Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amesema uchaguzi utafanyika
kama ilivyopangwa tarehe 30 mwezi Julai, ingawa kulitokea alichokiita jaribio
la kukatiza uhai wake lililotokea siku ya Jumamosi.
Katika hatua nyingine, msemaji wa Polisi, Charity Charamba amevitaka
vyombo vya habari na Umma kujitokeza iwapo wana picha za video za tukio la
mlipuko wakati huu ambapo uchunguzi unafanyika.
Amwewaambia wanahabari mjini Harare kuwa zawadi nono itatolewa kwa
taarifa itakayotolewa kusaidia kwenye uchunguzi wao.Idadi ya waliojeruhiwa
sasa imefika 49 na Polisi na idara za usalama ziko katika uwanja wa White
City eneo ambalo mlipuko ulitokea.
Watu walijeruhiwa kutokana na mlipuko uliotokea kwenye mkutano wa
hadhara mjini Bulawayo, tukio lililotokea karibu kabisa na Mnangagwa wakati
akiondoka jukwaani. Maafisa wamesema masuala ya usalama yataangaliwa
tena.
mchakato wa uchaguzi unaotarajiwa ni wa kwanza tangu aliyekuwa Rais wa
nchi hiyo Robert Mugabe kuondolewa madarakani na kurithiwa na
Mnangagwa.
Mnangagwa alisema kuwa mlipuko ulitokea baada ya kitu ''kulipuka hatua
chache na nilipokuwa-lakini muda wangu haujafika''. amesema kuwa ghasia
hazina maana na ametoa wito wa kuwepo umoja.
Kiongozi wa upinzani, Nelson Chamisa pia amekemea shambulio hilo,akisema
kuwa machafuko ya kisiasa ''hayakubaliki''.
Waliojeruhiwa kwenye shambulio hilo ni pamoja na makamu wa rais wawili,
Mwenyekiti wa Chama cha Zanu-PF, wanahabari wa Televisheni ya taifa na
maafisa wa usalama.
Rais wa nchi hiyo alikuwa mjini Bulawayo, mji wa pili wa nchini humo na
ngome ya upinzani, kwa ajili ya kufanya kampeni kwa ajili ya chama chake cha
Zanu-PF wakelekea kwenye uchaguzi wa mwezi Julai.

By Jamhuri