Kutokana na sekta ya utalii kutiliwa mkazo na Serikali ya Awamu ya Tano kwa ajili ya kuinua uchumi wa nchi, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi iliyopo Kilosa, mkoani Morogoro imejipanga kuongeza shughuli za kitalii kwa lengo la kuvutia watalii wengi zaidi.

Hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilometa za mraba 3,230, inasifika kwa kuwa na wanyama wa kila aina wakiwemo tembo, simba, nyati na twiga.

Katika mbuga hiyo inaelezwa kuwa faru ndiye mnyama pekee asiyepatikana kutokana na vitendo vya ujangili dhidi yake vilivyofanywa tangu mwaka 1980.

Hifadhi ya Mikumi inasifika kwa kufikika kwa urahisi. Hali hiyo ikielezwa kutokana na uwepo wa barabara ya lami iliyopitishwa katika hifadhi hiyo.

Akizieleza shughuli kubwa za kitalii zinayofanyika katika hifadhi hiyo, Mhifadhi Utalii wa Hifadhi ya Mikumi, Happiness Kiemi, anasema ni utalii wa kutumia magari (game drive tourism).

Aina hiyo ya utalii anaitaja kuwahusisha wageni wanaokuja na magari yao na kulipia kiingilio pamoja na gari ili waweze kuingia kutalii katika hifadhi hiyo.

Anasema kiingilio kwa wazawa wanaoingia katika hifadhi hiyo ni Sh 5,900 na kwamba gharama za kuingia na gari lenye uzito kuanzia kilo 2,000 ni Sh 35,000.

Pamoja na hifadhi hiyo kuwa kubwa, anasema si eneo lote linatumika kwa utalii, bali kuna maeneo maalumu yametengwa na mengine yamehifadhiwa kwa lengo la kutunza uoto.

Mhifadhi utalii huyo anasema wageni wanapofika hifadhini wanatembelea sehemu zilizoainishwa kwa utalii peke yake.

Kiemi anasema zipo barabara (circuit) ambazo zimetengenezwa mahususi kwa ajili ya magari kupita na kwamba wageni wanapopita katika barabara hizo hawaruhusiwi kufanya kitu chochote zaidi ya kupiga picha tu.

“Kama kuna maeneo wanaruhusiwa kushuka kwenye gari ni machache sana, vinginevyo wanatakiwa kukaa ndani ya magari, na hiyo ndiyo shughuli kubwa ambayo tunafanya katika Hifadhi yetu ya Mikumi,” anasema Kiemi.

Mbali na utalii wa aina hiyo, Kiemi anasema kuna utalii wa kuona wanyamapori nyakati za usiku, anasema utalii wa aina hiyo unatokana na tabia za wanyama wengine kupenda kuonekana usiku.

Anasema kwa nyakati za usiku watalii wanaweza kuwaona wanyama wote jamii ya paka, wakiwemo chui na simba.

“Kuna wanyama ambao mchana wanakuwa wamelala, lakini ukifika usiku wanaamka kwa ajili ya kutafuta chakula, ukifanya utalii wa usiku katika Hifadhi yetu ya Mikumi ndipo unaweza kuwaona wakifanya kitendo cha kuwinda.

“Hata simba ni rahisi kumuona usiku akiwinda, unaweza kutalii mchana ukamuona amelala tu na hafanyi chochote, ila ukitalii wakati wa usiku utabahatika kumuona akiwinda swala au nyumbu,” anaeleza Kiemi.

Anataja aina nyingine ya utalii ni wa kutembea kwa miguu. Anaeleza kuwa aina hiyo hufanywa na mgeni kwa kuambatana na askari wa wanyamapori kwa ajili ya kuwapatia ulinzi wakati wakitembea.

Utalii wa aina hiyo anauelezea kwamba unafanyika katika njia maalumu zilizotengenezwa kwa ajili ya watembea kwa miguu wenye lengo la kupata mshangao katika nafsi zao ‘adventures’.

