Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina,  Injinia Arcard Mutalemwa (Mwenye
shati jeupe), kufanya tathmini ili kujua  uwekezaji uliopo katika Ranchi
za Taifa (NARCO) akikabidhi  ripoti ya kazi hiyo jana  kwa
Waziri Mpina na viongozi wakuu wa Wizara hiyo. Mhe. (Picha na John
Mapepele)
 Picha ya pamoja  baina ya Kamati iliyoundwa
na Waziri wa  Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina (mwenye suti nyeusi
na miwani) kufanya tathmini ili kujua  uwekezaji uliopo katika Ranchi
za Taifa (NARCO) kushoto kwake ni  Injinia Arcard Mutalemwa, Mwenyekiti
wa Kamati hiyo, Dkt. Maria Mashingo Katibu Mkuu wa Mifugo, kulia ni
Naibu Waziri Abdalah Ulega na Mtendaji Mkuu wa NARCO,Profesa  Philemoni
Wambura (Picha na John Mapepele)
 Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina,  Injinia Arcard Mutalemwa
(aliyesimama),
kufanya tathmini ili kujua  uwekezaji uliopo katika Ranchi za
Taifa (NARCO)
akisoma na kuwasilisha  ripoti ya kazi hiyo jana  kwa Waziri
Mpina na Viongozi wakuu wa Wizara hiyo.(Picha na John
Mapepele)
Mtendaji Mkuu wa NARCO,Profesa  Philemoni Wambura
akichangia hoja kwa Waziri wa  Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina,
kwenye kikao cha kukabidhi taarifa ya kamati ya kufanya tathmini
ya uwekezaji
uliopo katika Ranchi za Taifa (NARCO) jana.(Picha na John
Mapepele)
 

WAZIRI wa Mifugo na
Uvuvi, Luhaga Mpina amepangua
hoja zilizotolewa na wabunge kuhusu namna Wizara yake inavyopambana
kutokomeza uvuvi haramu ili kunusuru  kupotea kabisa kwa samaki
na kuchochea kufa kwa viwanda vya  samaki na kusababisha kupungua
kwa ajira nchini.

Waziri Mpina alitoa
ufafanuzi huo wakati akijibu
hoja za baadhi ya wabunge bungeni  Mjini Dodoma ambao walikosoa
hatua zinazochukuliwa na Wizara hiyo katika kupambana na uvuvi haramu
hususan katika Ziwa Victoria pamoja na kudhitibi utoroshaji wa samaki
na mazao yake nje ya nchi.

 “Mimi na Wizara
yangu tutahakikisha hili
tunalisimamia kwa nguvu zote, hizi ni rasilimali za taifa na haziwezi
kugawanwa kwa ukanda, rasilimali hizi zinapashwa kunufaisha nchi nzima
kwa hiyo kama Wizara inayosimamia Sheria zilizopitishwa na Bunge hili
tutahakikisha kwamba hakuna kabisa uvuvi haramu katika nchi yetu, hakuna
mfanyabishara atakayejihusisha na kuuza wala kusambaza nyavu haramu,
hakuna kiwanda kitakachochakata samaki wasioruhusiwa, hakuna mtu yoyote
atakayevua kwa vyavu haramu wala kufanya biashara haramu ya mazao ya
uvuvi ni lazima mali zetu tuzilinde kwa nguvu zote”
alisisitiza.

Akifafanua hoja hiyo
alisema  Wizara  yake
katika kupambana  na suala la uvuvi haramu na utoroshaji wa mazao
ya uvuvi inatumia Sheria  ya Uvuvi namba 22 ya Mwaka 2003 pamoja
na kanuni zake za mwaka 2009, Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu ya Mwaka
1998, na marekebisho yake  ya mwaka 2007,Sheria ya Mazingira namba
20 ya Mwaka 2004, Sheria ya Uhujumu Uchumi (Economic and organized
crime Act Cap 200 CE 2002 as amended  by Act no 3 of 2016) na Sheria
ya  Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu namba 29 ya mwaka
1994. 

