Tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini na tajiri kijana barani Afrika, Mohamed Dewji, maarufu kama Mo, limewaumbua watekaji, haijapata kutokea.

Wakati wakidhani Mo hakuwa na mlinzi, na baada ya kuvua saa na kuacha simu katika eneo la Colosseum Hotel, Dar walipomtekea, hivyo wakidhani hana mawasiliano yoyote, kumbe alikuwa na kifaa maalumu kilichomo mwilini mwake kinachorekodi kila walichofanya watekaji, JAMHURI limeambiwa.

“Kwa kweli Mo alifanya uwekezaji wa maana kuwekewa ‘microchip’ mwilini mwake. Wakati anaweka kifaa hicho miaka 10 iliyopita, hakujua kuwa kitakuwa na faida kwa kiwango hiki, ila kifaa hiki kimemwokoa, kwani kimerekodi mazungumzo yote na wakati mwingine kupiga picha baadhi ya maeneo alikowekwa kulingana na positioning.

“Kifaa hiki kinaingizwa sehemu yoyote ya mwili unayotaka na hakina madhara. Ni kama kitendanishi cha mimba. Kinaungwa kwenye satellite, kisha kulingana na kiasi ulicholipa, kinakuwa na uwezo wa kutuma sauti, picha, kinaeleza hali yako kiafya, joto la mwili wako, aina ya ugonjwa ulionao au kama ugonjwa umeanza na katika mazingira ya utekaji kama haya, kinakusaidia kufahamisha mitambo kilipounganishwa uko wapi na unafanyiwa tukio lipi,” kimesema chanzo chetu kutoka London na kuongeza:

“Kimsingi hapo Tanzania wapo matajiri zaidi ya 35 ninaofahamu kuwa wamefungwa kifaa hicho. Zilipoanza vurugu za ugaidi na utekaji mwanzoni mwa miaka ya 2000 matajiri wengi Afrika walianza kujilinda kidijitali na hii ni salama zaidi kuliko kulindwa hata na mtu mwenye bunduki, maana anaweza kukugeuka yeye,” ameongeza mtoa habari wetu.

Chanzo hiki kimelieleza JAMHURI kuwa taarifa zilizorekodiwa zipo London – Uingerea, New York – Marekani na Johannesburg – Afrika Kusini katika mitambo ya kuhifadhia kumbukumbu (servers).

Mtaalamu wa mawimbi ya satellite aliyepo nchini Afrika Kusini ameliambia JAMHURI kuwa teknolojia ya ‘microchip’ inatumia satellite badala ya GPS (Global Positioning System), kuepusha aliye na microchip asipoteze mawasiliano muda wote. “GPS ukiwa sehemu isiyo na internet inapotea, lakini satellite hata ukitumbukia majini inaendelea kuona,” amesema mtaalamu huyo.

Kifaa hicho ni kidogo sawa na punje ya mchele na kinaingizwa mwilini kwa kutumia bomba la sindano. Kimehifadhiwa ndani ya plastiki na kina uwezo wa kuhifadhi kumbukumbu miaka milioni moja. Kifaa hiki kinachoitwa kwa kifupi RFID kinampa aliyekiweka namba ya utambuzi, kinatunza kumbukumbu zake na mawasiliano yake anayofanya kwa muda wote wa maisha yake.

Baadhi ya kampuni zinazotoa huduma hii zinampa mhusika fursa ya kuchagua watu watatu wa kupata taarifa zake iwapo litamtokea jambo lolote lisilo la kawaida, iwe la kiusalama au vinginevyo.

Teknolojia ya ‘microchip’ hapa nchini imekuwa ikitumika kulinda wanyama walioko katika hatari ya kutoweka wakiwamo faru, ambao kimsingi walikuwa wanawindwa na majangili kwa kiasi cha kutisha.

JAMHURI limekwenda nyumbani kwa Mo kupata ufafanuzi wa taarifa hizi kuwa ana microchip iliyorekodi taarifa zake zote, ila walinzi wakawaambia waandishi wetu: “Tumeambiwa hakuna mwandishi anayeruhusiwa kuingia ndani.”

