajibika kuisimamia kikamilifu. Wakishindwa kuisimamia sheria inaruhusu wenzetu wa Tume ya Ardhi kuwachukulia hatua za kisheria. Kwa hiyo hata viongozi wa vijiji watakuwa wamebanwa kisheria. Hawana namna nyingine yoyote ya kutumia mbinu kuharibu utaratibu ule ambao umewekwa kwa sababu wanaweza wakaishia mahakamani kwa kushindwa kusimamia sheria.

Kwa mantiki hiyo basi, utakuta katika maeneo yote yanayozunguka hifadhi tutakuwa na watu ambao wanasimamia maeneo yao kikamilifu na sisi itatusaidia nguvu kule nje na kuweka nguvu katika maeneo ambayo tuna mamlaka nayo kusimamia.

Eneo la Loliondo bado serikali haijatoa uamuzi. Yako mapendekezo ambayo yameshajadiliwa, taarifa tuliyonayo ni kwamba yameshafikia hatua ya juu ya uamuzi na wakati wowote uamuzi unaweza ukatolewa. Lakini serikali imetamka bayana kwamba ingependa kuona eneo lile linabaki katika hadhi yake ya uasili kwa maana kwamba ndiyo chanzo kikubwa cha maji kwa Mto Mbalageti;  kwa hiyo ni eneo ambalo ni muhimu kwa ajili ya uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Uamuzi wowote utakaotoka utahakikisha kwamba maeneo yale yanatunzwa kikamilifu na hayataharibiwa kwa ajili ya shughuli za kibinadamu. Sasa ni aina gani ya utawala utakaokuwapo kusimamia, hilo tunasubiri maelekezo ya serikali, lakini cha msingi ninachokijua ni kwamba serikali inatambua umuhimu wa hilo eneo na haitakubali kuona linaharibika.

 

Faida za Jeshi usu

Kuanzishwa kwa hili jeshi hii yote ni katika azima yetu ya kuhakikisha tunaimarisha nguvu katika kupambana na ujangili. Ili uweze kupambana na ujangili, lazima uwe na vifaa vya kutosha – maana ya silaha lakini pia na vifaa vingine ambavyo vitakuwezesha askari kupambana na ujangili.

Tumekuwa tukipambana na changamoto kama shirika ambalo linasimamia hifadhi, tumekuwa tukitumia silaha kupambana na majangili, lakini sheria inayoanzisha hizi hifadhi haitutambui sisi kama tunaweza kutumia silaha za kivita.

Kwa hiyo imekuwa vigumu wakati mwingine kukabiliana na ujangili kikamilifu, tumekuwa tukitegemea wenzetu wa Jeshi la Polisi  au wenzetu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) pale ambako tunaona kuna haja ya kutumika silaha na nguvu, kwa sababu sheria haitutambui sisi kwamba tunaweza tukatumia nguvu na tunaweza tukatumia silaha katika matukio kama hayo.

Lakini sisi ndio tumepewa mamlaka kisheria ya kulinda rasilimali hii. Unaweza ukaenda ukafanya doria ukakumbana na watu wana silaha nzito za kivita, huwezi ukaondoka kwenda kutafuta Jeshi la Wananchi au Polisi ili wakupe msaada.

Utakuta wale wameshafanya ujangili na wameondoka. Tumeona, na serikali imeona ni vizuri tukajenga uwezo wetu. Msaada wa hao wenzetu wa Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi utumike tu pale inapokuwa lazima, lakini sisi wenyewe tuwe na uwezo wa kupambana na majangili wakati wowote bila kutegemea nguvu ya polisi au JWTZ, lakini pia sheria itutambue kwamba hata tunapokabiliana nao lolote likitokea bado sheria inatutambua kwamba tunaweza kutumia nguvu na tukatumia silaha katika matukio kama hayo.

Hiyo imetusaidia pia kuwapa vijana wetu ari – ile kujiamini wanapokuwa kazini kwamba sheria inawalinda. Kulikuwa na woga wa awali kwamba mtu anatumwa kazi, lakini anasema hivi nikikutana na majangili nafanya nini?

Nikimpiga risasi, kitu cha kwanza [askari] ni kuwekwa ndani – umempiga risasi kwa mamlaka ipi? Sheria ipi inakulinda? Tulikuta vijana wetu wengi walikuwa wanawekwa ndani katika matukio ambayo kimsingi hawakustahili kuwekwa ndani. Kwa kuwa sasa tunatambuliwa kisheria, vijana watakuwa wanafanya kazi kwa kujiamini na itasaidia sana kudhibiti ujangili, kwa sababu ule woga wa kwenda doria na kutumia silaha unakuwa haupo.

By Jamhuri