Huduma ya maji kumfikia kila mwananchi

Kazi zinaendelea na Wiki ya Maji 2019 imekamilika. Kitaifa Wiki ya Maji imeadhimishwa jijini Dodoma kwa wataalamu na wadau wa sekta hii muhimu kukutana na kuangalia namna bora zaidi ya kufanikisha huduma muhimu ya majisafi na salama inawafikia wananchi bila vikwazo.

Matukio makubwa yanayoigusa sekta ya maji yaliyofanyika ni Kongamano la Kisayansi kuhusu sekta ya maji, Siku ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ambapo ripoti za utendaji wa mamlaka za maji zilizinduliwa na Mkutano wa Mapitio ya Sekta ya Maji nchini.

Kaulimbiu ya maadhimisho ikiwa “Hakuna Atakayeachwa: Kuongeza Kasi ya Upatikanaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa Wote katika Dunia Inayobadilika Kitabia Nchi”.

Changamoto katika sekta ya maji zipo, Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa anasema na kuongeza kuwa pamoja na changamoto hizo, siku za usoni ni zenye heri zaidi. Serikali inafanya juhudi kubwa kuhakikisha Watanzania wanapata majisafi, salama na yenye kutosheleza.

Waziri anaongeza kuwa kufanya kazi katika sekta ya maji ni heshima kubwa, na ukweli ni kuwa maji hayana mbadala, ndiyo yanayowezesha mambo mengi zaidi katika maisha ya kila siku, iwe kilimo, viwanda,  biashara au kuongeza thamani ya bidhaa.

Prof. Mbarawa pamoja na changamoto, anasema wakati wa wiki ya maji ndipo amepokea simu kutoka kwa wakazi wa Longido, mkoani Arusha wakishukuru kwa kupata huduma ya majisafi ambayo chanzo chake ni Mto Simba, ulioko Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.

Anaongeza kuwa wataalamu katika sekta ya maji wanapojitoa kwa nguvu zote katika kazi, wanaleta furaha kubwa kwa wananchi.

Mradi wa maji wa Longido unazalisha maji kiasi cha lita za ujazo 2,160 kwa siku wakati mahitaji halisi katika mji wa Longido ni lita za ujazo 1,462 kwa wakazi wapatao 16,700. Mradi huo umegharimu kiasi cha Sh bilioni 15.7 na umeleta mabadiliko kwa huduma kupatikana kwa asilimia 100.

Prof. Mbarawa anasema huduma ya maji ni muhimu kwa wananchi na serikali inatekeleza miradi mbalimbali, ikiwamo mradi wa maji wa Mwanga, Same – Korogwe. Mradi huo unatekelezwa katika awamu mbili; awamu ya kwanza inahusu ujenzi wa miundombinu ya uzalishaji wa majisafi, pamoja na miundombinu ya usambazaji wa maji katika Mji wa Same, Mji wa Mwanga na vijiji tisa (9).

Awamu ya pili inahusu usambazaji wa maji katika vijiji 29 vya wilaya za Mwanga, Same na Korogwe vilivyo katika eneo la mradi. Serikali inatekeleza awamu ya kwanza ambayo imegawanywa katika vipande vinne kwa kuzingatia ukubwa wa kazi.

Waziri Mbarawa anasema kuwa ujenzi ukikamilika mradi utakuwa na uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 103.68 kwa siku, ikilinganishwa na mahitaji ya sasa ambayo ni lita milioni 78.38 kwa siku.

Miradi mingine itakayowanufaisha wananchi ni pamoja na mradi wa maji wa Ziwa Victoria kwenda Nzega, Tabora na Igunga ambao umefikia asilimia 56 na utanufaisha vijiji 69. Uzalishaji wa maji katika mradi huu utakuwa lita za maji bilioni 55.

Waziri anaongeza kuwa mradi mwingine ni mradi wa maji wa Chalinze awamu ya tatu ambao umefikia asilimia 79.5 hadi kufikia Desemba, 2019. Jitihada hizi ni pamoja na kufikia malengo yaliyowekwa itakapofika mwaka 2020.

Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), 2015 – 2020, inaelekeza kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji mijini kufikia asilimia 95 katika miji mikuu ya mikoa na Dar es Salaam; na asilimia 90 katika miji mikuu ya wilaya, miji midogo na miradi ya kitaifa.

Hivyo, ili kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa Serikali inawekeza kwa kujenga, kupanua na kukarabati miradi ya maji katika maeneo mbalimbali. Hatua hizi zimewezesha kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi, kwa maeneo ambayo miradi imekamilika, na baadhi ya maeneo wakisubiri kukamilika kwa miradi.

Maadhimisho ya wiki ya maji kwa mwaka 2019 yamefanikishwa kwa kazi mbalimbali, ikiwamo, uwekaji wa jiwe la msingi la Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira Misungwi utakaotumia jumla ya shilingi bilioni 276. Hatua za utekelezaji wa mradi huu zinafanyika katika miji ya Mwanza, Musoma, Bukoba, Magu, Lamadi, na Misungwi.

Waziri wa Maji, Mhe. Makame Mbarawa (Mb), anasema mradi wa maji wa Misungwi  utaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita laki 6.5 ambazo ni sawa na asilimia 17 ya upatikanaji wa majisafi na salama, hadi kufika lita milioni 4.5 hadi 6, ambapo mahitaji ya maji kwa sasa ni lita milioni 3.9.

Waziri Mbarawa anaeleza kuwa pamoja na juhudi hizo, moja ya vigezo vya kupanga bei za maji ni vizuri kuangalia nishati inayotumika katika uzalishaji. Inaweza kuwa ni mafuta, maji kujisukuma yenyewe (gravity) au nishati ya jua (solar). Hatua hii pamoja na mengine itasaidia wananchi katika kupata huduma bora za maji na mamlaka za maji katika gharama za uzalishaji na kujiendesha.

Waziri wa Maji anazitaka mamlaka za maji nchini kufanya utafiti na kuangalia namna bora ya kuagiza dawa za kutibu maji kwa pamoja. Nia hasa ya kufanya utafiti ni kuangalia namna ya kupunguza gharama, na wananchi kuendelea kupata huduma bora zaidi za majisafi.

Kuhusu huduma za majisafi zinatolewa na mamlaka za maji nchini, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo, anasema mamlaka hizo kwa uhalisia zinatoa huduma kwa Watanzania na si biashara.  Prof. Mkumbo anasema mamlaka za maji zisichukuliwe kama kampuni za kibiashara, na ni vizuri kila mdau akilielewa hilo kwa undani zaidi.

Prof. Mkumbo anasema Wiki ya Maji ni jukwaa adhimu linalokutanisha sekta ya umma, sekta binafsi, Wanazuoni na AZAKI kuweza kubadilishana uzoefu na kung’amua masuala mbalimbali katika sekta ya maji. Lengo hasa likiwa moja la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya majisafi na salama, na kuhakikisha maeneo yenye changamoto yanapata jibu mara moja.

Anaeleza kuwa upo umuhimu wa kuweka mipango ya menejimenti na utunzaji wa rasilimali za maji, pia  kuimarisha taasisi zinazohusika na menejimenti ya rasilimali za maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya maji na yenye viwango.

Prof. Mkumbo anasema wakati maji hayaongezeki, matumizi yake yanaongezeka kila siku, ikiwamo idadi ya watu. Tafiti zinaonyesha kuwa ifikapo mwaka 2050 nchi tano (5) barani Afrika zitakuwa miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya watu duniani, nchi ya Nigeria ikiongoza ikiwa ya tatu (3) kwa watu milioni 793, wakati Tanzania ikiwa nafasi ya nane (8) kwa idadi ya watu milioni 303. Hivyo, kutunza vyanzo vya maji ni lazima kwa huduma endelevu na za uhakika.

Maadhimisho ya Wiki ya Maji yanafanyika sambamba na Azimio Na. 47/193 la Umoja wa Mataifa (UN) linalozitaka nchi wanachama kuadhimisha Siku ya Maji Duniani kila mwaka, tarehe 22 Machi kila mwaka.