IMG_2701Mara baada ya kuwatosa kwa muda wachezaji wake, Kipre Tchetche na Aggrey Morris, timu ya soka ya Azam FC imewarejesha haraka ili kujiweka sawa kwa ajili ya kuwania Ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
 Wachezaji hao walifungiwa kucheza mechi nne baada ya kubainika kufanya kosa la kuondoka kambini bila kuaga, lakini kabla ya adhabu hiyo kufika mwisho wamerudishwa kundini.


 Katika mechi ambazo wachezaji hao hawajacheza, Azam imekuwa ikiambulia sare ikianzia ile ya 1-1 dhidi ya Mbeya City na baadaye 1-1 na Mtibwa Sugar kabla ya kutoka sare tasa na Mgambo JKT.
 Lakini kabla ya mchezo dhidi ya Kagera Sugar, uliochezwa wikiendi iliyopita, Azam waliamua kuwarejesha wachezaji hao ili kuokoa jahazi lililokuwa likizama huku Simba ikiikaribia.


 “Angalau tubaki nafasi ya pili kweli Ligi Kuu,” anasema mmoja wa viongozi wa Azam, ambaye anashangazwa na timu hiyo kufanya vibaya wakati huu Ligi ikielekea ukiongoni.
 Kiongozi huyo anasema kwamba safu ya ulinzi ilicheza hovyo katika mechi zote ilizopata sare baada ya kumkosa Aggrey Morris, ambaye anacheza vizuri na Paschal Wawa, lakini safu ya ushambuliaji pia iliyumba kwa sababu Didier Kavumbagu alikosa mtu sahihi ambaye ni Kipre Tchetche.


Mechi dhidi ya Mgambo, Kavumbagu alicheza na Gaudence Mwaikimba ambaye dhahiri ameshaisha kiuchezaji kwa sababu ya umri na kutopangwa kabisa msimu huu. Naye Wawa alicheza na Mwantika dhidi ya Mbeya City na Mtibwa Sugar, lakini waliyumba kwa sababu hayuko imara.
 Uongozi wa Azam ulitangaza kuwa Kipre na Morris ni majeruhi wakati sivyo, na mtandao huu ukawashauri kuwaponya kiaina na kuwarudisha kambini na imekuwa hivyo.

By Jamhuri