Hata hivyo, JAMHURI limezungumza na baba mzazi wa Mo, Gullam Dewji na kumweleza kuwa Mo anayo microchip iliyorekodi tukio lote la utekwaji wake, naye akasema: “Wewe umeambiwa na nani?… Sasa utaleta matatizo. Mo hana hiyo chip,” amesema na kukata simu.

Kutoka Afrika Kusini

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, mtaalamu wa masuala ya usalama kutoka Johannesburg, Afrika Kusini, Mpho Mandla, anasema taasisi za ulinzi na usalama nchini humo bado zimeelekeza macho na masikio yake Dar es Salaam, Tanzania.

Mandla anasema taarifa za kuhusishwa kwa raia wa Afrika Kusini, ziliwafikia kwa njia ya mitandao ya kijamii, huku shauku kubwa ikiwa ni kuwafahamu wahusika wa tukio la utekwaji wa Mo Dewji.

“Unajua Tanzania na Afrika Kusini ni nchi zenye historia ya udugu, Tanzania imesaidia sana wakati wa mapambano ya ubaguzi wa rangi hapa kwetu…ninyi mnabaki kuwa ndugu zetu sana kuliko mataifa mengine yanatotuzunguka.

“Tuliposikia kwamba kuna mfanyabiashara Mtanzania ametekwa, kwanza nilisikitika kwamba matendo ya utekaji sasa yamehamia Tanzania… siku chache baadaye tukasikia kupitia kwa ofisa mmoja wa Jeshi la Polisi kwamba waliomteka mfanyabiashara huyo walikuwa wanaongea lugha ya Kizulu,” anasema Mandla.

Mandla ambaye ni mtaalamu wa masuala ya usalama hasa kwenye forensic ameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba baada ya kusikia kuhusu raia wa Afrika Kusini kuhusishwa na tukio hilo, alitamani kusikia majina yao pamoja na kufahamu kama wako katika orodha ya wahalifu wanaotafutwa kimataifa.

Taaluma ya forensic aliyonayo Mandla, kimsingi inahusu kukusanya na kuchambua masuala yote yanayohusisha matukio yanayohusiana na jinai, ushahidi unaoshikika ili kupata suluhisho kuhusu mtuhumiwa wa uhalifu.

Katika hali kama hiyo wachunguzi huchunguza vitu kama damu, vimiminika, alama za vidole, hard drives, kompyuta pamoja na teknolojia ili kubaini namna uhalifu ulivyotendeka.

 Mandla ametoa ushauri kwamba, katika dunia ya sasa ambapo uhalifu unazidi kuongezeka kwa kasi huku ukisaidiwa na teknolojia, ni vema wananchi wakachukua tahadhari zaidi kuliko kutegemea msaada wa polisi kwa asilimia 100.

“Umefikia wakati kwa vyombo vya ulinzi na usalama barani Afrika kutoa elimu kwa wananchi wake namna ya kujilinda… maana dunia ya leo imekuwa si sehemu salama sasa. Tusisubiri majanga yatufike,” anasema Mandla.

IGP Sirro azungumza na wanahabari

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simoni Sirro, ameeleza namna mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji, alivyopatikana katika viwanja vya Gymkana usiku wa kuamkia Jumamosi, huku akiahidi kwamba ‘mchezo ndiyo kwanza umeanza.’

Amewaambia wanahabari katika mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam kuwa kazi iliyobaki ni kuwasaka ili kuwaonyesha kuwa Tanzania si mahali salama kwa wahalifu.

“Unapoanza mbio lazima zifike mwisho, watakapokwenda na sisi tutakwenda, hatuwezi kuwaachia, tukiwaacha watajipanga upya,” anasema IGP Sirro.

Kuhusu namna alivyopatikana Mo, IGP Sirro anasema saa 8:30 usiku, gari lililombeba mfanyabiashara huyo bilionea, lilimshusha katika eneo hilo na wahusika walilitelekeza na kuondoka. Hata hivyo, alisema kabla ya kuondoka watekaji hao walijaribu kutaka kulichoma moto gari hilo.

