Wakati ikiwa imebaki takribani miezi mitatu tu kabla ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumpata mgombea wake kwa nafasi ya urais, mnyukano baina ya makada hao umezidi kupamba moto, JAMHURI imebaini.
Uchaguzi Mkuu unatarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu ambao tayari makada wamejipanga kumrithi Rais Jakaya Kikwete anayemaliza ngwe yake ya pili na kutimiza miaka 10 ya utawala.


 Wakati kila mgombea mtarajiwa akijinadi kivyake, wapambe au mashabiki wa wagombea hao nao wameongeza kasi ya kujipambanua, japo kimyakimya kuhusu ni nani au akina nani wanaowaona wanafaa kuiongoza nchi baada ya Rais Kikwete. Uchunguzi wa JAMHURI uliofanyika miongoni mwa wabunge bungeni mjini Dodoma kunakofanyika vikao vya Bunge kwa sasa, umebaini kwamba kumetokea mabadiliko makubwa kuhusu hadhi na umaarufu wa wagombea watarajiwa kwenye kipindi cha kati ya Novemba, mwaka jana hadi Machi, 2015.


 Uchunguzi umebaini kwamba baadhi ya majina makubwa ya vigogo wanaojinadi kumrithi Rais Kikwete, yameporomoka kwa kasi ya ajabu kiasi kwamba hata wabunge hawaelewi kilichowatokea vigogo hao.
Wabunge kadhaa waliozungumza na gazeti hili wameonesha woga wa kujadili majina kwa uwazi kutokana na kile kinachoonekana wanaweza kujiharibia.


Ingawa wabunge hao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini, matokeo ya hojaji hizo yanaonesha kwamba Mbunge wa Monduli na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ndiye anayeongoza kwa kutajwa zaidi, akifuatiwa na Mbunge wa Sengerema na aliyewahi kuwa waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Wengine wanaotajwa ni Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda, mawaziri Steven Wasira, Bernard Membe, Profesa Mark Mwandosya, John Magufuli, Samuel Sitta, Dk. Harrison Mwakyembe, Dk. Asha-Rose Migiro, Dk. Hussein Mwinyi pamoja na Mjumbe wa NEC, Dk. Emmanuel Nchimbi.


Zipo hisia miongoni mwa wabunge kwamba mambo yaliyosababisha  kuporomoka kwa baadhi ya majina makubwa yaliyokuwa yanatamba kabla ya Novemba 2014, ni sakata la akaunti ya escrow lililowagusa baadhi ya vigogo na namna baadhi ya vigogo hao walivyolishughulikia sakata hilo.
Pamoja na kwamba sakata la escrow limesababisha baadhi ya vigogo kuwajibishwa kwa namna mbalimbali, lakini kuna baadhi ya wabunge wanaona sakata hilo halikuwatendea haki baadhi ya waathirika wa sakata hilo.


Kundi hili la wabunge wenye mtizamo huu, linadai kubaini kwamba sakata la escrow kwa kiasi fulani lilipangwa kutumika kudhoofisha nguvu za baadhi ya wagombea urais watarajiwa kwa upande mmoja, huku likiwajenga baadhi ya wagombea kwa upande mwingine.
Wabunge wenye mtazamo huo sasa wamebaini kwamba haikuwa bahati mbaya kwa Bunge kutumiwa kushambulia miamala iliyofanywa na James Rugemalira tu kupitia Benki ya Mkombozi na kutochukua hatua madhubuti za kuwawajibisha wale wote waliochukua fedha kiasi cha Sh. bilioni 73. 5.


Fedha hizo zilitoka Kampuni ya PAP ya Harbinder Singh Sethi kupitia Benki ya Stanbic ambako Kamati ya Bunge ya PAC ilisema watuhumiwa hao walichukua fedha hizo kwa kutumia viroba, visafleti, visandarusi, matoroli, magunia, lumbesa na kadhalika.
Kwa kadri siku zinavyokwenda, wabunge hao wanazidi kung’amua kwamba baadhi ya wagombea na wapambe wao walilitumia sakata la escrow kujiimarisha na kuwaumiza mahasimu wao, kitu ambacho wabunge wengi sasa wanaona haikuwa haki.


“Ilipaswa wote walionufaika na miamala ya benki zote mbili za Stanbic na Mkombozi watajwe na washughulikiwe kwa kiwango sawa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi,” anasema mbunge mmoja kutoka Mkoa wa Ruvuma.
Anasema upendeleo huu uliotumika kushughulikia suala la escrow ndiyo sasa unaozaa huruma kwa wale waliokandamizwa kinyume na taratibu na kujenga chuki dhidi ya wale waliotumia mbinu chafu kuwakandamiza wenzao.


Aidha, gazeti hili limebaini kutoka viunga vya Bunge kwamba jambo  jiingine lililosababisha kuporomoka kwa baadhi ya majina ya vigogo waliomo kwenye kinyang’anyiro cha urais ni kutumia wapambe wasioaminika kwa walengwa.
Wabunge waliozungumzia hoja hii wanatanabahisha kwamba baadhi ya wagombea wanatumia wapambe ambao hawaaminiki katika jamii.


“Hawa ni wapambe wanaojulikana kujali maslahi yao binafsi zaidi kuliko ya umma, ni wapambe wanaopita huku na kule kuomba na kukusanya fedha kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali hususan jijini Dar es Salaam na Zanzibar, kwa kisingizio kwamba wametumwa na wagombea wanaowanadi,” anasema mbunge mwingine wa Dar es Salaam.
Anasisitiza, kwa kuwatumia wapambe wa namna hiyo wabunge wengi wameanza kupoteza imani kwa wagombea wanaowatumia wapambe hao nuksi.

 

2186 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!