Ni vigumu kutokomeza ukeketaji

Vita dhidi ya ukeketaji kwa wasichana na kinamama Wilaya ya Tarime mkoani Mara, inaweza kuwa ngumu kwa sababu mangariba huchukulia jambo hilo kama ajira licha ya kuwa ni ya msimu tu, likifanyika kila Desemba.
Taarifa kwamba wanafaidika kiuchumi imetolewa na mangariba hao waliofanya mahojiano na mwandishi wa makala hii hivi karibuni ambako, pamoja na mambo mengine, alitaka kufahamu sababu zao za kuendelea na kazi hiyo.


“Sisi ni wajane,” anasema mmoja wa mangariba hao,  Wankuru Samwel Mang’embe, na kuongeza: “Tukifanya kazi hii, ndiyo tunapata ujira ambao hutusaidia kulea familia, sasa utaniambiaje niache ungariba? Hii ni mila na ajira.”
Wankuru aliyezaliwa miaka 43 iliyopita katika Kijiji cha Borega, Kata ya Ganyange katika Ukoo wa Wanyabasi, anasema kwamba alianza kazi hiyo mwaka 2002 kwa kurithi kutoka mama yake.


Anasema kwamba ukiacha fedha ya matumizi ya kawaida ya nyumbani, kuna mangariba wanaovuna kiasi kikubwa kinachotosha kujenga nyumba za familia zao, kusomesha hali kadhalika kumiliki mifugo.
Ngariba huyo anadai kwamba hawaogopi polisi licha ya vitisho wanavyopata mara kwa mara, kwani wanalindwa na wazee wa mizimu na ikitokea wanakosea basi huadhibiwa kwa mujibu wa mila na desturi.


Anasema kwamba ni makosa makubwa kumkeketa binti mjamzito kwenye eneo la kukeketea wasichana wengine, kwani binti wa aina hiyo hutakiwa kukeketwa nyumbani nyuma ya ghala la kuhifadhi chakula.
Anasema kwamba wanavuna pesa nyingi kwa msichana ambaye humshika mkono ngariba au kutikisa mguu kabla ya kumaliza kazi yake na wakati mwingine hutozwa faini ya kulipa ng’ombe.


Wankuru anasema amefaidika kwa kusomesha watoto na sambamba na kumwozesha kijana wake kwa mahari ya Sh. 500,000 na kwa mwaka huu 2015, hatahangaika kununua mboga na unga kwani wasichana huwapelekea unga, nyama pamoja na togwa inayofahamika kwa jina la busara.
Ngariba mwingine, Nyabanosi Magoiga Nyankorongo, mwenye umri wa miaka 82, kwa sasa anasema kwamba ni ngumu kwake kuacha kazi hiyo licha ya kufungwa jela na kumaliza kifungo mwaka jana.


Ngarika huyo mzaliwa wa Kijiji cha Tagota, Kata mpya ya Kenyamonyori katika ukoo wa Watimbaru, alianza kazi hiyo miaka 20 iliyopita na kukamatwa mwaka 2010 na Jeshi la Polisi chini ya RPC Constantine Massawe na kufikishwa mahakamani.
Alifikishwa kortini na kutiwa hatiani na  Hakimu Yusto Luboroga kwenda jela miaka 30 na kufanya kazi ngumu sambamba na kulipa faini ya Sh. 200,000. Lakini alikata rufaa na kuachiwa huru baada ya mwaka mmoja.


Mara baada ya kutoka jela, alitangaza kutoendelea na kazi hiyo, lakini ambayo imemfanya ajenge nyumba imara ya bati kwani awali aliishi kwenye nyumba za nyasi na wajukuu wake yatima.
Pia yumo Florence (Rhobi) Mwita Nyaigega, aliyezaliwa mwaka 1974 katika ukoo wa Wasweta, Kata ya Nyandoto, anayesema kuwa alianza kazi hiyo mwaka 2007 aliyorithi kutoka kwa bibi yake.


Anasema kwamba kwa kila msichana anavuna Sh. 5,000; unga, nyama pamoja na busara (togwa). Anasema kwamba faida nyingine ni kununua mifugo ambayo baadhi imeibwa na watu wasiojulikana.
Kazi ya ungariba imekuwa ni ya kurithi katika koo mbalimbali wilayani Tarime, kama vile Wairege na Wanyabasi ambayo ni kubwa yenye mangariba kama vile Wankuru Mag’embe, Mgosi  Rioba Gweswa pamoja na Nyakumusi Siruri, aliyestaafu mwaka jana.


Pia wamo wa ukoo wa Watimbaru wenye mangariba Nyabanosi Magoiga Nyankorongo, Motatiro Muhagachi pamoja na Ghati Iritega.
Mwandishi wa makala hii ni mkazi wa Tarime mkoani Mara, ambaye amefanya kazi hiyo kwa ufadhili wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa).
 
0758 997070