“Kwa maelezo ya Mo, alimpata mlinzi mmoja akapiga simu kwa wazazi wake, baadaye polisi tukapata taarifa na kuwahi eneo la tukio. Kwenye lile tukio tuliamua kuweka utepe na kuimarisha ulinzi ili watu wasiingie hadi asubuhi ya leo (Jumamosi) ili upekuzi ufanyike,” anasema.

Amesema upekuzi ulipofanywa na timu ya askari wanaohusika na matukio, walilibaini gari hilo Toyota Surf kuwa ndilo lile lililotajwa na polisi awali kuwa lilihusika siku alipochukuliwa ambako aliwataka wasamaria wema kutoa taarifa popote watakapoliona.

“Gari ni lilelile halina mashaka. Lakini ndani ya gari tumekuta silaha nne ambazo ni AK47 moja yenye risasi 19 na bastola tatu zenye risasi 16,” anasema Sirro.

Ameeleza kuwa baada ya Mo kuhojiwa, amesema watekaji walikuwa na wasiwasi na walichokuwa wakikihitaji kwake ni fedha na yeye alichukua jukumu la kuwapa namba ya simu ya baba yake.

“Aliwaambia namba hii mkimpigia baba mtazungumza naye. Watekaji hawa walikuwa na wasiwasi, hawakutaka kuzungumza na baba yake Mo Dewji (mzee Gullam Hussein Dewji) na lugha waliyokuwa wakizungumza ni Kiingereza na Kiswahili cha kubahatisha,” anasema Sirro.

Mapema Jumamosi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alikaririwa akisema: “Kwa mujibu wa maelezo ya Mo Dewji, watekaji walisikika wakizungumza kwa lafudhi ya lugha moja ya Afrika Kusini.”

Sirro amesema upelelezi uko vizuri na aliwashukuru wakazi wa Dar es Salaam kwa ushirikiano wanaouonyesha kuhakikisha wahusika wanapatikana.

“Nawaomba sana… waendelee kutupa taarifa kwa sababu mchezo ndiyo kwanza umeanza . Tunataka kuwaonyesha kuwa Tanzania si mahali salama kwa mtu anayetaka kufanya uhalifu.

“Nafikiri lile tangazo nililolitoa na picha ilivyoonekana wakawa na wasiwasi kuwa wangekamatwa na kweli wangekamatwa, maana hawakuwa na namna, maana gari linajulikana, dereva na mmliki wake pia, kilichobakia ni kuchunguza tu wapo wapi,” anasema Sirro.

Akizungumza na wanahabari, Ijumaa ya wiki iliyopita, IGP Sirro amesema kumekuwepo na matukio ya baadhi ya watu kujitokeza na kukimbilia nchi jirani.

“Kulikuwa na shida maeneo ya Kibiti, siku za hivi karibuni tuliwakamata watu, wachache waliobaki wakakimbilia Msumbiji. Juzi tumewakamata watu 104 walikuwa wanataka kuvuka mpaka kwenda Msumbiji, mipaka yetu iko thabiti,” anasema Sirro.

IGP ametoa takwimu mwezi Machi hadi Septemba mwaka huu katika operesheni ya kupingana na matukio ya kihalifu, ambapo anasema Jeshi la Polisi lilikamata silaha 190, zikiwemo bunduki za kivita AK47-10 pamoja na risai 235 za aina mbalimbali.

Akizungumza kuhusu kutekwa kwa Mo Dewji, IGP Sirro anasema gari lililotumika kumteka Mo limegundulika baada ya kuonekana kwenye CCTV kamera, huku akiongeza kwamba maganda mawili ya risasi yamepatikana na yapo maabara kwa uchunguzi zaidi.

 Sirro ameutangazia umma wa Watanzania kwamba gari lililotumika kumteka Mo Dewji lilikuwa limetoka nchi jirani, huku akisisitiza dereva pamoja na mmiliki wa gari hilo wanafahamika. Anasema Jeshi la Polisi linashirikiana na Polisi wa Kimataifa (Interpol) kwa hatua zaidi za kiuchunguzi.

 “CCTV kamera imetusaidia, tumeweza kutambua gari lililotumika…lilielekea Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, na tumefuatilia hadi roundabout ya Kawe na tunaendelea na msako na tayari tumepata taarifa za mmiliki wa lile gari,” anasema Sirro.

