Bunge Maalum la Katiba limeahirisha vikao vyake hadi Agosti mwaka huu, kupisha vikao vya Bunge la Bajeti vitakavyopokea na kujadili taarifa za mapato na matumizi ya Serikali ya Muungano kwa mwaka 2014/2015.

Bunge hilo kabla ya kuahirishwa Aprili 25, mwaka huu kwa takriban miezi miwili, yaani tangu Februari 18, mwaka huu wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba walikuwa katika vikao vizito, wakifanya mambo makuu mawili. Watanzania tumeshuhudia.

Kwanza walifanya kazi tuliyowatuma ya kujadili na kuweka mustakabali wa kupata mapendekezo ya Katiba mpya ya nchi yetu.

Pili, walifanya kazi ambayo hatukuwatuma kama vile kudharauliana na kutusi baadhi ya watu, viongozi na wananchi.

Kazi hii ya pili ya kukashifu, kudharau, kutusi na kuendeleza misuto na mipasho miongoni mwao na dhidi ya watu wengine, ukweli Watanzania hatukupendezwa nayo. Aidha, tumesikitishwa na kauli za kupuuzwa viongozi na waasisi wa Taifa letu.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye ni mwasisi wa Taifa la Watanganyika, Sheikh Abeid Amani Karume ambaye ni mwasisi wa Taifa la Wazanzibari na hatimaye wote wawili kuwa waasisi wa Taifa la Watanzania kuonekana bure aghali.

Waliofanya udhalilishaji huo kwa waasisi wetu ni wenzetu tuliowaamini na kuwatuma, vijana wetu ambao miongoni mwao ni wajukuu wa waasisi hao. Ama kweli, wahenga walisema tenda wema uende zako usingoje shukurani!

Tenda wema uende zako usingoje shukurani. Binadamu hawana wema ni maneno mazito na yenye busara na falsafa ndani yake. Ukipima maneno haya na ukiangalia vituko vilivyofanywa kule bungeni hutaacha kulia.

Joseph Sinde Warioba aliyepata kuwa Mwanasheria Mkuu, Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na bado ni Jaji aliyetukuka, leo kabezwa na kuonekana eti hana jambo wala mtaji; loo salala! Hii ni laana hata mbele ya Mwenyezi Mungu.

Waasisi, viongozi na wataalamu wetu Tanzania, hawakustahiki hata chembe tuzo ya maneno makali, matusi wala dharau walizopewa na wajumbe tuliowatuma na kuwaamini kwenye Bunge Maalum la Katiba. Ukweli wamefanya fadhila za punda ni mateke!!

Chanzo cha maneno makali na kuwakosea adabu waasisi wa Taifa letu yaliyotolewa na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba ni misimamo yao ya kisiasa kuhusu muundo wa serikali mbili na wa serikali tatu.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jumuiya zake na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na jumuiya zake kila upande ni king’ang’anizi wa sera yake. Mazingira hayo yamewasukuma wajumbe na kuweka kando mjadala wa kuzungumzia sababu, faida na hasara za serikali mbili au tatu.

Cha kushangaza UKAWA wamesusa mjadala bungeni na kutoka ukumbini.  CCM nao badala ya kuendelea na mjadala wa upande mmoja wamejikita katika kuwajadili wana- UKAWA! Kulikoni? Huo siyo uungwana. Wajirekebishe.

Nadhani kuahirishwa kwa Bunge Maalum la Katiba na kupitisha Bunge la Muungano la Bajeti, kutawapa wajumbe wa CCM na UKAWA nafasi nzuri ya kuwaza, kupanga na kujenga hoja nzito zaidi ama kuwa na serikali mbili au tatu.

Ukweli, wananchi wa Tanzania hawahitaji “mipasho na mipashuo”, wanahitaji hoja za maana na adilifu ambazo zitawawezesha kupatikana kwa Katiba ya wananchi, iwe ni ya serikali mbili au tatu kwa ridhaa yao wenyewe.

Nina imani na matumaini makubwa katika Bunge Maalum la Katiba litakapokutana tena Agosti mwaka huu kwa awamu ya pili na ya mwisho, wajumbe watakuwa makini katika majadiliano kuhusu Katiba.

Sitaamini penye majaliwa kuendelea kuona na kusikia mipasho, matusi na kejeli dhidi ya waasisi, viongozi na wataalamu wa Taifa hili, wala wao wenyewe kudharauliana tena, kwani ajenda hiyo haina muamala kwa Watanzania.

Mungu ibariki Tanzania, wabariki viongozi wake — wake kwa waume na watoto, Mungu ibariki Tanzania na watu wake.

1301 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!