DODOMA.

EDITHA MAJURA.

Ufisadi kwenye Miradi ya Maji

Madai ya baadhi ya watendaji wasiyo waadilifu kushirikiana na wakandarasi, kuiba fedha zinazoidhinishwa na Bunge na kutolewa na serikali kwa ajili ya kujenga miradi ya maji, ni miongoni mwa hoja zilizounganisha wabunge wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Wakati wengine wakitaka iundwe Kamati Maalumu ya Bunge kuchunguza tuhuma hizo, wengine wameshauri kazi hiyo ipewe Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) huku wengine wakitaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi maalumu kwenye miradi yote ya maji.

Lakini Mbunge wa kuteuliwa, Abdallah Bulembo, akasema anaamini hakuna mbunge anayetilia shaka uwezo wa  serikali ya awamu ya tano katika kushughulikia mafisadi, akashauri wasiunde kamati ya Bunge na badala yake viachiwe vyombo vya dola vifanye uchunguziu.

“Hata tukiamua kuunda kamati, kweli itafanya kazi lakini mwisho wa siku taarifa na maamuzi yote ya Bunge yatatakiwa kuishia mikononi mwa vyombo vya dola, na hatimaye mahakamani kwa wale watakaopatikana na kesi za kujibu,” ameshauri Bulembo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni mstaafu George Mkuchika, ameliambia Bunge kuwa kwa wakati huu hakuna sababu za kuunda kamati ya bunge kwani serikali ipo katika hatua tofauti za kushughulikia kila aliyehusika na mambo ambayo yamesababisha kukwama kwa miradi ya maji nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, amewaomba  wabunge kuwa wapole katika suala hilo ili serikali ikamilishe kazi dhidi ya wanaotuhumiwa kufanya uhalifu kwenye miradi ya maji.

“Labda niwaarifu tu, katika kushughulikia figisu hizi tunachukua hatua za kitumishi na kisheria, kitumishi wapo ambao wameishachukuliwa hatua na hata baadhi ya wakandarasi wamepokonywa hati zao za kusafiria, kinachofanyika sasa tunatafuta ushahidi ili tuwafikishe mahakamani,” amesema Mwigulu.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Aloyce Kamwelwe, ameungana na wabunge kwamba hakuna ubishi kuwa fedha nyingi zimetolewa na serikali na kuingizwa kwenye miradi ya maji ambayo mingi haitoi maji.

“Wizara yangu imeshaunda kamati maalumu inayoongozwa na Profesa Tolly Mbwete wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM)  hivyo naomba wabunge mkubali kuidhinisha bajeti hii mkiwa na imani na sisi kwamba serikali yenu haijalala, inawatumikia wananchi usiku na mchana,” amesema Mhandisi Kamwelwe.

Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Bunda mjini, Ester Bulaya (Chadema), ametaja mradi wa maji Bunda, kuwa kuna watu wakishirikiana na watoto wa vigogo walishaugeuza kichaka cha kulia fedha za serikali ambazo ni kodi za wananchi.

Amesema hata vituo vilivyojengwa vya Nyasura, Bariri msikitini, Bariri stoo na Kunzugu ni kinyume cha makubaliano, ilikuwa vituo vijengwe kuanzia chanzo cha maji Nyabehu, lakini Mamlaka ya Maji Bunda ikajenga kituo kimoja tu cha Nyabehu, huku chanzo cha kituo cha Tairo kikiwa cha zamani siyo cha mradi mpya.

“Kwa takriban miaka Nane tunazungumzia chujio, kuna habari nimepata kwamba huko wizarani kwako, either (ama) mmepigwa au ilikuwa mpigwe, chujio la sh. bilioni 3 mliambiwa lijengwa kwa sh. bilioni 12 hatuhitaji Mkoa wa Bunda kugeuzwa vichaka vya wezi,” amesema Bulaya.

Mbunge wa Nachingwea, Hassan Masala (CCM), ametaja mradi mkubwa wa maji uliyopo eneo la Mnero Miembeni kwamba mkandarasi aliyeujenga ameweka umeme jua (solar) zisizo na uwezo wa kusukuma maji.

“Mradi ni mkubwa wenye uwezo wa kuhudumia vijiji sita na umeshatumia zaidi ya milioni 150, lakini mpaka sasa haujaanza kutoa maji huku mkandarasi akionekana kama vile ameshamaliza kazi, tunaomba uchunguzi ufanyike ili ifahamike kuna nini kinaendelea,” amesema Masala.

By Jamhuri