‘Mmasai wa kwanza kupiga dansi’ (3)

Wimbo mwingine uliotia fora wakati huo ni ‘Bide’, alitunga na kuimba kwa lugha ya Kipogoro.

Juma Ubao aliamua kupumzika mambo ya muziki kwa kipindi kifupi.

Atumia muda huo wa mapumziko kwenda kusoma  masomo ya jioni akiwa na lengo la kuendeleza elimu yake.

Alisoma masomo ya Uhasibu na Biashara ambako aliweza kupata cheti.

Cheti chake kilimpa nafasi ya kupata ajira katika Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), kama mhasibu katika klabu ya Jet.

Baadaye alihamishiwa kwenda Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere ambako alipewa kitengo cha kusimamia vyakula vya kwenye ndege.

Katika kitengo hicho, Ubao alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za malipo zilizokuwa zikilipwa na ATC.

Yeye aliweza kusimamia ipasavyo vyakula vyote kuandaliwa kutoka klabu ya Jet, badala ya kuvinunua katika Hoteli ya Kilimanjaro.

Shirika hilo la ATC baadaye likaanza kuyumba kiuchumi kiasi cha kulazimika kupunguza baadhi ya wafanyakazi wake mwaka 2002, miongoni mwao akiwa yeye Juma Ubao.

Demokrasia katika tasnia ya muziki ilifanya kazi yake pale mwaka 2008, ilipomchagua Juma Ubao kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA).

Alichukua nafasi hiyo baada ya Kassim Mapili aliyekuwa mwenyekiti  wa kwanza wa chama hicho, kumaliza muda wake.

Juma Ubao umekwishapewa nafasi nyingi za uongozi katika tasnia ya muziki.

Mwaka 2009, aliteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA).

Juma Ubao ni baba wa familia ya mke na watoto watano.

Alimtaja mkewe Ashanti Mwinjuma kwamba katika kipindi chote kwenye muziki, ndiye aliyekuwa akimfariji na kumpa moyo kila alipokuwa akikwama.

Watoto wake aliwataja kwa majina ya Athumani, ambaye amefuata nyayo zake, yupo nchini Austria akifanya mambo ya muziki, Laizer, Ibrahim, Aboubakar na Salma.

Nguli huyu hakuchelea kuiomba serikali kuwatambua  wanamuziki wa zamani ambao anasema walitoa mchango mkubwa kupitia tasnia ya muziki wakati wa kutafuta Uhuru, pia walishiriki katika harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na kuhamasisha maendeleo ya taifa letu.

“Kuthaminiwa kwa wanamuziki hawa si kwa kuwapa pesa pekee, la hasha, bali ni  kuwepo kwa utaratibu japo wa kuweka majina yao kwa baadhi ya mitaa, shule ama hospitali katika halmashauri za manispaa zetu  ili yawe kama vielelezo kwa vizazi vijavyo….” anasisitiza Ubao.

Juma Ubao anatolea mifano ya maeneo ya Makumbusho ambako mitaa mingi imepewa majina ya nchi za Afrika.

Mzee Ubao hakuacha kuanika mifano mingine akisema: “…ukienda Muhimbili wodi zote zimepewa majina maarufu ya Mwaisela, Sewa Haji, pia kuna shule za Sekondari ya Shaaban Robert, Benjamin Mkapa, mitaa ya Samora, Bibi Titi,  Kiyungi, Fundikira, Makamba,  Barabara ya Kawawa, Barabara ya Ali Hassan Miwnyi na sasa hivi ipo ya Mwai Kibaki. Hizi ni kumbukumbu kubwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo…”

Aidha, ameviomba vyombo vya utangazaji hususan redio, kutenga muda japo kidogo wa kupiga nyimbo zao za zamani.

Gwiji huyo wa muziki hakusita kukemea vijana wa muziki wa kizazi kipya kufanya upuuzi wa kutotaka kujifunza kupiga ala za muziki. Kwa kufanya hivyo ni kama wanacheza ‘maigizo au makida makida.’

Juma Ubao huku akikomelea msumari mwingine kwa wanamuziki wa kizazi kipya, amewaasa wasibweteke kwa sifa wanazopambwa na mashabiki wao kwani sifa na mafanikio waliyonayo, anasema si endelevu.

Juma Salim Laizer ‘Ubao’ mwaka huu ametimiza miaka 69 ya kuzaliwa kwake.

Huruma imemjaa kwa kuona jinsi vijana hao walivyopoteza mwelekeo katika muziki. ‘Wazee dawa’ Juma Ubao ameamua kutumia ujuzi wake alionao kuwafundisha muziki.

“Nipo tayari kutumia weledi wangu kuwafundisha kupiga ala za muziki na kuimba wale vijana watakaopenda…” anamalizia nguli huyo.

>>TAMATI

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu namba: 0713331200, 0736331200, 0767331200 na 0784331200.