NA MOSHY KIYUNGI
Tabora
Sifa za mwanamuziki Fally Ipupa zimeenea kila pembe kuliko na wapenzi wa
muziki wa dansi. Yeye pamoja na mwenzake, Ferre Golla; wanatajwa kuelekea
kuchukua nafasi za wanamuziki wakubwa waliomtangulia.
Hawa ni wanamziki vijana wanaotamba katika anga ya muziki Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo. Wanapishana kwa mwaka mmoja wa kuzaliwa – Ferre
Gola alizaliwa Machi 3, 1976 wakati Fally Ipupa alizaliwa Desemba 14, 1977 –
wote katika jiji la Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Jina lake kamili anaitwa Fally Ipupa Nsimba, akiwa na ndugu zake watatu
akikiwamo kaka yake anayejulikana jina la Bony Listton pamoja na dada zake
wawili – Tyna na Niclette.
Baba yake mzazi anaitwa Faustin Ebamba na mama yake anajulikana kwa majina
ya Monique Bolutuli Mbo.
Fally alianza kuvutiwa zaidi katika muziki kati ya miaka ya 1992 na 1993,
akashirikiana na wenzake akina Sankara Dekunta, Atele Kunianga, Pitshou
Luzolo kwa pamoja wakaunda kundi lao la muziki walilolipa majina ya Flash
success.
Kundi hilo lilikuwa limejikita katika mitaa yao iliyopo kwenye Manispaa ya
Bandalungwa aka Bandal, jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kundi hilo likaungana na la Fraternité Musica.
Wazazi wake hawakupenda awe mwanamuziki, walikuwa wakimuhimiza na
kumshinikiza kuendelea na shule. Wao walitaka kijana wao asomee fani ya
udaktari badala ya muziki.
Kati ya mwaka 1995 na 1996, Fally Ipupa alikwenda kujiunga na kundi la Kibinda
Nkoy, kwenye Manispaa ya Kintambo. Alipoingia kundini aliwakuta wanamuziki
wengine kama Seguin Mignon.
Wakati anaendelea kupiga muziki katika bendi hiyo, ukatokea mgawanyiko
kwenye kwenye kundi hilo.
Fally Ipupa, Seguin Mignon na wengine wakajiengua na kwenda kuunda kundi
jingine walilolipa majina ya Nouvelle Alliance. Kundi hilo ndiko Fally Ipupa
umaarufu wake wa kuimba na unenguaji ulikoimarika.
Mwaka 1997, Fally alijiunga na bendi ya Talents Latent’s, akawa kama kiongozi
wa bendi. Kwenye bendi hiyo pia walikuwapo marafiki zake ambao ni Atele

Kunianga, Pitshou Luzolo, Gentamicine Lissimo na Cellulaire Yankobo.
Mwaka 1999, Fally Ipupa akajiunga katika bendi ya Quartier Latin. Akiwa na bendi
hiyo Ipupa akatokea kupendwa sana na kiongozi wa bendi hiyo, Koffi Olomide Le
Grand Mopao Mokonzi.
Fally hajachelewa kutafutiwa hati yake ya kusafiria, akaungana na wanamuziki
wenzake kwenda hadi jijini Paris, nchini Ufaransa, kufanya onesho la Bercy.
Kwenye albamu ya Attentat ingawa Fally Ipupa alikuwa bado mpya kwenye bendi,
alichangia kwa kiasi kikubwa sana.
Koffi Olomide aliweka matumaini makubwa sana kwa Fally Ipupa, hata pale
albamu ya Force De Frappe ilipotolewa alipewa fursa ya kuimba na Mopao
kwenye wimbo wake wa Éternellement.
Wakati anatunga wimbo huo, Fally alikuwa na umri mdogo wa miaka 15. Wakati
imetolewa albamu ya Effrakata mwaka 2001, Koffi Olomide akampendelea zaidi
Fally Ipupa ikilinganishwa na wenzake.
Licha ya kuweka sauti yake kwenye nyimbo takriban zote, pia aliweka rap kwenye
wimbo wa Generation Bercy. Ipupa aliimba kwa pamoja na Koffi Olomide kwenye
wimbo wa Effervescent.
Kama hiyo haitoshi, Koffi Olomide akampa cheo cha kuwa kiongozi wa bendi
badala ya Felly Tyson ambaye ndiye iliyetakiwa apewe wadhifa huo.
Mwaka 2003, ikatolewa albamu ya Affaire D’etat, Fally Ipupa akawa mwanamuziki
pekee ambaye wimbo wake wa Ko Ko Ko Ko uliwekwa kwenye CD zote mbili za
albamu.
Kwenye albamu ya Monde Arabe iliyotolewa mwaka 2004, Fally Ipupa akapewa
kipaumbele tena. Sauti yake yasikika kwenye nyimbo zote zilizopendwa, nyimbo
(Esili na Eputsha) ni mfano tosha.
Ipupa ana talanta nyingi zikiwamo za kutunga na kuimba nyimbo, unenguaji, pia
anao uwezo mkubwa wa kurap.
Baada ya kujiona kuwa ameiva katika muziki, majina yake si ya kutambulishwa
tena, wazo la kutaka kujitegemea likajengeka kichwani mwake.
Fikra zake za mwanzoni zilikuwa apewe fursa ya kufanya muziki kivyake vyake
‘solo artist’, ndipo akaanza kununua nyimbo kutoka kwa watunzi mbalimbali.
Ipupa akijiweka mwenyewe katika kazi ya kutunga akisaidiwa na marafiki zake.
Akawa anasubiria wakati mwafaka ambao atatangaza hadharani nia yake ya
kufanya ‘solo album’ wakati huo huo akiendelea kufanya kazi katika bendi ya
Quartier Latin.
Mwaka 2005 ikatolewa Maxi-Single ya Boma Nga N’elengi, ambapo Fally Ipupa
alichangia pia kwenye matayarisho ya albamu ya Danger De Mort.
Hapo ndipo alipoamua kuifichua siri yake, akamwendea bosi wake Koffi OLomide,
akamwambia nia ya kutaka kutoa ‘solo album’ yake.