“Suala la nani aje kutusaidia, sisi ndio tunajua nani aje, na tukiona kuna haja lazima tutamtaarifu Amiri Jeshi Mkuu (Rais Dk. John Magufuli) kwamba tunafikiri hapa tusaidie, lakini kwa hali tuliyonayo sidhani kama tunahitaji watu watusaidie, lazima tulinde heshima ya nchi yetu.

 “Tusidharau vitisho, mtu unapoona unatishiwa na mtu yeyote, tupe taarifa, ili tuweze kufanyia kazi mapema. Na pia wale wenye uwezo kifedha ni vema wakawa na silaha na wasaidizi wenye silaha, kwa sababu fedha walizonazo kila mtu anazitaka,” anasema IGP Sirro.

Walijaribu kuchoma moto gari

Sirro amesema wahalifu walijaribu kuchoma moto gari lililotumika kumtekea Mo Dewji.

Akizungumza na waandishi wa habari, Sirro alisema baada ya kumwachia, wahalifu walijaribu kuharibu ushahidi kwa kulichoma gari lakini ilishindikana.

“Mkienda pale eneo la tukio mtaliona hilo gari, kuna madumu ya mafuta, walijaribu kuliwasha moto, lakini ikashindikana,” alisema Sirro.

Sirro alisema wamehakiki gari hilo na kugundua kuwa gari hilo ndilo ambalo walikuwa wakilishuku kutumika katika mkasa wa kumteka Mo Dewji Oktoba 11, mwaka huu.

Zimamoto wazungumza

Kwa kuwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ndilo lenye jukumu la kushughulikia majanga yote yanayohusiana na moto nchini, JAMHURI limemtafuta Kamishna Jenerali wa Zimamoto, Thobias Andengenya, kufahamu kama Jeshi la Zimamoto limehusishwa katika sakata ya Mo kutekwa, hasa baada ya IGP Sirro kusema kuwa watekaji walijaribu kulipua gari wakashindwa. Andengenye amesema yuko nje ya mipaka ya eneo la tukio na akataka Kamishna wa Operesheni wa Zimamoto ndiye ajibu.

Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Billy Mwakatage, amesema: “Mara zote tunafanya kazi na polisi kweli, kwa matukio kama haya, lakini mara nyingi tukio lolote la arson (kuungua), huwa wao wanalichunguza, na pale ambapo wanaonekana wanataka kushirikisha taaluma ya kwetu ya moto, kama wataona inafaa kufanya hivyo, wanaweza kutushirikisha. Wanatushirikisha, lakini kwa hili hatujashirikishwa kwa kweli.”

Amesema inawezekana gari lilikataa kuungua iwapo jambo moja kati ya matatu halikuwapo. “Ili moto utokee lazima kuwepo na vitu vitatu vya msingi. Moja ni joto, pili ni oxygen, lakini hivi viwili joto na oxygen haviwezi vikalipua moto, ni mpaka kuwe na chakula cha moto, ambayo ni fuel (mafuta), kwa hiyo missing one of the items (kukosekana kwa jambo moja) lazima moto usitokee,” amesema.

Ameongeza kuwa inawezekana hilo gari walilokuwa nalo watekaji limeshindikana kuungua iwapo walifunga milango mapema oxygeni ikatoweka ndani ya gari. “Kwa hiyo, yamkini inawezekana kuna kimoja kilikuwa kinakosekana katika hivyo vitatu. Kwa hiyo hauwezi kutokea moto hata ufanyeje,” ameongeza.

CIA wachunguza

Taarifa ambazo JAMHURI limezipata ni kuwa makachero wa Marekani (CIA) wanaendelea na uchunguzi wa kutekwa kwa Mo kwa kutumia taarifa zilizopatikana kupitia hiyo microchip na wameahidi kuwachukulia hatua wanaohusika na utekaji huo.

