Mji wa Morogoro ni miongoni mwa miji iliyokuwa maarufu kwa michezo na burudani katika miaka ya 1950, 1960 na ya 1970.
  Watu wengi walitoka Dar es Salaam na kwenda kufanya starehe za kumaliza wiki mjini humo. Hali ya hewa na kuwapo kwa bendi mbili maarufu zilizokuwa na uwezo mkubwa, ilifanya wafanyakazi wengi watamani kupangwa kufanya kazi mjini Morogoro.


  Bendi hizo mbili zilizokuwa shindani zilikuwa ni Morogoro Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Mbaraka Mwinshehe Mwaruka na Cuban Marimba iliyokuwa ikiongozwa na Salum Abdallah Yazidu a.k.a SAY.
 Katika makala hii nitamzungumzia kiongozi huyo wa bendi ya Cuban Marimba, Salumu Abdalah Yazidu, aliyezaliwa Mei 5, 1928 mkoani humo. Baba yake alikuwa Mwarabu na mama yake alikuwa ni mwenyeji wa Mkoa wa Morogoro.


  Alisoma hadi darasa la sita pale Msamvu na akachaguliwa kuendelea na masomo Dar es Salaam. Kwa hiyo alilazimika kwenda Dar es Salaam ili kuendelea na masomo. Pamoja na kufaulu huko, baba yake aliamua abakie nyumbani kumsaidia katika shughuli za biashara.
  Katika kipindi hicho, Salum alianza kuonesha kupenda kwake muziki. Alifurahia sana santuri kutoka Cuba zilizokuwa maarufu kwa kuitwa kwa namba zake GV1, GV2, GV3 na kadhalika. Pamoja na baba yake kutokupenda aina ya muziki aliokuwa anaupenda mwanae, aliona ni heri amnunulie gramophone au  gramafoni kama ilivyokuwa ikiitwa ili apigie hizo santuri.


  Haukupita muda Salum akatoroka kwao ili aende Cuba kujifunza muziki. Alikwenda hadi Mombasa, Kenya ili apande meli kwenda Cuba. Ilikuwa mwaka 1945 wakati kulikuwa bado na vuguvugu la Vita ya Pili ya Dunia na safari yake ikaishia hapo hapo Mombasa.
 Baba yake alimrudisha Morogoro, akamfungulia mgahawa ili atulie, lakini Salum alikuwa keshapata mzuka wa muziki na akawa ameanza kuhudhuria kumbi nyingi zilizokuwa zikipiga muziki wa dansi. Alipendezwa sana na vifaa vya Dar es Salaam Jazz Band Wanamundo ‘Majini wa Bahari’ hawa.
  Wakati huo yeye na wenziwe walikuwa wameanzisha kikundi ambacho kilikuwa na vyombo vya kuchonga na ngoma za kiasili, wenyewe wakikiita bendi na kuipa jina La Paloma.


  Hilo lilikuwa jina la wimbo mmoja katika santuri za GV. Wimbo huu ni mzuri kiasi kwamba mpaka leo bado unapigwa duniani kote, hata kurekodiwa na wanamuziki mbalimbali akiwamo Elvis Presley, mwanamuziki wa Marekani, aliyeingia katika anga za muziki baadaye sana.
  La Paloma ilikuwa na viongozi kama Juma Said aliyekuwa Rais, Abubakar Hussein akawa Mweka Hazina, Ramadhan Salum alipewa nafasi ya Katibu Mkuu, Ali Waziri, Naibu Katibu Mkuu, Salum Abdallah akawa mkuu wa bendi.


  Baada ya kuviona vyombo vya muziki vya bendi ya Dar es Salaam Jazz, hamu ya kuwa na vyombo kama hivyo ilikuwa kubwa hadi kufikia Salum Abdallah kuuza kwa siri nyumba mojawapo za baba yake na kununua vyombo kama vya Dar es Salaam Jazz Band.
  Mwaka 1948 La Paloma ikawa bendi rasmi. Viongozi wake walikuwa Salum Abdallah aliyeteuliwa kuwa kiongozi, Abubakar Hussein akawa Mweka Hazina na Juma Ndehele akapata nafasi ya Katibu, wanamuziki walikuwa Kibwana Seif, Juma Kilaza, Ligongo, Mgembe, Juma Kondo, Nzige na Daulinge.
  Kundi hili mwaka 1952 likajipa jina la Cuban Marimba Jazz Band ambalo lilianza kuwa maarufu kiasi cha kwamba mwaka huohuo kampuni ya santuri ya Mzuri Records walikwenda Morogoro kurekodi nyimbo za bendi hiyo.


  Bendi ya Cuban Marimba ikiwa na nguli huyo, iliwahi kurekodi vibao vingi vikiwamo vya ‘Ngoma Iko Huku’, ‘Naumiya’, ‘Ubaya’, ‘Nalia Nalia’, ‘Wanipendeza’, ‘Cuba Chacha’ na ‘Ndiyo Hali ya Dunia’.
 Nyingine ni ‘Kazi Tanzania’, ‘Shemeji’, ‘Tanzania Twist’, ‘Sipati Majibu’, ‘Salaam Kwa Jumla’ na ‘Wanawake Tanzania’.
  Salum Abdallah hakuishia hapo, alitoka pia na vibao vingine vya ‘Kachacha’, ‘Tulime Mashamba’, ‘Mabeberu’, ‘Kimanzi’, ‘Si Kosa Lako Unavunja Utu’, ‘Mpenzi Wee’ na ‘Maisha Matamu’. Bendi iliendelea kuwa na umaarufu mkubwa hadi kwenye miaka ya 1970.


  Ama kweli kizuri hakidumu, usemi huo ulijidhihirisha pale mwanamuziki huyo alipopata ajali Novemba 19, 1965 na kufariki dunia. Chanzo cha ajali kilielezwa kuwa taa za gari lake zilizimika ghafla akiwa katika mwendo. Gari hilo lilitoka nje ya barabara na yeye kutupwa nje, akapasuka kibofu na kufariki siku hiyo hiyo.
  Juma Kilaza aliendelea kupiga muziki katika bendi hiyo akishindana kwa kiasi kikubwa na hasimu wake Mbaraka Mwinshehe. Mungu azilaze roho zao pahala pema peponi, amina.
 
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba 0784 331200, 0767 331200 na 0713 331200.

2038 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!