Anasema aina ya wageni hao mara nyingi ni wale wanaotaka damu yao ikimbie na kusisimuka wakiwaona wanyama kama simba au tembo wakiwa karibu yao.

“Hawa wakati wanatembea wanaweza kuona wanyama wa kila aina, wanaweza kuwaona tembo au simba, hapo lazima wapate msisimko na kuwafanya damu kukimbia kwa sababu ya kupata mshituko usio wa kawaida,” anasema Kiemi.

Mhifadhi huyo anafafanua kuwa wametenga njia za aina mbili za kufanya utalii wa kutembea kwa miguu, ambapo kuna njia fupi na ndefu.

Kiemi anaongeza kuwa ipo fursa ya utalii kwa wafanyabiashara au wageni wanaopata nafasi ya kufanyia mikutano yao katika kumbi zilizomo kwenye Hifadhi ya Mikumi.

 Anasema ikiwa wafanyabiashara watafanya vikao vyao katika kumbi hizo hupata fursa ya kutembelea hifadhi kwa muda wa jioni na kuona wanyama.

Kwa mujibu wa Kiemi, aina hizo za utalii zinafanyika katika upande wa kaskazini wa hifadhi na kwamba katika kupanua wigo wa kufanya shughuli za kitalii katika Hifadhi ya Mikumi wanao mpango wa kufungua shughuli nyingine ya kitalii ya kupanda milima (hiking).

Anasema kutokana na Hifadhi ya Mikumi kuzungukwa na Milima ya Tao la Mashariki wana mpango wa kuitumia milima hiyo kwa ajili ya kuboresha shughuli za kitalii.

“Wageni watakaofika juu ya kilele cha milima hii wataweza kuona kwa urahisi maeneo yote ya hifadhi na uoto wake,” anasema.

Kiemi anasema kuwa mpango wa kutekeleza aina hiyo ya utalii unategemewa kufanyika katika safu ya Milima ya Malundwe (Eastern Ark), milima inayotajwa kutoka eneo la Mikumi hadi ilipo Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa.

Anataja utaratibu utakaotumika kufanya aina hiyo ya utalii kuwa ni kuweka kambi, kwamba mgeni atakapofanya utalii wa aina hiyo atatembezwa na baada ya umbali fulani anakutana na hema kwa ajili ya kupumzika hadi atakapofika kileleni mwa milima hiyo.

Kiemi anasema watajenga kambi juu ya kilele cha Milima Malundwe kwa ajili ya wageni kupata sehemu ya kupumzika na kupata chakula.

“Kule kuna misitu pia, kwa hiyo watalii watanufaika na kuona misitu iliyoko huko na kujionea mandhari nzuri ya uoto wa asili.

“Pia kule kuna mapango ya kihistoria, kwa atakayetembelea milima hiyo atapata fursa ya kujifunza mengi kuhusu mapango hayo,” anasema Kiemi.

Kwenye Hifadhi ya Mikumi pia wana mpango wa kuanzisha utalii wa puto la hewa ya joto, ‘balloon’.

Anasema kwa sasa wanahamasisha wawekezaji kuja kuwekeza kwenye utalii wa puto hilo, ‘balloon’.

 Anasema aina hiyo ya utalii itahusisha kuwasafirisha watalii ndani ya hifadhi kutoka eneo moja kwenda eneo jingine na kwamba watalii wakati wakifanya utalii wa puto hilo watapata fursa ya kuona wanyama waliomo kwenye hifadhi.

Puto litakuwa linatumia upepo unaotokana na joto la moto, na kwamba watalii watakaa sehemu maalumu katika puto hilo, halafu moto utawashwa kwenye kifaa maalumu kilichopo kwenye puto hilo ili kulifanya liweze kuelea angani likiwa na watalii.