“Walichosema ni kuwa yule mwandishi Jamal Khashoggi iwapo asingekuwa na microchip, basi angefariki dunia bila kujulikana kuwa maofisa wa Ubalozi wa Saudi Arabia wameshiriki kumuua na kumkatakata vipande kisha kuondoka navyo kuvipeleka kusikojulikana,” kimesema chanzo chetu na kuongeza kuwa hata Mo watekaji wake wamepata taarifa kuwa serikali inafuatilia tukio hili kwa nguvu zote na CIA imeanzisha uchunguzi, hivyo wakaona yatawafika makubwa kwani siri imevuja ikabidi wamwachie.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, wiki iliyopita ametoa taarifa akihoji maofisa 15 wa Saudi Arabia walikwenda kufanya nini Uturuki na kwa nini Saudi Arabia imewakamata watu 18 baada ya kifo cha Khashoggi aliyekuwa ametekwa. Baada ya hotuba hiyo, Saudi Arabia kwa mara ya kwanza imekiri kuwa mwandishi huyo alifariki dunia katika mapigano ndani ya ubalozi. Hata hivyo, hawakuonyesha mwili wake uliokatwa vipande vipande uko wapi.

Marekani ambaye ni mshirika mkubwa wa Saudi Arabia, imetishia kuliwekea vikwazo taifa hilo. Hadi sasa tayari Saudi Arabia imepoteza uwekezaji wa wastani wa dola bilioni 5 karibu Sh trilioni 14, baada ya wawekezaji na nchi za Ulaya na Amerika kuamua kuahirisha uwekezaji wao na kuondoa biashara zao nchini humo kutokana na mauaji ya Khashoggi.

Taarifa zinasema CIA watafanya kila wawezalo kupata ukweli jinsi Mo alivyotekwa na kurejeshwa kisha wahusika watachukuliwa hatua mmoja mmoja kwa kadiri alivyochangia uhalifu huo.

Mtiririko wa matukio kutekwa Mo

OKTOBA 11

Mfanyabiashara maarufu nchini, ambaye pia ni mwekezaji wa Klabu ya Simba, Mohammed Dewji (Mo Dewji) alitekwa na watu wasiojulikana waliokuwa na silaha za moto, saa 11 alfajiri wakati akiingia kufanya mazoezi katika gym ya Colosseum, Oysterbay jijini Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kinondoni, Jumanne Muliro, athibitisha tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema Polisi Dar inafuatilia madai ya kutekwa kwa mfanyabiashara huyo maarufu nchini.
Dereva wa Uber aliyekuwa amefika hotelini hapo kumchukua mteja wake alinukuliwa akisema kwamba aliona watu wanne wakishuka kwenye gari dogo, wakiwa wamejifunika usoni, wakapiga risasi moja juu na kumchukua Mohammed Dewji.
Baada ya muda, Mambosasa alisema kwamba waliomteka Mo ni Wazungu wawili na msako mkubwa unafanywa kwa raia wa kigeni wote waliopo nchini kutokana na tukio hilo. Mchana; Mambosasa alibainisha  kuwa watu watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano kuhusu kutekwa kwa Mo Dewji.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paulo Makonda alitoa onyo kali kwa yeyote atakayeibuka na kuanza kusambaza taarifa za uongo kuhusiana na tukio hili au kuligeuza na kulifanya mtaji wa kisiasa.

OKTOBA 12

Msemaji wa Klabu ya Simba, Haji Manara, alikamatwa na kuzuiliwa kwa mahojiano kuhusiana na sakata la kutekwa kwa mfadhili wa timu hiyo, Dewji.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Mambosasa alisema Manara anashikiliwa kutokana na kusambaza taarifa za tukio hilo la kutekwa kwa Mo kwenye mitandao kwa madai ya kutumwa na familia, bila kutumwa na familia hiyo.

“Hajatumwa na familia hivyo tunamshikilia,” alisema Mambosasa.

Watu 12 wanashikiliwa na jeshi hilo kutokana na tukio hilo huku uchunguzi ukiendelea.

OKTOBA 13

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, alizungumza na vyombo vya habari nchini na kubainisha kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kumtafuta mfanyabiashara huyo pamoja na watu wengine wanaodaiwa kupotea.

Alibainisha kuwa tayari watu 20 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano kuhusiana na sakata hilo ili kuweza kuwabaini wahusika. Pia alieleza kuwa amewaagiza polisi kutowashikilia zaidi ya saa 24 wale watakaobainika kutokuwa na mahusiano na tukio hilo.

