Sifa kubwa alizonazo Aslay ni ule uwezo wa kutunga, kuimba na kurekodi nyimbo nyingi kwa kipindi kifupi.

Aslay ni msanii wa kizazi kipya ambaye tungo zake zimekuwa zikiwakuna wapenzi wa muziki huo, ndani na nje ya nchi.

Nyimbo za kijana huyo mdogo zimejikita zaidi katika mapenzi.

Majina yake kamili ni Isihaka Nassoro, alizaliwa Mei 6, 1995, akapata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Yussuf Makamba kati ya mwaka 2003 na 2009, kabla ya kuingia Sekondari ya Tandika mwaka 2010 aliposoma hadi kidato cha nne.

Nyimbo anazotunga na kuziimba haziendani na umri wake, lakini kupitia kipaji alichonacho, anafanya vitu kama hivyo.

Aslay ni msanii wa muziki wa kizazi kipya kutoka nchini Tanzania, maarufu kama ‘Dogo Aslay’.

Alianza kufahamika kuanzia mwaka 2011 baada ya kuachia ngoma yake ya ‘Nakusemea’, aliyoitoa akiwa chini ya msimamizi wake, Said Fella, maarufu kwa jina la ‘Mkubwa Fella’.

Baadaye akatoa nyimbo kadhaa kabla ya kuundwa rasmi bendi ya vijana ya Yamoto.

Bendi hiyo ya Yamoto ilidumu kuanzia 2013 hadi 2017 ilipovunjika kwa sababu mbalimbali.

Kuanzia 2017, Aslay akawa msanii wa kujitegemea bila bendi wala usimamizi wa Mkubwa Fella. Amebaki akiwa na meneja wake wa zamani Chambuso.

Aslay ametoa nyimbo nyingi mfululizo, hali ambayo imewachanganya baadhi ya watu, wakiwamo wasanii wenzake.

Akielezea kwa nini aliamua kufanya hivyo, amesema sababu kubwa ni kwamba hana nyimbo nyingi alizofanya akiwa msanii wa kujitegemea, zaidi ya zile alizokuwa na bendi ya Yamoto.

Ili asiimbe za Yamoto akiwa kwenye matamasha, ameamua kutoa nyimbo nyingi.

Baadhi ya nyimbo ni pamoja na ‘Angekuona’, ‘Usiitie Doa’; akimshirikisha Mama Khadija Kopa, ‘Muhudumu’, ‘Baby’, ‘Likizo’, ‘Pusha’, ‘Natamba’ na ‘Huna’.

Awali ilidhaniwa kuwa Mkubwa Fella ndiye hasa mmiliki wa muziki wa kizazi kipya, lakini kupitia Aslay, Chambuso amesema si lazima yeye ndiye awe meneja bora wa muziki huo.

Aslay amemtaja kaka yake, Idd, kuwa ndiye aliyegundua kipaji chake na kumkutanisha na mdau wa muziki kutoka TMK, Said Fella ‘Mkubwa’, baada ya kumuona akipenda kuimbaimba kila alipokaa. Amepata kufanya vizuri zaidi katika muziki wa dansi la kizazi kipya akiwa na kundi la Yamoto Band.

Yamoto Band

Ndani ya kituo cha Mkubwa na Wanawe, Aslay alipokelewa na kunolewa kikamilifu na baadhi ya wakali aliowakuta, wakiwamo Yusuph Chambusso na Fella mwenyewe.

Mwaka 2011 akishiriki onyesho la Nchi za Majahazi, maarufu kama (ZIFF) aliweza kulitendea haki ipasavyo onyesho hilo kwa kuimba kibao ‘Zuwena’, ambacho ni cha marehemu Marijani Rajabu ‘Jabali la Muziki’.

Mwaka huo huo, 2011 akachomoka na ngoma yake ya kwanza, iliyotokea kutikisa vilivyo na kuteka nafsi za wengi, hususan watoto na wanawake, inayokwenda kwa jina la ‘Nakusemea’.

Mwaka uliofuata, 2012 Aslay alirekodi kibao ‘Umbea’ alichomshirikisha Chegge Chigunda kabla ya kuachia kete nyingine tena iliyojulikana ‘Bado Mdogo’.

Baada ya kushuka na kupanda huko, ndipo mwishoni mwa mwaka 2013, lilipoundwa kundi la Yamoto Band kwa kushirikisha pia vijana wengine watatu ambao ni Beka, Maromboso na Enock Bella.

“Changamoto kubwa tunayoipata ndani ya Yamoto Band ni kupendwa na kuchukiwa, kwa sababu tumetokea kukubalika ghafla, basi wapo wanaotupenda na wengine kutuonea kijicho,” amesema Aslay katika mahojiano maalumu.

Malengo ya baadaye ya Dogo Aslay ambaye hakutarajia kama atafanikiwa kwa kiwango hicho katika muziki, ni kumiliki kituo chake mwenyewe cha kuibua na kukuza vipaji vya wasanii, kama ilivyo kwa bosi wake, Fella.

Aslay anayevutiwa na Banana Zorro katika muziki, amesema kwamba alipitia madrasa Aswabirina, Temeke, jijini Dar es Salaam na hiyo ndiyo siri yake ya kupenda muziki.

Kukosa ushirikiano kwa baadhi ya wasanii wa muziki na hali ya kuibuka kwa bifu ni kati ya mambo yanayomkera nyota  huyo mpya asiyependa majivuno.

Aslay amekuwa akipakua nyimbo nyingi kila baada ya kipindi kifupi, kitendo kinachowachanganya wasanii wenzake. Baadhi ya nyimbo hizo za Aslay ni pamoja na ‘Natiririka’, ‘Natamba’, ‘Nibebe’, ‘Kwa Raha’, ‘Nasubiri Nini’, ‘Ananikomoa’, ‘Kaitesi’, ‘Ndoa’, ‘Unanitekenya’, ‘Kwalu’, ‘Totoa’, ‘Hakuna’ na hivi karibumi amepakua wimbo mpya unaoitwa ‘Kwa Watu’.

Kupitia safu hii nakutakia kila la heri ili uweze kufikia malengo yako uliyojipangia ili mradi ‘usilewe sifa’ zitakuponza.

Mwandishi wa makala hii anaptikana kwa namba 0784331200, 0767331200, 0736331200 na 0713331200.

Please follow and like us:
Pin Share