Wabunge hao waliokuwa
wakichangia taarifa ya Kamati
ya Kilimo, Mifugo na Maji ni pamoja na Joseph Msukuma wa Geita Vijijini,
Constantine Kanyasu na Geita mjini na Dk Raphael Chegeni wa
Busega

Mpina alisema kwa
mujibu wa tafiti zilizofanywa na
Wizara yake samaki aina ya Sangara wanaoruhusiwa kuvuliwa wenye urefu
wa kati ya sentimita 50 mpaka 85 wamebaki asilimia 3 samaki wazazi wamebaki
asilimia 0.4 samaki wachanga wasioruhusiwa kuvuliwa chini ya sentimita
50 ni asilimia 96.6  kwa mantiki hiyo hatuna samaki wanaofaa kuvuliwa
katika Ziwa Victoria.

Alisema Kamati hiyo
imezungumzia juu ya viwanda vya
samaki kufungwa ambapo kabla uvuvi haramu haujashamiri kulikuwa na viwanda
13  vilivyokuwa na uwezo wa kuchakata tani 1, 065 na kutoa ajira 4,000
katika ukanda wa Ziwa Victoria lakini kutokana na kuendelea na uvuvi
haramu vimepungua na kubaki 8 vyenye uwezo wa kuzalisha tani 171 na
kusababisha kubaki na ajira 2,000 tu.

Mpina aliongeza kuwa
Kamati ya Bunge imetoa msukumo
mkubwa kwa Wizara hiyo kupitia katika ukurasa wa 32 wa taarifa yao kwamba
Serikali iongeze bidii katika kupambana na uvuvi haramu sambamba na
kuhakikisha wale wanaotorosha samaki na mazao yake wanawadhibitiwa
vilivyo.

Aidha, Mpina alisema
katika operesheni hiyo, maamuzi
hayafanywi na mtu mmoja katika kutafsiri mambo mbalimbali ikiwa ya
vipimo vya nyavu za ngazi mbili au tatu badala yake timu nzima ya wataalamu
inachambua na kuishauri Serikali hatua zinazopaswa
kuchukuliwa.

Aliongeza kwamba
Kamati hiyo imejuisha Maafisa Uvuvi,
Maafisa kutoka Baraza la Mazingira la Taifa(NEMC), Jeshi la Polisi,Ofisi
ya Rais, Tamisemi, Idara ya Uvuvi .

“Lakini mheshimiwa
Mwenyekiti mambo tuliyoyaona
kwenye operesheni hii yanatisha zipo gari za waheshimiwa wabunge tumezikamata
na samaki haramu,wapo wenyeviti wa halmashauri ,wapo wenyeviti wa vijiji,
madiwani, watendaji wa Serikali  tumewasimamisha kazi  kwa
hiyo katika
operesheni hiyo tulipokagua viwanda tukakuta viwanda vyote  vinachata
samaki wasioruhusiwa, tumekamata viwanda vya nyavu
haramu”alisema.

Aidha baadhi ya
Wabunge akiwemo  Mbunge wa Kishapu,
Suleiman Nchambi na Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba kwa nyakati
tofauti walimtaka Waziri Mpina kutaja hadharani majina ya wabunge hao
wanaotuhumiwa kufadhili uvuvi haramu. 

“ Waziri amesema
katika shughuli hii ya kutokomeza
uvuvi haramu kuna magari ya wabunge yamekamatwa na samaki ambao wamevuliwa
kiharamu,kuna wenyeviti wa halmashauri ambao magari yao yamekamatwa
na samaki ambao wamevuliwa kiharamu hawa watu ni wabaya wanaangamiza
Taifa letu nakuomba mheshimiwa Waziri uwataje watu hawa ili tuwalaani”
alisema Serukamba.

Aidha Waziri Mpina
alisema kwa sasa timu yake inakamilisha
taarifa ya awamu ya kwanza ya operesheni Sangara mwaka 2018 inayoendelea
ambayo iko mbioni kumaliza na kwamba ataifikisha mbele ya kamati na
baadae taarifa hiyo itaingia bungeni.

Kufuatia mjadala
huo,Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan
Zungu aliwataka wabunge kuacha kumpa taarifa Waziri Mpina kwani tayari
ameshaeleza kuwa taarifa ikikamilika ataiwasilisha kwenye
kamati. 

“Waziri ameeleza
vizuri ,tuhuma za watu amezitaja
taarifa inaandaliwa itawasilishwa kwenye muda muafaka end of the story
sasa ninyi mnakataa nini hatupigi daku hapa kuanzia sasa hakuna taarifa
yoyote mhe Waziri maliza..”alisema Zungu.