OKTOBA 14

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Injinia Hamad Masauni, alisema serikali inatarajia kufunga kamera maalumu za CCTV katika miji mikubwa na baadhi ya mikoa nchini ili kukabiliana na uhalifu.

Masauni alipoulizwa uwezekano wa kuomba msaada nje ya nchi ili kufanikisha kukamata wahalifu alikataa na kusema wachunguzi wa ndani ya nchi wanatosha.

OKTOBA 15

Familia ya Mohamed Dewji ilitangaza donge nono la Sh bilioni moja kwa mtu yeyote atakayefanikisha kupatikana kwa mtoto wao huku wakiahidi kumlinda mtoa taarifa.

Familia ilitangaza namba za simu zitakazotumika kukusanya taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa Mo.

Akisoma taarifa iliyotolewa na familia, Azim Dewji, ambaye ni alijitambulisha kama msemaji wa familia akiwa ameongozana na baba mzazi wa Mo, Gulam Hussein Dewji, alisema familia inasikitishwa na tukio la utekwaji wa kijana wao na kwamba yeyote atakayetoa taarifa za upatikanaji wa kijana huyo familia itampatia kiasi hicho cha fedha.

OKTOBA 16

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema kuwa watu 19 kati ya 26 waliokuwa wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na utekaji wa Mo Dewji wameachiwa kwa dhamana akiwemo Haji Manara.

OKTOBA 19

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, aliwaambia waandishi wa habari kuwa kwa kutumia kamera za CCTV wamebaini gari lililotumika kumteka Mo Dewji.

Alisema gari hilo aina ya Toyota Surf liliingia nchini Tanzania kutoka nchi jirani ambayo hakuitaja jina Septemba Mosi, 2018, likiendeshwa na Obasanjo Zacharius Junior.

Namba za usajili wa gari hilo ni AGX 404 MC, ni gari ambalo polisi wanaamini lilitumika kumteka Mo Dewji katika Hoteli ya Colosseum Alhamisi, Oktoba 11.

Sirro amesema kwa kutumia CCTV wamebaini kwamba gari hilo aina ya Surf baada ya kutoka Hoteli ya Colosseum, lilipita barabara za Haile Sellasie, Ali Hassan Mwinyi, Maandazi, Mwai Kibaki na kisha likapotelea kwenye eneo la Mlalakuwa karibu na mzunguko wa Kawe.

“Bado watu wetu wanafuatilia kuona kama walielekea maeneo ya Silver Sands au Kawe. Hapo ndipo tunaamini gari hilo lilipotelea, tunakwenda jumba kwa jumba kutafuta,” alisema Kamanda Sirro.

Katika hatua nyingine, Kamanda Sirro amebainisha kuwa kati ya watu wanane ambao wanaendelea kuwashikilia wakati wakichunguza tukio hilo, ni kapteni wa boti. Lakini hakusema ni wa boti gani, na inayofanya safari zake maeneo gani, japo awali polisi walisema wameimarisha ulinzi wa mpaka katika Bahari ya Hindi kuzuia Mo kutoroshwa nchini.

Mpaka sasa bado hazijajulikana sababu za Mo kutekwa na nani hasa ambao wamemteka. Awali ilidaiwa kuwa Mo ametekwa na Wazungu wawili jambo ambalo IGP Sirro alikataa kukubali ama kukanusha akisema hilo ni suala la kiupelelezi zaidi.

Sirro alisema bado hawajui alipo Mo, lakini walibaini kuwa waliomteka walikuwa na bastola ambazo ni za kufyatua risasi za ukubwa wa 9mm.

OKTOBA 20

Katika ujumbe ulioandikwa kwenye ukurasa wa twitter wa Kampuni ya Mohamed Enterprise Tanzania Limited (MeTL), ulisema: “Namshukuru Mwenyezi Mungu nimerudi salama nyumbani. Nawashukuru Watanzania wenzangu na watu wote kote duniani kwa dua na sala zao. Nashukuru mamlaka zote, namshukuru Rais Magufuli, likiwemo Jeshi la Polisi, zilizofanya kazi ya kuhakikisha narudi salama.”

Ujumbe huo uliandikwa saa 09:15 alfajiri baada ya Mo Dewji kupatikana.