Aina hiyo ya utalii kwa sasa inafanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, hivyo hata wao wanataka kuuanzisha katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Mbali na aina hizo, Kiemi anasema wanataka kuanzisha utalii wa kutazama nyota, ambapo anasema wakati wa kutalii usiku mgeni atapata fursa ya kutazama nyota kwa kutumia kifaa maalumu ‘telescope’.

Anaongeza kuwa kauli mbiu ya Hifadhi ya Mikumi ni ‘Wildlife at gaze’, akimaanisha kwamba ‘kuona wanyama wengi katika utupu wa macho’.

Kiemi anawahamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo ya kwenda kuona wanyama wengi katika utupu wa macho yao.

Swaumu Muhamed, mkazi wa Kitongoji cha Tambukareli kilichopo Kata ya Mikumi, analieleza Gazeti la JAMHURI kuwa hawezi kwenda kutalii katika Hifadhi ya Mikumi kwa sababu kila anapopata nafasi ya kusafiri kwenda Morogoro huwa anawaona wanyama.

“Sioni umuhimu wa kwenda ndani kutalii, kwani kufanya hivyo nitakuwa napoteza fedha zangu, kwa sababu karibu wanyama wote nilikwisha kuwaona wakati nikipita na basi,” anasema Muhamed.

Naye, Raymond Chamonza, mkazi wa Kijiji cha Kikwalaza, kata ya Mikumi, anasema anatamani kuingia kwenye hifadhi kutalii lakini hana uwezo wa kumudu gharama za kukodi usafiri wa kumtembeza katika hifadhi hiyo.

Mwandishi wa Gazeti la JAMHURI alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Hifadhi ya Mikumi na kujionea kwa macho aina mbalimbali za wanyama na uoto uliomo katika hifadhi hiyo.

Moja ya mambo ambayo mwandishi wa makala hii ameyashuhudia ni fahari ya Hifadhi ya Mikuni, ni eneo ulipo mbuyu mkubwa unaokadiriwa kuwa na miaka zaidi ya 400.

Mbuyu huo unatembelewa na wageni wengi ambao hufika pale kwa ajili ya kuona aina mbili za miti iliyoota kwa kubanana na shina la mbuyu huo. Miti hiyo ni ile ya ukwaju na aina nyingine ya mti ambao jina lake halikufahamika haraka.

Nickson Mungure, ni dereva anayefanya kazi ya kutembeza watalii katika hifadhi hiyo, analieleza JAMHURI kuwa mbuyu huo umekuwa kivutio kwa sababu watu hushangaa inawezekanaje mti wa mbuyu kukaa na miti ya aina nyingine.

“Mizizi ya mbuyu ina sumu kwa mimea mingine, ulipo hakuna mmea unaweza kuota, lakini maajabu huu umeruhusu miti mingine kuota,” anasema Mungure.

Katika Hifadhi hiyo ya Mikumi kuna bwawa la viboko, huku ndege mbalimbali wakiwa juu ya miti iliyo karibu na bwawa hilo, na kuelezwa kuwa Hifadhi ya Mikumi ina zaidi ya aina 300 za ndege.

Ikumbukwe kuwa katika Hifadhi ya Mikumi kuna barabara ya kimataifa inayounganisha nchi ya Tanzania na nchi za Zambia na Malawi (Tanzam), imekatiza katikati ya hifadhi hiyo na kuigawa katika pande mbili ambazo ni upande wa kusini na kaskazini.

Hivyo, Kiemi anaeleza kuwa uwepo wa barabara hiyo imekuwa kikwazo cha kuingiza mapato ya kutosha yatokanayo na watalii wengi kutembelea hifadhi hiyo.

Anasema ili kuhakikisha rasilimali hiyo inawanufaisha watu wengi, wasafiri wanaotumia barabara hiyo wanatakiwa kutozwa kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kupita katika hifadhi kama njia ya kuinua sekta ya utalii katika Hifadhi ya Mikumi.

1237 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!