Aidha Waziri Mpina
alisema Serikali imekamata zaidi
ya kilo 133,000 ya samaki aina ya kayabo na dagaa zikitoroshwa kwenda
Rwanda, Burundi, Kongo na Kenya, pia wamekamatwa samaki wachanga kilo
73,000 ambazo rasilimali hizi zote za nchi zinachezewa kwa kiasi huku
operesheni hiyo ikiwakamata hadi raia wa kigeni kutoka Rwanda, Kenya
na Burundi wakiwa ndani ya visiwa wakishiriki uvuvi na kununua samaki
jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Pia walikamata viwanda
vya mabondo 22 vinafanya biashara
lakini vilivyokuwa na leseni halali ni viwili tu hivyo Serikali ikisema
inapambana na uvuvi haramu inapambana kweli kweli huku akisisitiza kuwa
operesheni hiyo haina mwisho hadi uvuvi haramu utakapomaliza hapa
nchini

Kuhusu Uvuvi wa Bahari
Kuu  Waziri Mpina alisema tayari
Serikali imeshapata meli ya kufanya doria kwani ilizoeleka meli hizo
zinakuja kuvua na kuondoka huku taifa letu linaachwa halina
chochote.

“Tunashindwa kukusanya
chochote na ndio maana kwa
mara ya kwanza tumekamata meli na kuipiga faini  milioni 770 nilitegemea
Bunge hili litapongeza jitihada hizi kubwa za Wizara ambazo zinalinda
rasilimali hizi leo hii mkakati wa kulinda uvuvi wa bahari kuu tutazikagua
meli zote zikiwa zinavua huko huko hakuna mtu atakayeondoka kwenye maji
ya Tanzania akiwa amebeba rasilimali za
watanzania”alisema. 

Alisema Serikali
itaongeza meli mbili za doria katika
ili kuhakikisha uvuvi wa bahari kuu pamoja na bahari nzima unalindwa
kwa nguvu zote na kuhakikisha kwamba rasilimali  nchini mwetu zinanufaisha
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.

“Hataruhusiwa mtu
yoyote na niseme Mheshimiwa Mwenyekiti
kama mtu atajishughulisha na uvuvi haramu aache mimi Mpina hata Mzee
Mpina mwenyewe ninyi doria mkamateni kama anajishughulisha na uvuvi
haramu hatuwezi kuongelea kwa maneno mepesi mambo makubwa ya mstakabali
wa taifa letu’alisema.

Waziri Mpina
alisisitiza  timu yake ya
doria kufanya kazi kwa weredi kwa kufuata sheria  na kutokumwonea
mtu yeyote wakati wa operesheni hii.

Aidha alisema katika
ulinzi wa rasilimali za taifa
Serikali ni walinzi tu hivyo mlinzi ukikutwa mlango wa tajiri umevunjwa
atakuwa na shida .

“Mimi ni kibarua wenu
kazi yangu ni kuhakikisha
katika wizara mliyonipa rasilimali zinalindwa kwa nguvu zote na kazi
hiyo mimi na wizara yangu tutaifanya usiku na mchana lakini nasema kama
kuna hoja ya msingi wabunge wasituhumu kwa ujumla yawezekana kuna mtendaji
akakosea katika kuchukua hatua, unasema katika eneo fulani katika kijiji
fulani kuna jambo hili na hili limefanyika Mpina lishughulikie hata
sasa hivi ukiniletea nitafanyia kazi na kuchukua hatua mara moja
”alisema.

Alisema rasilimali za
taifa zimetoroshwa vya kutosha
na kwamba Bunge  muda wote limekuwa likilia juu ya makusanyo
hafifu  yatokanayo
na uvuvi ambapo Serikali inakusanya wastani wa bilioni 20 tu ukiwaondoa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hivyo  ni wakati sasa wa Bunge
kuisaidia
Wizara kuinua sekta hiyo .

Kuhusu
Ranchi za Taifa (NARCO) Waziri Mpina alisema
Kamati ilishauri Serikali ifanye tathmini ili kujua  uwekezaji uliopo
katika ranchi hizo unatija  ili ije na  mapendekezo sahihi
ya namna bora
ya kuwekeza katika ranchi hizo ambapo alisema tayari Wizara imeshaunda
kamati hiyo inayoongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu Mstaafu wa DAWASA, Arcard
Mutalemwa
.

By Jamhuri