Msongamano wa abiria wanaotumia usafiri wa mabasi ya haraka jijini Dar es Salaam maarufu kama (mwendokasi) kwa kiasi kikubwa unatokana na uzito wa kufanya uamuzi miongoni mwa watendaji serikalini.

Hali ya kuchelewa kufanya uamuzi inakinzana na kasi ya Rais Dk. John Magufuli katika kutatua kero za wananchi, Gazeti la JAMHURI limebaini kuwa wakati mradi ukiwa umepangwa kuwa na mabasi 305 kwa ajili ya kuhudumia abiria 300,000 kwa siku, kwa sasa kuna mabasi 140 tu ambayo hutoa huduma ya abiria hadi 220,000 kwa siku.

Lakini wakati hali ikiwa hivyo kitakwimu, kuna mabasi mengine 70 yamezuiliwa bandarini kwa sababu mbalimbali, mabasi ambayo yangeweza kuondoa msongamano wa sasa unaohusisha mabasi hayo kubeba abiria hadi mara mbili ya uwezo wake.

Mabasi hayo 70 yamezuiwa kutokana na kile kinachoitwa mvutano kati ya Wakala wa Serikali anayesimamia mradi huo (DART) na kampuni inayotoa huduma kwenye mradi huo (UDA Rapid Transit – UDART) bila kujali namna abiria wanavyohatarisha maisha yao kwa kujazana kupita kiasi kwenye mabasi nyakati za asubuhi na jioni.

Kwa kipindi cha mwaka mzima tangu mabasi haya yaingie nchini DART Agency wamekuwa wakinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari kuwa UDART hawajafuata utaratibu katika kuyaagiza na kuyaingiza nchini huku UDART wakieleza kuwa wanasubiri kibali cha wakala wa serikali ili mabasi haya yaingie barabarani.

Taarifa za kiuchunguzi zinabainisha kuwa idadi ya juu ya kusafirisha abiria iliyofikiwa kwa siku ni 220,000, kwa idadi ya mabasi 140 yaliyopo lakini mradi huo unapaswa kuhudumiwa na mabasi 305 na malengo yakiwa kusafirisha abiria 300,000 kwa siku katika awamu ya kwanza yenye barabara zenye jumla ya kilomita 20.9.

“Mradi ulianza kwa majaribio ndiyo maana mabasi 140 yakaanza badala ya idadi iliyotakiwa. Kilichotokea ni kwamba mwitikio wa abiria haukuwa wa majaribio, sasa kilichopaswa kufanyika ni kuhakikisha kuwa muda wa majaribio unakuwa mfupi ili kuruhusu idadi inayotakiwa ya mabasi, hii ingefanyika kwa wakati tusingefika hapa,” anasema mmoja wa wahandisi aliyehusika katika usanifu wa mradi wakati wa hatua za awali, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuwa si msemaji rasmi.

 “Chanzo cha matatizo yote unayoyaona sasa ni capacity (uwezo wa kubeba abiria). Hili lisiposhughulikiwa mapema litaufanya mradi huu ukose maana pamoja na malengo yake mazuri,” anasisitiza mtaalamu huyo.

Mradi huo unaofahamika kwa jina la Dar Rapid Transit (DART) unatumia mabasi 140 yakiwamo mabasi marefu 39 yenye mita 18 (articulated buses) yakiwa na uwezo wa kubeba abiria 155 kila moja na mafupi 101 yenye urefu wa mita 12 (rigid) yenye uwezo wa kubeba abiria 90 kila moja. Hata hivyo uchunguzi wetu umebaini kuwa magari hayo yamekuwa yakijaza abiria kupita kiasi hasa nyakati za asubuhi na jioni.

“Abiria tunajazana mno kiasi kwamba siku kukitokea jambo (Mungu aepushe mbali) nchi itazizima. Lakini nashangaa, haya mabasi ni machache yanatakiwa kuongezwa. Mimi sijui kwa nini viongozi hawalioni hili,” anasema Maria Joseph, mkazi wa Kimara Korogwe anayetumia usafiri huu kila siku.

Akizungumza kuhusu mvutano unaohusisha mabasi 70, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa UDART, Deus Bugaywa, anasema UDART waliagiza mabasi hayo baada ya kujiridhisha na ongezeko kubwa la abiria.

“Ilikuwa wazi tangu mwishoni mwa mwaka 2017 tulipofikia idadi ya abiria zaidi 200,000 kwamba kuna haja ya kuongeza idadi ya mabasi. Juhudi zilifanyika na Februari 2018 tulipokea mabasi 70 mapya yenye uwezo wa kubeba abiria 155 kila moja.

 “Haya yakiingia barabarani yataongeza uwezo wetu wa kubeba abiria mara mbili zaidi, na haya matatizo ya kujaza kupita kiasi, kusubiri kwenye vituo muda mrefu yatakwisha,” anasema Bugaywa.