Kwa makusudi mazima jambo hilo lilipingwa vikali na Koffi Olomide. Fally Ipupa
hakuridhishwa na uamuzi wa Koffi, hali ya kupungua kutokuelewana kati yao
ikaanza.
Mvutano ukaanza kujitokeza huku wapambe wa pande zote mbili wakaingilia kati
kujaribu kupata suluhisho.
Wapambe wa Fally Ipupa wakamshauri aweke tishio la kujiondoa kwenye bendi
yake ya Quartier Latin, ikiwa ni njia mojawapo ya yeye akubali kufanya ‘solo
album’ yake.
Mwafaka ukapatikana, ombi lake likakubaliwa, baada ya kuzungumzwa kwenye
jopo la uongozi, japo wanamuziki wengi hawaridhishwi na jambo hilo hasa upande
ya waimbaji.
Baadhi ya wanamuziki waliokubali na kumpa kampani Fally Ipupa ni Modogo
Abarambwa na Montana Kamenga, ambao kwa kiasi kikubwa walichangia kwenye
albamu ya Danger de Mort.
Fally Ipupa akatangaza kwenye luninga kwamba wimbo wa Associe ndiyo
atakaouweka kwenye albamu hiyo.
Baadaye akabadili mawazo hayo, akaamua kuweka wimbo wa Pharmacien huku
wa Associe akiuweka kwenye albamu yake.
Mwaka 2006, Fally akajiunga na Lebo ya Obouo Music, iliyokuwa ikiongozwa na
David Monsoh ambaye ni raia kutoka nchi ya Cote D’Ivoire.
Pasipo kuchelewa, David akamtolea Ipupa albamu yake ya kwanza ya Droit
Chemin. Albamu hiyo ilikubalika mno na kundi la walio wengi, ikafanikiwa kupewa
Tuzo la Dhahabu baada ya mwaka mmoja tangu itolewe.
Mwaka 2009 alitoa albamu ya Arsenal Des Belles Melodies. Pia mwaka 2013
akatoa albamu ya Power Kosa Leka.
Fally Ipupa ni kiongozi na mmiliki wa Lebo ya F’Victeam, jina ambalo amelipa
bendi yake muziki ya Fally na F’Victeam. Walifanikiwa kutoa Albamu ya Libre
Parcours.
Baadhi nyimbo za Fally Ipupa ni pamoja na Eloko Oyo, Kiname, Bad Boy, Jeudi
Soir, Nidja, Mannequin na Liputa. Nyingine ni Just une danse, Na Lingui Ye,
Travelling Love, Mon Amour, Double Clinc, Esengo Sexy dance, Sopeka na
Bakandja.
Ipupa na kundi lake waliachia vibao vya Associe, Siamois, Cadenas, Orgas na
Ndoki.
Walitoka na video za Origina na Sweet Life na Love don’t care. Video ya Original
aliyoitoa Mei 5, 2014, wimbo huo umefuatiliwa na kutizamwa na watu takribani
milioni 10 kwenye You Tube.
Mwanamuziki Fally Ipupa alifunga ndoa ya asili mwaka 2000 na mkewe mwenye
majina ya Nana Ketchup Bafana. Wamebahatika kupata watoto watatu ambao ni

Marcosins,Vincenzo na Jayden. Mwanae mwingine ni Keyna, aliyemzaa na Nicky
Menga.
Fally ni msanii mwenye moyo wa kusaidia jamii kupitia shirika lake la Fally Ipupa
Foundation (FIF) ambalo hutoa misaada kwa makundi ya watu walio na hali duni
ya kimaisha, watoto, pia hupenda kuwajulia hali wagonjwa.
Ipupa ameshanyakua tuzo nyingi za kimataifa. Mwaka 2008 alipokea tuzo ya
msanii bora wa Kiume Afrika kwenye Kora Awards.
Mwaka 2013, alipewa tuzo la msanii bora wa Afrika kwenye Trace Urban Music
Awards.
Aidha, mwaka huohuo wa 2013, alipata tuzo mbili kwenye Ndule Awards, albamu
bora ya Power Kosa Leka na video bora Eke.
Julai 2014, alichukua Tuzo la Afrimma kama mwanamuziki bora wa kiume Afrika
ya Kati, jijini Dallas nchini Marekani.
Amewahi kushiriki kwenye MTV All Stars, akiambatana na wanamuziki wenye
majina makubwa akina Snoop Dogg, 2Face Idibia, Flavour na wengineo wengi.
Wakati wa uongozi wa Rais Barack Obama wa Marekani, Fally Ipupa aliwahi
kuwa mmoja wa wasanii wengine waliopokea mwaliko kutoka kwa rais huyo, ili
wapate fursa ya kushiriki kwenye kikao cha Ushirikiano na Maendeleo kati ya
Marekani na nchi za Afrika.
Ni mmoja wa wanamuziki waliotumbuiza mara mbili na kuujaza ukumbi wa kifahari
wa Zenith, uliopo katika jiji la Paris nchini Ufaransa. Hiyo ilikuwa kati ya Januari 2,
2010, kwa mara ya pili Ilikuwa Machi 12, 2011.
Ikumbukwe kwamba mwanamuziki huyo kijana Fally Ipupa, aliwahi kufika nchini
Tanzania, akafanya maonesho kadhaa katika jiji la Dar es Salaam mwaka 2009.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0713 331200, 0767 331200 na
0784 331200.

By Jamhuri