NA BASHIR YAKUB
Umemuuzia mtu kiwanja au nyumba. Mmeandika mkataba na kuusaini tena
mbele ya mwanasheria. Kwenye mkataba mmeweka vipengele vingi lakini
kimojawapo kinahusu umaliziaji wa pesa ya manunuzi.
Hii ni kwa sababu mnunuzi amelipa kiasi kidogo na kiasi kingine ameahidi kwenye
mkataba kukimalizia baada ya muda fulani.
Mkataba umesainiwa na umekamilika. Muda umekwenda na kufika ule ambao
mnunuzi alitakiwa kumalizia kiasi kilichobaki, lakini bado haoneshi dalili za
kumalizia kiasi hicho.
Umejaribu kumkumbusha mara kadhaa lakini maneno yake ni yaleyale na pesa
halipi. Muda mlioahidiana sasa umepita lakini bado mnunuzi hajamalizia hela. Na
pengine sasa hapokei hata simu au hujui aliko au anatoa majibu ya dharau au
yasiyoridhisha au vinginevyo.
Nini ufanye katika mazingira kama haya, zipi haki zako, ipi hadhi ya mkataba
wenu wa mauziano ambao uliusaini n.k. Tutaona hapa chini.
1. Kuhusu kuuziana na kubaki na deni
Sheria haikatazi kuuziana ardhi na likabaki deni. Suala hilo limeachwa katika hiari
ya muuzaji na mnunuzi. Ni wao watakaoamua kuhusu kulipa hela yote au kulipa
kiasi na kubaki na deni.
Kifungu cha 10 cha Sheria ya Mikataba kimesema mkataba ni halali ikiwa
umefanywa na wahusika timamu/kamili, huku wakiuziana kitu halali, na kwa
masharti halali ya kisheria. Basi madhali haya yametimia jambo la kubaki na deni
halikatazwi kisheria.
2. Kushindwa kumaliza deni
Kushindwa kumalizia deni ndani ya muda ambao umeainishwa ndani ya mkataba
kwa ufupi ni kuvunja mkataba. Unapovunja sharti katika mkataba ni umevunja
mkataba. Basi kwa mazingira ya namna hii mnunuzi anakuwa amevunja mkataba.
Kifungu cha 39 cha Sheria ya Mikataba kinasema kuwa kushindwa kutekeleza
yale yaliyokubaliwa katika mkataba ndiyo kufa kwa mkataba.
Kwa hiyo, ni vyema mnunuzi ambaye hajamaliza ahadi yake ya kimkataba
kufahamu kuwa amevunja mkataba na hivyo ameua mkataba.
3.Nini ufanye ikiwa pesa haijamalizwa
Ikiwa muda umepita na mnunuzi hajamalizia hela, basi kifungu cha 73 cha sura ya

113 sheria Namba 4 ya Ardhi kimekupatia majibu kuwa unaweza kufanya haya;-
(a) Unaweza kurejea katika umiliki kwa amani bila kupitia/kutumia
mamlaka/taasisi yoyote (resume into possession peaceably).
Utakachotakiwa kufanya ni kumpa taarifa ya maandishi mnunuzi kuwa
kwa kuwa ameshindwa kutekeleza ahadi iliyo kwenye mkataba, basi
narejea tena katika umiliki wa shamba, kiwanja, au nyumba yako. Na
utarejea kweli.
(b) Kurejea katika umiliki kwa kuitumia Mahakama. Hapo juu unarejea
katika umiliki bila kuihusisha Mahakama wakati hapa unaitumia
Mahakama kurejea katika umiliki.
Njia hii ya pili unaweza kuitumia pengine kwa kuwa mnunuzi
ameshaanza kulitumia eneo na hivyo ukaona ni vigumu kurejea katika
umiliki bila nguvu ya sheria, au namna nyingine ambayo unaona ni
vigumu kuurejea umiliki kwa amani.

(c) Unaweza kufungua shauri la madai ya hela ya kiasi kilichobaki. Hapa unaamua
kutorejea katika umiliki lakini unachotaka ni kiasi kilichobaki tu umaliziwe na
mambo yaishe. Njia hii haipo kwenye sheria ya ardhi bali sheria ya mikataba na
katika madai ya kawaida.
(d) Unaweza kumtafuta msuluhishi (mediator) kumaliza tofauti zenu. Msuluhishi
anaweza kuwa yule aliyetajwa katika mkataba wenu au yeyote ambaye hakutajwa
ambaye mtamridhia asuluhishe.
Wakili, hakimu au jaji anaweza kuwa msuluhishi mzuri kwa kumtumia kama mtu tu
wa kawaida bila kutumia utaratibu wa kawaida wa kufungua kesi.
(e) Unaweza kusamehe deni kwa maandishi ikiwa utaona inafaa kufanya hivyo.
Haikatazwi kusamehe deni.
4. Fidia
Ikiwa utaamua kutumia njia yoyote hapo juu, unaweza pia kudai fidia kama
nyongeza ya hicho unachodai, kifungu cha 73(2) cha Sheria ya Ardhi kimesema
hivyo. Fidia ni kwa sababu huyu amevunja mkataba, fidia ni nyongeza tu wala
haipunguzi kile unachodai.
Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, kampuni, ndoa nk, tembelea SHERIA
YAKUB BLOG.

1499 Total Views 4 Views Today
||||| 1 Unlike! |||||
Sambaza!