Alfajiri hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba:

“Mohammed Dewji amerudi salama. Nimezungumza naye kwa simu dakika 20 zilizopita. Sauti yake inaonyesha yu mzima bukheri wa afya. Shukrani kwa wote kwa dua na sala. Naenda nyumbani kwake kumuona muda huu.”

Aliandika ujumbe mwingine uliosema:

“Nimemuona na kuongea kwa kirefu na Mohammed Dewji. Ni mzima wa afya isipokuwa ana alama za kufungwa kamba mikononi na miguuni. Mnamo saa nane usiku, watekaji waliamua kumtupa kwenye maeneo ya viwanja vya Gymkana. Naamini Polisi watatoa taarifa za ziada kuhusu kilichojiri.”

Kamanda Mambosasa aliyefika nyumbani kwa Dewji kuthibitisha kurejea kwake nyumbani, alisema watu waliomteka Mo Dewji walikuwa na lafudhi ya mojawapo ya lugha za mataifa ya Afrika Kusini, kwamba hatua hiyo imethibitisha wazi hakutekwa na Watanzania.

“Nataka kuuthibitishia umma wa Tanzania kwamba nimefika nyumbani kwa kina Mo Dewji, nimeongea naye niko na kikosi cha makachero hapa na ndugu yetu ni mzima kama IGP alivyozungumza na umma kwamba Jeshi la Polisi litaendelea na uchunguzi ili kuhakikisha kwamba tunampata mhusika akiwa mzima,” anasema Mambosasa.

Wakati huohuo, gari ambalo linaaminika kutumika katika kumteka Mo, limepatikana kando ya viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam ambapo bilionea huyo aliachwa.

Hata hivyo, zamu hii lilionekana likiwa na namba za usajili wa Tanzania T 314 AXX.

Hakuna mtu aliyekamatwa, na bado haijulikani watu waliomtelekeza Mo eneo hilo walitumia usafiri gani kuondoka katika eneo la tukio. Sambamba na hilo, hakuna majibizano ya risasi baina ya watekaji na Polisi, lakini watekaji hao wametelekeza gari likiwa na silaha ya kivita aina ya AK47 na bastola tatu.

IGP Sirro amewaambia waandishi wa habari kuwa waliomteka Mo Dewji walifanya hivyo kwa lengo la kujipatia pesa.

Sirro amesema bilionea Mo aliwapa namba ya simu ya baba yake mzazi mzee Gulam ili waongee naye juu ya hilo, lakini hawakupiga simu wakihofia kunaswa na polisi.

“Mohammed Dewji amesema watekaji hao walikuwa na wasiwasi sana, walimwambia wanataka pesa, alipowauliza shilingi ngapi hawakusema. Aliwapa namba ya simu ili waongee na baba yake, lakini waliogopa kwa sababu wanafahamu ulinzi wetu ni imara na tungewakamata,” alisema IGP Sirro.

Amesema kuwa watu waliokuwa wakimshikilia Mo walikuwa watatu, wawili walikuwa wakiongea Kiingereza na mmoja akiongea Kiswahili kidogo.

Polisi nchini Tanzania wamesema watafanya kila wawezalo kuwatia nguvuni watu waliomteka na kumshikilia bilionea Mohammed Dewji, Mo, kwa siku tisa.

IGP Sirro aliwaambia waandishi wa habari kuwa kuachiwa kwa Mo ni mwanzo wa kuwanasa wahalifu hao na kuwapata wakiwa wazima au wamekufa.

“Mbio ukizianza sharti uzimalize. Huu ni mwanzo tu. Hao wahalifu wanaotaka kuchafua jina la nchi yetu lazima tuwatie nguvuni,” amesema Sirro.

Amesema upelelezi umeimarishwa kwa kushirikiana na mtandao wa Polisi wa Kimataifa (Interpol).

“Nataka niwaambie wahalifu yawezekana wananisikiliza hivi sasa kuwa popote watakapokwenda tutawanasa. Wakienda Afrika Kusini tunao, Kenya tunao, Uganda tunao hata Msumbiji, popote pale tutawakamata, maana tayari tuna ushirikiano na wenzetu,” amesema Sirro.

16508 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!