Mimba za utotoni tishio Tarime/Rorya

Mimba za utotoni sasa zimekuwa tishio wilayani Tarime, mkoani Mara. Taarifa rasmi zinaonyesha kwamba katika kipindi cha Juni hadi Agosti mwaka huu wanafunzi 51 wanatajwa kupata mimba na kuathiri masomo yao.

Akisoma taarifa ya wilaya hiyo, Kaimu Mkurugenzi, Silvanus Gwiboha, amesema kuanzia kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti mwaka huu jumla ya wasichana 51 wamepewa ujauzito na tayari taarifa zao ziko kwenye vyombo vya dola.

Amesema kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia navyo vimefanyika kwa wanawake na wasichana 40, ambapo wanawake ni 16 na waliobaki ni wasichana wadogo, kati yao wasichana watatu wamekwisha kutoa ushahidi katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime kuhusu mashauri ya ubakaji.

Wakati Tarime ikihangaika na kupunguza tatizo hilo, hali ni mbaya wilayani Rorya, ambako wasichana 68 walitajwa kupata mimba hivi karibuni na kukatisha masomo yao.

Diwani wa Viti Maalumu, Anna Daaje, ameomba madiwani kupewa usafiri wa kuzunguka katika shule za msingi na sekondari kutoa elimu na kubaini chanzo cha mimba hizo ambazo idadi yake inaongezeka kila siku.

Amesema katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wasichana 68 wamekatishwa masomo yao, hivyo kufifisha ndoto zao.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Charles Chacha, amesema kutokana na tatizo hilo kuwa kubwa madiwani wanatakiwa kujitolea na kuwa msitari wa mbele kufuatilia katika shule na kubaini chanzo na si kutegemea kupewa usafiri.

Mwanafunzi mmoja wa Shule ya Sekondari Mogabiri ambaye hakupenda jina lake litajwe, amesema wazazi wamejisahau na hawana muda nao, hali inayosababisha kukosa vitu vyao vya muhimu kama vile taulo za kike na mahitaji megine muhimu na kujikuta wametumbukia mikononi mwa wanaume.

Ameongeza kuwa ukosefu wa chakula shuleni pia ni chanzo cha tatizo la mimba kwa wanafunzi wa kike, kwa sababu  wanapotamanishwa kununuliwa chipsi hawawezi kukataa wakati wana njaa na hapo huwa mwanzo wa matatizo.