Alipoulizwa kwa nini mabasi hayo hayakufuata utaratibu wakati wa kuingizwa nchini na sakata hili litafikia mwisho lini kwa sababu mivutano yao inawaumiza wananchi wanaotumia usafiri huo, anasema suala hilo limefika ngazi za juu na hawezi kulizungumzia.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kwamba kuagizwa kwa mabasi hayo kulifanywa na mwanahisa mmoja wa UDART ambaye ni Simon Group mwenye hisa asilimia 51 bila kushirikisha upande wa mwanahisa wa pili (Serikali) anayemiliki hisa asilimia 49 kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Chanzo kingine kutoka ndani ya DART Agency kimeeleza kuwa wakati mabasi hayo yanaagizwa, bodi ya UDART ilikuwa na wajumbe wa upande mmoja tu wa Simon Group Ltd, wakati upande wa Serikali ulikuwa haujateua wajumbe wake.

“Msingi wa tatizo uko hapo. Mwanahisa mwingine hataki kuyatambua (mabasi 70). Masuala ya kodi yanayosemwa siyo kikwazo kikubwa … yanajadilika,” kinasema chanzo hicho.

Akizungumza kuhusu suala la abiria kuhatarisha maisha kutokana na msongamano kwenye magari hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa DART, Ronald Lwakatare, anasema: “Tumekuwa tukishirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) pamoja na Jeshi la Polisi. Ni kweli kuna tatizo la uchache wa mabasi. Tumechukua hatua za muda mfupi kama kuingiza mabasi madogo yaliyokuwa yakifanya safari kati ya Mbezi na Kimara sasa yafanye safari ndefu.

“Unajua huu mfumo wetu, kwenye haya mabasi hakuna kondakta au mtu wa kuwazuia abiria wasiingie pale basi linapokuwa limejaa. Kwa hiyo hatua za muda mfupi ni hizo za kuingiza mabasi hayo madogo yanayoitwa ‘bombardier’.

 “Lakini kuna hatua za muda mrefu, hizi ni pamoja na kumpata mzabuni mwingine wa kuongeza nguvu. Na tunatarajia hapo baadaye kuweka utaratibu wa vituoni kuonyesha ratiba za mabasi, kwamba baada ya muda fulani basi litafika kwa hiyo abiria hawatakuwa tena na usumbufu.

“Mwekezaji aliyepo amekuwa akijitahidi ingawa anakabiliwa na changamoto kadhaa. Haya mabasi yamekwisha kutembea kilomita 300,000 ambazo ni nyingi kiasi cha kuhitaji kufanyiwa matengenezo makubwa (overhaul) yanayohitaji hadi uagizaji wa vipuri kutoka nje, mwekezaji anajitahidi kwa hilo,” anasema Lwakatare.

Kuhusu mabasi 70 yaliyozuiwa, amesema mwekezaji anatakiwa kukamilisha taratibu za uagizaji wa mabasi hayo na kusisitiza kuwa yanahitajika kwa haraka kusaidia kuondoa tatizo la msongamano lililopo.

JAMHURI limezungumza na Msajili wa Hazina, Athuman Mbutuka, ambaye ndiye msimamizi wa hisa za Serikali katika mradi huo, ambaye hata hivyo alilitaka JAMHURI kuwasiliana na Ofisa Mawasiliano wa ofisi yake.

JAMHURI limezungumza na Ofisa Mawasiliano huyo, Gerald Temu, ambaye amefafanua kuwa Msajili wa Hazina ni mwanahisa, kwa hiyo hawezi kuzungumzia operesheni za kila siku za mradi huo, na kwamba hilo ni jukumu la waendeshaji wa mradi.

“Sisi wanahisa tunavyo vikao vyetu vya kuhudhuria. Tukisema tuzungumzie mwenendo wa mradi tutakuwa tunaingilia majukumu ya waendeshaji. Wasiliana na waendeshaji wa mradi huo,” anasema Temu.

Kwa upande mwingine, kutokana na msongamano unaohatarisha maisha ya abiria, wadau mbalimbali waliozungumza na gazeti hili wametaka busara kutangulizwa ili hatimaye mabasi hayo 70 yaachiwe kwenda kukabiliana na msongamano wa sasa.

Rais Magufuli alizindua mradi wa mwendokasi awamu ya kwanza Januari 25, mwaka 2017. Mradi huo umefanywa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.

Katika siku hiyo ya uzinduzi Rais Magufuli aliziagiza mamlaka zinazohusika na uendeshaji wa mradi huo wa mwendokasi (DART) kuhakikisha unaendeshwa kwa faida.

Rais amesisitiza kuwa ni lazima DART iwe chachu ya kufanikisha utekelezaji wa miradi mingine ya miundombinu  na kwamba mradi huo katika awamu yake ya kwanza wenye umbali wa kilometa 20.9 umeigharimu serikali kiasi cha shilingi bilioni 403, ambapo kati ya hizo shilingi bilioni 317 ni mkopo kutoka Benki ya Dunia.

Kwa wakati huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi hayo (DART), Leonard Lwakatare, alisema wakati wa uzinduzi wa mradi wa mabasi hayo tayari walikuwa wamekusanya kiasi cha shilingi milioni 800.2 na kiasi hicho kilipanda mwezi Desemba mwaka 2016 kufikia shilingi bilioni 3.39.

By Jamhuri